
SENETA wa Nairobi Edwin Sifuna ametangaza kikosi cha viongozi anaopendekeza kuongoza chama cha Linda Mwananchi Movement (LMM), akimteua aliyekuwa Gavana wa Meru Kawira Mwangaza na Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi miongoni mwa vigogo watakaokuwa na majukumu makubwa.
Sifuna alitangaza mapendekezo hayo jana wakati wa uzinduzi wa makao makuu ya chama hicho jijini Nairobi, huku viongozi wa Linda Mwananchi wakijiandaa kwa mkutano wa kitaifa wa wajumbe utakaopitisha na kuidhinisha uongozi huo.
Alisema chama hicho kinapendekeza kuwa na kiongozi mkuu na manaibu wanne, huku nafasi moja ikitengewa mwakilishi kutoka eneo la Pwani.
Mwangaza, mbunge wa Mavoko, Patrick Makau na aliyekuwa Rais wa Chama cha Wanasheria Kenya (LSK) Faith Odhiambo ni miongoni mwa waliopendekezwa kuwa manaibu wa kiongozi wa chama.
“Tumekubaliana kuwa na kiongozi wa chama na manaibu wanne. Kwa sasa, tumependekeza kuwa Kawira Mwangaza mmoja wa manaibu hao,” alisema Sifuna.
Osotsi amependekezwa kuwa mwenyekiti wa chama, akisaidiwa na aliyekuwa Mbunge wa Makadara Reuben Ndolo.
Mbunge wa Suba Kusini Caroli Omondi amependekezwa kuwa katibu mkuu, huku Pauline Njoroge akitajwa kuwa naibu wake.
Seneta wa Kisii Richard Onyonka amependekezwa kuwa mweka hazina wa kitaifa, akisaidiwa na Abigael Gikonyo.
Kari Karani amependekezwa kuwa katibu wa masuala ya maandalizi na mipango, huku Francy Kadide akipewa nafasi ya katibu wa masuala ya sheria.
Katika uongozi wa wanawake, Caroline Mayuzu amependekezwa kuongoza chama cha wanawake, huku Fredah Onduso akitajwa kuongoza vijana.
Torome Nalengoyo, aliyekuwa mwenyekiti wa zamani wa ODM Kaunti ya Narok, amependekezwa kuwa mwakilishi wa makundi madogo katika jamii.
Eunice Juma, mmoja wa waanzilishi wa chama hicho, amependekezwa kuwa katibu wa masuala ya Wakenya wanaoishi ughaibuni, huku Gilbert Shanga akitajwa kuwa katibu wa masuala ya kimataifa.
Mbunge wa Trans Nzoia George Natembeya amepewa jukumu la kusimamia kampeni za urais, huku Faith Odhiambo akipendekezwa kuwa naibu mwenyekiti wa kampeni hizo.
Seneta wa Kakamega Boni Khalwale amependekezwa kuwa katibu wa masuala ya kisiasa.
Majina hayo yatawasilishwa kwa mkutano wa kitaifa wa wajumbe ili kujadiliwa na kuidhinishwa kabla ya chama hicho kukamilisha kuunda mifumo yake ya uongozi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Sifuna alisema safari ya kuanzisha chama hicho imekuwa ngumu, akidai kuwa mikutano yao imekuwa ikivurugwa na wahuni.
Alitaja vifo vilivyotokea wakati wa mikutano yao Kitengela na Homa Bay, akisema viongozi na wafuasi wao wamepitia changamoto licha ya Kenya kuwa taifa la kidemokrasia.
Alisema chama hicho kina azma ya kuweka wananchi mbele na kuunda serikali itakayoheshimu haki za binadamu.
Sifuna pia aliahidi kupunguza matumizi ya serikali na kufuta ushuru wa nyumba siku ya kwanza watakapoingia madarakani.
Alimkosoa Rais William Ruto, akidai kuwa amekuwa akiiga sera na mawazo ya Linda Mwananchi, huku akiahidi kuwa chama hicho kitamwondoa mamlakani katika uchaguzi ujao.
Hafla hiyo ilipambwa na vinara wengine wa upinzani akiwemo kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka aliyesisitiza umuhimu wa mashauriano miongoni mwa viongozi wa upinzani kabla ya kuamua mgombea wa urais.
Kalonzo alisema katiba ya chama inahitaji NDC itakayofanyika Novemba 13 kabla ya Sifuna kutangazwa rasmi kuwa mgombea wa urais.
Alisema lengo lake kuu ni kuhakikisha Rais Ruto anakuwa kiongozi wa muhula mmoja, akionya kuwa upinzani hautafikia azma hiyo bila kuwa na mgombea mmoja.
“Kama ni mimi, basi Sifuna lazima aniunge mkono,” alisema Kalonzo, akisisitiza kuwa viongozi wanahitaji kuketi pamoja na kukubaliana.
Kwa upande wake, aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua aliwataka viongozi wa upinzani kumpa Sifuna nafasi ya kuongoza, akisema ana uwezo wa kufanya hivyo licha ya kuwa na umri wa miaka 44.
Osotsi alisema jukumu lake kama mwenyekiti litakuwa kujenga mifumo ya chama kote nchini na kuhakikisha nidhamu inadumishwa.
Alionya kuwa chama hicho kinaweza kukumbana na vurugu, lakini akasema atahakikisha wanachama wanafuata taratibu na kufanya kazi kwa umoja.
Hafla hiyo inaashiria hatua mpya kwa mrengo wa Linda Mwananchi katika juhudi za kujijenga kama chama na kujiandaa kwa uchaguzi mkuu wa 2027.
from Taifa Leo https://ift.tt/OVo9Trs
via IFTTT
Tags
TRENDING NEWS