Ebola ilivyoingia Kenya licha ya tahadhari mipakani

BAADA ya kuchukua tahadhari kwa miezi kadhaa,  Wizara ya Afya jana ilithibitisha kisa cha kwanza cha Ebola aina ya Bundibugyo nchini Kenya. Wizara ilisema mgonjwa huyo aliyekuwa raia wa Kenya alifariki Jumatatu usiku na hatua zimechukuliwa kwa kuzingatia taratibu za kiafya. Waziri wa Afya Aden Duale alisema Jumanne kuwa mwanamume huyo alikuwa ameishi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kwa miaka saba, ambako aliugua takriban mwezi mmoja uliopita na kutibiwa katika hospitali kadhaa. Mgonjwa huyo alisafiri kwa barabara kutoka DRC hadi Kampala, Uganda, kabla ya kupanda ndege ya Jambojet 8523 kuelekea Nairobi. Alifika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) saa saba mchana Jumamosi, Oktoba 3, na kufanyiwa ukaguzi wa kawaida wa afya katika kituo cha afya cha uwanja huo kabla ya kupitia taratibu za uhamiaji. Jamaa na rafiki walimchukua JKIA kwa gari aina ya Toyota Fielder na kumpeleka katika hospitali moja jijini Nairobi, ambako alitengwa haraka katika chumba maalum katika kitengo cha dharura kabla ya kuhamishiwa kituo cha kutengwa wagonjwa cha East Wing. Alifika hospitalini akiwa na homa, baridi, uchovu mwingi, udhaifu, maumivu ya misuli, maumivu wakati wa kumeza, maumivu ya koo na kutokwa na damu chini ya ngozi katika maeneo aliyodungwa sindano. Madaktari walishuku alikuwa na homa ya virusi inayosababisha kutokwa na damu kutokana na dalili na historia yake ya safari nchini DRC. Sampuli zake zilipimwa katika Maabara ya Kitaifa ya Virusi na maabara ya Kenya Medical Research Institute (KEMRI), na zote zikathibitisha kuwa alikuwa na Ebola aina ya Bundibugyo. Mgonjwa huyo alipatiwa matibabu ya kumsaidia, lakini alifariki. Mazishi yake yalipangwa kufanyika Jumanne kwa kuzingatia taratibu salama na zenye heshima za mazishi ya waathiriwa wa Ebola. Wizara imetambua watu 28 waliowasiliana na marehemu, wakiwemo jamaa na wahudumu wa afya waliomhudumia. Duale alisema pia abiria 23 na wahudumu wanne waliokuwa katika ndege moja na marehemu wanafuatiliwa huku mipango ya kuwaweka walio katika hatari karantini ikiendelea. “Kenya imekuwa katika hali ya tahadhari ya juu tangu mlipuko huu ulipoanza Mei 2026,” alisema Duale. Kufikia Jumanne, Wizara ilikuwa imewapima wasafiri 652,584 na kuchunguza sampuli 267 katika maabara tano. Aidha, wahudumu 4,971 wa afya katika ngazi ya kitaifa na kaunti wamefunzwa kuhusu kinga na udhibiti wa Ebola. “Ni kipimo kimoja pekee ambacho kimepatikana kuwa cha Ebola,” taarifa ya Wizara ilisema. Duale aliwataka Wakenya kutokuwa na hofu, akisema mifumo yote ipo tayari kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo. Aliwashauri wananchi kunawa mikono mara kwa mara, kutumia dawa za kusafisha mikono na kuepuka mawasiliano ya karibu na wagonjwa wanaotoka katika nchi zilizo na maambukizi. Wananchi wenye dalili wanashauriwa kutafuta matibabu katika vituo vya afya vinavyotambuliwa na kutoa taarifa kuhusu wagonjwa wanaowajua. Wizara pia imewaagiza wahudumu wa afya kuzingatia viwango vya juu vya kuzuia na kudhibiti maambukizi. Wananchi wanaweza kupata taarifa kupitia majukwaa rasmi ya Wizara au kupiga simu ya bila malipo 719.  

from Taifa Leo https://ift.tt/NzkYepG
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post