
Raila Odinga alikuwa zaidi ya kiongozi wa chama cha ODM. Kwa wanasiasa waliotembea naye kwa miaka mingi, alikuwa mshauri, rafiki, mzalendo na mwavuli uliowapa nafasi watu wenye misimamo tofauti kufanya kazi pamoja.
Mwaka mmoja baada ya kifo chake, viongozi waliokuwa karibu naye wanakumbuka ujasiri wake, uwezo wake wa kujenga miungano na alivyoshawishi mijadala ya kisiasa na kuathiri mwelekeo wa serikali.
Waziri wa Kawi Opiyo Wandayi anasema kifo cha Raila kilikuwa pigo kubwa kwake, kwani alipoteza mtu aliyekuwa amesafiri naye kwa miaka mingi kisiasa.
Wandayi alipokea habari za kifo cha Raila asubuhi ya Oktoba 15, 2025, akiwa ndani ya ndege kuelekea Kitui kuungana na Rais William Ruto katika ziara ya maendeleo.
Alipigiwa simu na mtu aliyewafahamu wote wawili, kisha akapigiwa na Seneta Oburu Oginga, aliyethibitisha habari hizo za kusikitisha.
Wandayi anasema Raila hakuwa tu kiongozi wa chama, bali pia rafiki, mshauri na dira yake ya kisiasa. Anakumbuka kuwa alipoamua kujiunga na Baraza la Mawaziri la Rais Ruto Agosti 2024, alifanya hivyo akiwa na imani kuwa Raila alikuwa amemuunga mkono.
Uamuzi huo ulimfanya aachane na wadhifa wa Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa, ambao ulimpa nafasi muhimu ya kuongoza upinzani bungeni.
Kwa Wandayi, hatua hiyo ilikuwa ishara ya imani ambayo Raila alikuwa nayo kwake.
Anasema kifo cha Raila kilifichua changamoto ya urithi wa kisiasa ndani ya ODM, huku viongozi wakishindania nafasi ya kuongoza chama.
“Raila hakuwa mwanasiasa wa kawaida. Alikuwa na uwezo wa kusoma mikondo ya kisiasa, kuweka ajenda ya taifa na, muhimu zaidi, kujenga miungano,” anasema Wandayi.
Kwa upande wake, Waziri wa Fedha Kitaifa John Mbadi anakumbuka mazungumzo yake ya mwisho na Raila katika Nairobi Club, siku chache kabla ya kiongozi huyo kusafiri kwenda India kwa matibabu.
Mazungumzo hayo yalihudhuriwa pia na Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa Junet Mohamed na aliyekuwa kamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).
Mbadi alikuwa amewasilisha hali ya uchumi katika mkutano wa mwisho wa wabunge uliohudhuriwa na Raila. Walikutana tena kujadili uchumi na fedha za kaunti, huku Raila akimtaka Mbadi kushauriana na Profesa Hiroyuki Hino kuhusu madeni ya nchi.
“Hakikisha Ruto anafanikiwa, nasi tutakusaidia,” Mbadi anakumbuka Raila akimwambia.
Mbadi anasema Raila alitaka Rais Ruto afanikiwe katika mipango yake, ikiwemo Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA) na mradi wa nyumba za gharama nafuu.
Anamtaja Raila kama mzalendo aliyekuwa tayari kuweka kando azma yake binafsi kwa maslahi ya nchi. Pia alikosoa serikali ikikosea na kuisifu ikifanya jambo linalofaa.
Hata hivyo, viongozi hao wanakiri kuwa ODM inakabiliwa na changamoto ya kudumisha umoja bila kiongozi huyo. Mbadi anataka viongozi washauriane zaidi na kuhakikisha chaguzi za mchujo zinafanyika kwa uwazi.
Wandayi anasema chama kinapaswa kuimarisha taasisi zake, kuheshimu maoni tofauti na kuzuia azma za kibinafsi kusigeuka kikwazo cha maendeleo.
Kwao, urithi wa Raila hauishii katika ODM. Maisha yake yalihusishwa na mapambano ya demokrasia ya vyama vingi, mageuzi ya Katiba, ugatuzi na uhuru wa kisiasa.
Ingawa hayupo tena, Wandayi anasema kizazi cha sasa kitahukumiwa kwa namna kitakavyotumia nafasi ya kisiasa aliyoisaidia kuunda.
from Taifa Leo https://ift.tt/Qh31JUr
via
IFTTT