
SERIKALI imepokea maombi 800 kutoka kwa wakulima wanaotaka kununua nyati wa kufuga kwa ajili ya kukamuliwa maziwa.
Haya yanatokea wakati ambapo Kenya ikikabiliwa na uhaba wa maziwa unaochangiwa na ukame wa mara kwa mara na gharama ya juu ya malisho ya mifugo.
Katibu katika Idara ya Ustawi wa Mifugo, Jonathan Mueke, alisema serikali imekamilisha masharti ya vyeti vya afya ya mifugo vinavyohitajika kuagiza nyati hao kutoka India na sasa inakamilisha makubaliano kuhusu bei na gharama za usafirishaji.
Mpango huo ulijadiliwa kwa mapana wakati wa Mkutano wa kwanza wa Mabadiliko ya Kilimo na Mifumo ya Chakula wa 2026, uliofanyika katika uwanja wa Jamhuri vya Shirika la Kilimo la Kenya (ASK) kuanzia Oktoba 7 hadi 9.
Rais William Ruto alimwagiza Katibu Mueke kuandaa mpango wa kuanzisha ufugaji wa nyati hao kupiga jeki sekta ya maziwa nchini.
Rais alisema wakulima wanakabiliwa na changamoto za uzalishaji kutokana na ukame na gharama kubwa ya chakula cha mifugo.
Pia alieleza wasiwasi kuhusu Kenya kutegemea bidhaa zinazoagizwa kutoka nje, zikiwemo soya na alizeti zinazotumika kutengeneza chakula cha mifugo.
Bw Mueke alisema serikali imekuwa ikishauriana na wakulima kuhusu mpango huo kwa mwaka mmoja na nusu na kuanzisha ushirikiano na India, ambayo ina uzoefu mkubwa wa kufuga nyati kwa ajili ya maziwa.
Alisema nyati hao wapatao milioni 203 wanafugwa duniani na maziwa yao yana kiwango cha mafuta kinachokaribia mara tatu ya maziwa ya ng’ombe wa kawaida.
Kiwango hicho cha mafuta huyafanya maziwa ya nyati kufaa kutengeneza bidhaa zenye thamani kubwa kama jibini, mtindi, siagi na samli.
Kenya huagiza baadhi ya bidhaa hizo kutoka nje, hivyo uzalishaji wa ndani unaweza kupunguza mtindo huo.
Serikali inalenga kuagiza nyati aina ya Murrah kutoka India, inayosifika kwa uzalishaji wa maziwa. Bei ya nyati hao nchini India inakadiriwa kuwa kati ya Sh102,572 hadi Sh410,289, kutegemea umri, afya na kiwango cha maziwa anayozalisha.
Bw Mueke alifafanua kuwa nyati wanaozungumziwa ni wa kufugwa, wala si nyati wa porini wanaopatikana Afrika.
Ujumbe wa Kenya unaojumuisha wakulima, wataalamu na waundaji sera unapanga kutembelea India Novemba kujifunza mbinu za ufugaji na uzalishaji wa kibiashara. Misri pia ina nyati milioni tano wanaofugwa kwa ajili ya maziwa.
Mbali na maziwa, nyati hao wanaweza kutoa nyama na ngozi kwa matumizi ya viwandani. Hata hivyo, mafanikio ya mpango huo yatategemea upatikanaji wa maji, chakula cha mifugo cha bei nafuu, mbinu bora za ufugaji na masoko.
from Taifa Leo https://ift.tt/gz6oShB
via IFTTT
Tags
TRENDING NEWS