
FAMILIA ya aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga inakabiliwa na mtanziko wa kiitifaki huku Rais William Ruto na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta wakitarajiwa kuhudhuria maadhimisho ya mwaka mmoja tangu kifo cha Raila, uwanjani Migwena, eneobunge la Bondo hapo Alhamisi.
Viongozi hao wawili wamekuwa wakishambuliana hadharani, hali inayozua hofu kwamba hafla hiyo inaweza kugeuka uwanja wa mzozo wa kisiasa.
Taifa imebaini kuwa baadhi ya jamaa wa familia walitaka Bw Kenyatta awe mgeni wa heshima, huku wengine wakipinga pendekezo hilo.
Mwaliko wake ulitolewa kwa matarajio kwamba Rais Ruto hangekuwepo baada ya kuzindua makavazi ya Raila mnamo Jumatano. Hata hivyo, Rais Ruto anatarajiwa kuhudhuria hafla hiyo ya Alhamisi.
Msemaji wa mawasiliano wa Bw Kenyatta, Kanze Dena-Mararo, naye alisema kuhudhuria kwake “bado hakujathibitishwa”
Jamaa wa familia ya Jaramogi alisema baadhi ya jamaa waliambiwa kuwa Bw Kenyatta angekuwa mgeni rasmi.
“Hatujui hilo linamwacha Rais William Ruto katika nafasi gani, kwa sababu hakuna anayeweza kuhutubia baada ya Rais katika hafla. Hatujui kama naye atahudhuria,” akasema.
Mbunge mmoja wa ODM alisema Bw Kenyatta hawezi kuwa mgeni rasmi katika hafla ambayo rais ambaye yupo madarakani anahudhuria.
Mvutano huo unajiri huku familia ikionekana kugawanyika kuhusu mwelekeo wa kisiasa wa nchi.
Raila Junior, anayetaka kuwania kiti cha ubunge cha Kibra, ameunga mkono Serikali Jumuishi na kuidhinisha azma ya Rais Ruto kuwania muhula wa pili. Anashirikiana na ami yake Kiongozi wa ODM, Dkt Oburu Oginga.
Hata hivyo, dada yake Winnie Odinga, mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), na Mwakilishi wa Kike wa Kisumu Ruth Odinga wamekuwa wakikosoa namna ODM inavyoendeshwa baada ya kifo cha Raila.
Winnie anatarajiwa kujiunga rasmi na vuguvugu la Linda Mwananchi linaloongozwa na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna, ambaye ni kati ya viongozi wa upinzani wanaotarajiwa kuhudhuria hafla hiyo.
Mama Ida Odinga, ambaye ni balozi wa Kenya na Mwakilishi wa Kudumu katika Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP), amesisitiza kuwa mumewe hakuwa na maadui wa kudumu.
“Waliokuwa wapinzani wake, wakijua siasa za Kenya, huenda wanamfahamu Raila vizuri kwa sababu mwishowe wote huungana, na mnakaribishwa. Huyo ndiye Raila,” akasema Jumatano wiki jana.
Jamaa mwingine wa familia alikiri kuwa kuna mvutano kuhusu mwaliko wa Bw Kenyatta.
“Kamati inapaswa kutoa uamuzi wa mwisho. Kuna wanaotaka hafla hiyo iachwe kwa upinzani, lakini kwa kuwa hii ndiyo sherehe kuu, Rais Ruto anatarajiwa kuhudhuria,” akasema.
“Unawezaje kumzuia Rais kuhudhuria hafla kwa sababu ya maslahi ya kisiasa? Huu si mkutano wa kisiasa, bali ni hafla ya kuwakutanisha wote waliompenda Baba. Hakuna anayepaswa kuogopa kushiriki jukwaa na mwingine kwa sababu ya uhasama wa kisiasa,” akaongeza.
Naibu wa Baraza la Wazee wa Jamii ya Waluo, Ker James Ayaga, alimtaka Dkt Oginga kuhakikisha familia ya Jaramogi ina umoja.
“Yote yanayotokea katika familia ya Odinga ni jukumu la Dkt Oginga kama mwana mkubwa wa Jaramogi kuhakikisha anaunganisha familia,” akasema Bw Ayaga.
Alimtaka aketi na wanafamilia wote, akiwemo Ida, ili wazungumze kwa sauti moja. Alisema umoja ndio urithi muhimu wa Jaramogi na Raila.
Winnie, akizungumza katika hafla ya wiki iliyopita, alisema watu wa misimamo tofauti ya kisiasa, makabila na mataifa jirani wamealikwa kuadhimisha urithi wa babake. “Tunaweza kuwa na misimamo tofauti ya kisiasa na kutokubaliana kuhusu mwelekeo wa nchi yetu, lakini mnakaribishwa hapa. Hakuna anayetakiwa kuacha imani yake mlangoni,” akasema.
Aliwataka wanasiasa kutogeuza Oktoba 15 kuwa mashindano ya kisiasa.
“Sisi kama familia, tunatoa wito wa kusitishwa kwa mivutano ya kisiasa kwa heshima yake. Tafadhali, Oktoba 15 iwe siku ya kumkumbuka na kusherehekea maisha yake,” alisema.
Kwa upande wake, Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa, Junet Mohammed, alisema kamati inayoongozwa na Prof Adams Oloo ndiyo itasimamia hafla ya Alhamisi, huku ODM ikihusika na mikutano ya chama ya kumuenzi Raila.
“Kamati ndiyo inayosimamia kila kitu. Sisi tunasimamia tu shughuli za chama za kusherehekea maisha ya kiongozi wetu aliyeaga dunia,” akasema Prof Oloo jana alisema alikuwa anaingia kikaoni, hivyo mkuu wake wa mawasiliano angetuma taarifa lakini hakuwa amefanya hivyo kufikia wakati wa kuchapisha habari hizi.
from Taifa Leo https://ift.tt/8AfjUQd
via IFTTT