
KINARA wa Wiper, Kalonzo Musyoka na wandani wake jana walisaka uungwaji mkono kutoka kwa aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua, mirengo hiyo miwili ikiahidi kushirikiana kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.
Hata hivyo, wakati wa mazungumzo kati ya wawili hao, utata wa lini upinzani utatangaza mgombea mmoja wa urais ulitawala mazungumzo kati yao yaliyoandaliwa nyumbani kwake Wamunyoro, Nyeri.
Duru ziliarifu kuwa mrengo wa Bw Musyoka ulipendekeza mgombea huyo atangazwe kufikia Desemba mwaka huu ili apate muda wa kutafuta rasilimali na kujenga mitandao ya kampeni ndani na nje ya nchi.
Hata hivyo, Bw Gachagua na washirika wake walitaka mchakato huo uahirishwe hadi miezi michache kabla ya uchaguzi wa Agosti 10, 2027. Wana hofu kuwa Rais William Ruto anaweza kuwashawishi baadhi ya viongozi wa upinzani kujiondoa ikiwa mgombea urais atatajwa mapema.
Seneta wa Kitui, Enoch Wambua alisema mkutano huo haukuafikiana kuhusu tarehe kamili, kwa kuwa upinzani unajumuisha washirika wengi.
“Hata hivyo, wazungumzaji katika mkutano huo walitambua kuwa Wakenya wanazidi kukosa subira kutokana na kuchelewa kutangazwa kwa mgombea wetu wa urais,” akasema Bw Wambua.
“Tunapoendelea kujenga muungano imara, huenda zawadi ya Krismasi ikawa kutangazwa kwa mgombea huyo,” akaongeza. Hata hivyo, alisema uamuzi wa mwisho uko mikononi mwa viongozi wakuu wa vyama.
Mbunge wa Gatanga Edward Muriu na mwenzake wa Embakasi ya Kati, Benjamin Gathiru, maarufu kama Mejja Donk, walisema upinzani unahitaji muda zaidi kabla ya kumchagua mgombeaji.
Bw Muriu alisema wamekubaliana kurasimisha ushirikiano wao kwa kutia saini mkataba, kabla ya kuunda muungano wa kisiasa.Bw Gathiru alionya kuwa kutangaza mgombeaji mapema kunaweza kumpa Rais Ruto nafasi ya kuvuruga upinzani na kuwadhamini wagombeaji miongoni mwao.
“Tumekubaliana kuwa vyama tanzu vinapaswa kuheshimiana. Pia tumewapa viongozi wakuu ruhusa ya kuzungumza na kuamua kuhusu mgombea,” akasema
“Lakini mchakato huo haupaswi kuharakishwa. Tunajua Ruto anaweza kufanya nini. Anaweza kufadhili baadhi ya viongozi wajiondoe na kuwania urais,” akaongeza.
Kiongozi wa People’s Party of Kenya (PPK) , Ndindi Nyoro alisema mazungumzo yanahitaji muda ili kupata mgombea anayefaa kukabiliana na changamoto za nchi.
“Tunapaswa kuangalia hali ya nchi, kisha tuamue ni nani katika mrengo wetu ana uwezo zaidi wa kukabiliana na changamoto hizo. Tunatumai mchakato utakuwa wa haki na utazingatia sifa,” akasema Bw Nyoro. Alisema chama chake kiko tayari kumuunga mkono mgombeaji atakayechaguliwa kupitia maridhiano.
Bw Musyoka aliandamana na Bw Wambua, Gavana wa Makueni Mutula Kilonzo na mwenzake wa Machakos Wavinya Ndeti, miongoni mwa viongozi wengine.
Bw Gachagua alihudhuria akiwa na Bw Muriu, Seneta wa Nyandarua John Methu, Mbunge wa Kipipiri Wanjiku Muhia na Seneta wa Kiambu Karungo wa Thang’wa.
Bw Wambua alisema Musyoka na Gachagua walifanya mazungumzo ya kirafiki kuhusu mustakabali wa nchi.
“Viongozi hao wawili wamejitolea kufanya kazi pamoja, kuunganisha wafuasi wao na kuhakikisha azma ya kumfanya Ruto kuwa rais wa muhula mmoja inatimia Agosti 10, 2027,” akasema
Bw Methu alisema DCP na Wiper zimekubaliana kufanya kazi kama vyama tanzu na kuendelea kutafuta njia ya kumpata mgombea mmoja wa urais.
Viongozi hao wanataka kufikia makubaliano yatakayowawezesha kukabiliana na Rais Ruto katika uchaguzi ujao.
Mkutano wa jana ulifanyika wiki moja baada ya Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna kumtembelea Gachagua nyumbani kwake pindi alipotoka Amerika.
Changamoto zinazokabili upinzani zinafanana na zile zilizokumba muungano wa National Rainbow kabla ya uchaguzi wa 2002. Wakati huo, viongozi wa upinzani walijadiliana kwa muda mrefu kuhusu mgombea wa kumkabili Kanu, chama kilichokuwa madarakani.
Katika kitabu chake Seasons of Hope, aliyekuwa Seneta wa Kitui David Musila anakumbuka jinsi Raila Odinga alivyotatua mtanziko huo kupitia kauli maarufu ya “Kibaki Tosha” Septemba 22, 2002, miezi mitatu kabla ya uchaguzi.
“Ujumbe ulikuwa wazi; upinzani uliokuwa umeungana dhidi ya Kanu ulikuwa umejipanga. Hata hivyo, hatukuweza kupuuza umuhimu wa kutaka kujua mgombea wetu angekuwa nani. Umati ulikuwa na hamu ya kupata jibu, lakini hakuna aliyekuwa nalo,” aliandika Bw Musila.
Alisema Raila alipofikia zamu yake ya kuzungumza, alitangaza ghafla kuwa Bw Kibaki ndiye aliyefaa kuwa mgombea. Kauli hiyo ilishangiliwa na umati na kutatua mzozo wa uteuzi.
Historia inaonyesha kuwa wagombea wa urais nchini Kenya mara nyingi hutangazwa miezi michache kabla ya uchaguzi. ODM ilimteua Raila Septemba 1, 2007, huku muungano wa Cord ukimuidhinisha Disemba 22, 2012.
NASA ilimtangaza Raila Aprili 27, 2017, na Azimio La Umoja ikamuidhinisha Machi 12, 2022. Kwa upande wa Kenya Kwanza, William Ruto aliteuliwa rasmi kuwa mgombea wa UDA Machi 15, 2022.
from Taifa Leo https://ift.tt/NIdUxiL
via IFTTT