Ruto kuvamia ngome ya Kalonzo na minofu tele

RAIS William Ruto anatarajiwa kuzuru ngome ya kisiasa ya kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka kuanzia Jumamosi, katika ziara ya siku nne itakayompeleka Machakos, Makueni na Kitui kuzindua miradi ya maendeleo. Bw Kalonzo ni mmoja wa wawaniaji urais katika uchaguzi mkuu wa 2027 na mkosoaji mkuu wa utawala wa Rais Ruto. Katika ziara hiyo, Rais atazindua barabara, kukagua miradi ya nyumba za gharama nafuu, kupanua usambazaji wa umeme, kuboresha upatikanaji wa maji na kutoa vyeti vya kumiliki ardhi. Ziara hiyo inajiri huku serikali ikiendelea kusisitiza kuwa maendeleo yanapaswa kugawanywa kwa usawa katika maeneo yote ya nchi, yakiwemo maeneo ambayo kwa muda mrefu yamekuwa yakilalamikia kupuuzwa katika ugavi wa miradi ya kitaifa. “Tutapeleka maendeleo katika sehemu zote za Kenya. Hakuna sehemu itakayobaki nyuma katika juhudi za kuleta usawa na kubadilisha nchi yetu,” Rais Ruto amekuwa akisisitiza. Ruto ataanza ziara yake Mbiuni, eneobunge la Mwala, kaunti ya Machakos, ambako atakagua ujenzi wa chuo cha michezo na kuzindua miradi ya maji ya Mwala inayolenga kupunguza uhaba wa maji katika eneo hilo nusu kame. Ataelekea Kako, Mbooni, kaunti ya Makueni, kuzindua barabara ya Wote-Kako-Ngoluni, ambayo inatarajiwa kurahisisha usafiri na kuwasaidia wakulima na wafanyabiashara kufikisha bidhaa zao sokoni. Pia atatoa hati za kumiliki ardhi kwa wakazi wa Ilima, katika juhudi za kutatua migogoro ya umiliki wa ardhi na changamoto zinazowakumba watu wanaoishi kama maskwota. Katika eneobunge la Kaiti, Makueni, atazindua barabara ya Kyambeke-Kyuasini-Ukia na kuidhinisha kuanza kutumika kwa barabara ya Kyambeke-Kikoko. Katika kaunti ya Kitui, atazindua barabara ya Kwa Vonza-Kanyangi-Chandula, Kitui Rural. Jumapili, Ruto atakuwa Kitui mjini, ambako ataweka jiwe la msingi la chuo cha  Mafunzo ya Utabibu Kenya Medical (KMTC) Kitui na kukagua mradi wa nyumba za gharama nafuu wa Kwa Ngendu. Pia atazindua mpango wa kusambaza umeme katika maeneo ambayo hayajaunganishwa na huduma hiyo. Jumatatu, ziara itaendelea katika maeneo mbalimbali ya Kitui na Kibwezi, Makueni. Katika Mwingi North, Rais atakagua mradi wa nyumba za gharama nafuu wa Tseikuru, kuzindua barabara ya Twimiwa-Tseikuru-Usueni na kutoa hati za umiliki wa ardhi kwa wakazi. Katika eneo la Kathekani, Kibwezi Mashariki, atazindua Shule ya Upili ya Kathekani iliyojengwa na Shirika la Reli Kenya na kuanzisha awamu nyingine ya miradi ya kuunganisha wananchi na umeme. Atazindua pia barabara ya Machinery-Kyumani-Tuberie katika Soko la Machinery, Kibwezi Mashariki, kabla ya kuelekea Kitui Magharibi kuweka jiwe la msingi la mradi wa nyumba za gharama nafuu wa Kabati. Siku ya mwisho, Jumanne, Ruto atatembelea Ngaie, Mwingi North, ambako ataweka jiwe la msingi la kiwanda cha simiti kinachotarajiwa kuunda nafasi za ajira na kuchochea shughuli za kiuchumi katika Bonde la Mui, eneo lenye makaa ya mawe. Atamalizia ziara yake Machakos kwa kuzindua mradi wa umeme na barabara ya Kagonde-Masinga-Kithyoko, Kithyoko, Masinga. Kisha atazindua barabara ya Matuu-Kyasioni-Katangi katika eneobunge la Yatta. Katika kipindi cha miaka minne iliyopita, serikali imesema imeongeza uwekezaji wa miundombinu na miradi mingine ya maendeleo Ukambani. Ruto amekuwa akisisitiza kuwa utawala wake unalenga kuhakikisha kila eneo na jamii inanufaika na uwekezaji wa umma na fursa za kiuchumi.  

from Taifa Leo https://ift.tt/WRLdfYA
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post