
MAADHIMISHO ya mwaka mmoja tangu kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga yalifichua mivutano kuhusu urithi wake wa kisiasa, huku wanafamilia wakionekana kuelekea katika kambi tofauti kabla ya uchaguzi mkuu wa 2027.
Katika uwanja wa Migwena, Bondo, mjane wake Ida aliwapokea viongozi kutoka makundi hasimu, binti yake Winnie akatangaza azma ya kuwania useneta wa Nairobi, huku mwanawe Raila Junior akisisitiza uaminifu wake kwa chama cha ODM.
Wakati huo huo, dadake Raila, Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Kisumu Ruth Odinga, alitishia kuondoka ODM akilalamikia kupotoka kwa chama hicho kutoka kwa misingi yake.
Hatua hizo zimeibua maswali kuhusu iwapo familia hiyo imeamua kuweka dau katika pande tofauti ili kuhifadhi ushawishi wake, au iwapo kila mmoja anafuata malengo yake binafsi.
Kuna mihimili miwili inayoibuka na kundi moja linaegemea kwa Rais William Ruto, Kiongozi wa ODM Dkt Oburu Oginga na Raila Junior, wanaounga mkono ushirikiano wa ODM na serikali.
Kundi jingine linahusisha Winnie, Ruth na vuguvugu la Linda Mwananchi linaloongozwa na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna, ambalo limepinga ushirikiano huo.
Dkt Oginga amepinga madai kuwa kufanya kazi na Ruto ni kusaliti misingi ya ODM. Anasema chama hicho lazima kihamie kutoka kutetea Katiba ya 2010 hadi kutekeleza masharti yake kuhusu usawa wa kiuchumi, ugatuzi na uadilifu wa taasisi.
“Hatuwezi kutekeleza maadili yetu ya maendeleo tukiwa pembezoni,” alisema katika hotuba yake ya maadhimisho, akisisitiza kuwa ODM inapaswa kutumia idadi ya wafuasi wake na mtandao wake wa kisiasa ili kuunda serikali ijayo.
Ushirikiano huo umewawezesha baadhi ya wanachama wa ODM kupata nyadhifa serikalini. Ida, kwa mfano, aliteuliwa kuwa balozi na mwakilishi wa kudumu wa Kenya katika Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) Februari mwaka huu.
Hata hivyo, Winnie alituma ujumbe tofauti alipotangaza kuwania useneta wa Nairobi, akionekana kuhusisha azma yake na kambi ya Sifuna.
“Edwin Sifuna anapotafuta nyadhifa nyingine, nafasi ya useneta wa Nairobi iko wazi, na ndiyo sababu nimeamua kuwania kiti hicho. Sitaenda peke yangu, nitaandamana na vijana,” akasema.
Mchangunuzi wa siasa Profesa Obora Okoth anasema kauli za Winnie na Ruth zinapaswa kuchukuliwa kwa uzito, akizitafsiri kama ishara ya kutoridhishwa kwa sehemu ya familia na ushirikiano na Ruto.
Anasema kauli ya Winnie inaashiria uwezekano wa kujiunga na Linda Mwananchi, huku akionya kuwa wanafamilia wanaowania nyadhifa za kisiasa hawataweza kutegemea jina la marehemu Raila pekee.
“Ukoo wa kisiasa iliishia kwa Raila. Mmoja au wawili wanaweza kuchaguliwa, lakini itategemea uwezo wao binafsi,” akasema.
Bi Ruth naye alionya kuwa yuko tayari kuondoka ODM ikiwa kubaki kwake kutamaanisha kusaliti misingi ya haki na demokrasia aliyotetea kaka yake.
“Ikiwa itamaanisha mimi, Ruth Odinga, kupoteza kila kitu ili kusimama na ODM, nitafanya hivyo. La sivyo, nitahamia chama kingine kwa sababu ninataka haki iendelee kuwepo nchini Kenya,” akasema.
Kauli hiyo ilizua majibu kutoka kwa naibu kiongozi wa ODM Simba Arati, aliyewaambia wanaotaka kuondoka kuwa wako huru kufanya hivyo.
Alidai kuwa baadhi yao wamenunuliwa, huku akisisitiza kuwa ODM bado ina nguvu eneo hilo.
Kwa upande wake, Raila Junior alisisitiza kuwa ODM ndicho chama alichoachiwa na baba yake. Alisema siasa za Raila zililenga kutetea wananchi wa kawaida, wanyonge, ugatuzi na umoja wa kitaifa na analenga ubunge wa Kibra kupitia ODM.
Ida, ambaye aliwataka Wakenya kudumisha maridhiano na uvumilivu, pia alionya kuhusu wanasiasa wanaotumia jina la Raila kwa manufaa yao binafsi.
“Wengi wataendelea kulitaja jina lake kwa sababu najua Wakenya walimpenda sana. Baadhi watafanya hivyo kwa mapenzi ya kweli, lakini wengine kwa kujinufaisha,” akasema.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Luo, Ker Odungi Randa, aliitaka familia kubaki katika ushirikiano na serikali ya Ruto, akisema Raila alikuwa na sababu za kuchagua njia hiyo.
“Naiomba familia ibaki imara katika serikali jumuishi alikowaachia. Wasitawanyike kwa kushawishiwa na wimbi la sasa. Nyasi zinaweza zisiwe za kijani zaidi upande mwingine,” akasema.
Kwa jumla, mivutano hii inaonyesha kuwa urithi wa Raila si suala la nani atarithi jina lake pekee, bali pia ni nani atakayefafanua mwelekeo wa kisiasa aliouacha.
Familia inaweza kuwa na nafasi katika pande tofauti kwa sasa, lakini kadri uchaguzi wa 2027 unavyokaribia, itakabiliwa na shinikizo la kuweka wazi misimamo yake.
za Winnie na Ruth zinaonyesha kutoridhishwa na njia ya sasa ya ODM, huku Dkt Oginga na Raila Junior wakisisitiza umuhimu wa kubaki ndani ya chama na kuendeleza mkondo wa ushirikiano.
from Taifa Leo https://ift.tt/7Vzp0IF
via IFTTT
Tags
TRENDING NEWS