
SENETI ya Amerika imemthibitisha mwanadiplomasia mkongwe Henry Wooster kuwa balozi mpya wa Washington nchini Kenya, hatua inayofungua njia kwa mwakilishi huyo kuanza kazi Nairobi kabla ya uchaguzi mkuu wa 2027.
Wooster alithibitishwa Septemba 30 kwa idhini ya pamoja ya Seneti, baada ya Kamati ya Seneti ya Mahusiano ya Kigeni kuidhinisha uteuzi wake.
Rekodi rasmi ya Seneti inamtaja kama mwanachama wa ngazi ya juu wa Foreign Service mwenye cheo cha Minister-Counselor.
Anachukua nafasi hiyo baada ya Meg Whitman kuondoka mwaka 2024. Tangu wakati huo, Ubalozi wa Amerika Nairobi umeongozwa na kaimu balozi huku nafasi hiyo ikiwa haina balozi aliyethibitishwa na Seneti.
Uteuzi wa Wooster unakuja wakati Kenya ikijiandaa kwa uchaguzi mkuu wa Agosti 2027, jambo ambalo lilikuwa miongoni mwa masuala makuu yaliyoibuliwa wakati wa kikao chake cha kuthibitishwa Septemba 16.
Akijibu maswali ya Seneta Chris Coons kuhusu namna Amerika itakavyoshughulikia uchaguzi huo, Wooster alisema Washington itafuatilia kwa karibu mchakato huo, huku kipaumbele chake kikiwa utulivu na kuepusha ghasia.
Alisisitiza kuwa Amerika itasimamia haki bila kuonyesha upendeleo katika uchaguzi wa Kenya.
Wooster pia alielezea Kenya kama mshirika muhimu Afrika Mashariki, akitaja ushirikiano wake katika masuala ya usalama, mapambano dhidi ya ugaidi na jukumu la maafisa wa polisi wa Kenya katika misheni ya kimataifa ya usalama nchini Haiti.
Wakati wa kikao hicho, aliulizwa kuhusu uhusiano unaokua kati ya Nairobi na Beijing na iwapo hilo linaashiria Kenya kujitenga na Washington.
Wooster alipinga mtazamo huo, akisema uhusiano wa Kenya na China hauongozwi na mshikamano wa kiitikadi.
Kauli hiyo ilitofautiana na msisitizo wa baadhi ya maseneta kuhusu kuongezeka kwa ushawishi wa China barani Afrika.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mahusiano ya Kigeni, Jim Risch, alisema Kenya ni mshirika muhimu wa Amerika lakini akaibua wasiwasi kuhusu uhusiano wake wa kidiplomasia na China pamoja na msimamo wake kuhusu Sudan. Mbali na usalama, Wooster alisema kuna nafasi ya kuimarisha ushirikiano kati ya Kenya na Amerika katika biashara, uwekezaji, afya na teknolojia.
Alitaja sekta ya teknolojia nchini Kenya, mazingira ya ujasiriamali na taasisi zake kuwa maeneo ambayo yanaweza kuvutia ushirikiano zaidi wa kiuchumi kati ya nchi hizo.
Kwa upande wake, Seneta Jeanne Shaheen alisema Wooster anakabidhiwa jukumu hilo wakati Kenya ikiingia kipindi cha uchaguzi na huku mustakabali wa misaada ya Amerika kwa afya na programu nyingine za maendeleo ukiwa miongoni mwa masuala yanayohitaji kushughulikiwa.
Wooster ni mwanachama wa Senior Foreign Service ya Amerika. Aliwahi kuwa balozi wa Washington nchini Jordan kuanzia 2020 hadi 2023 na baadaye kushikilia nyadhifa za juu katika Wizara ya Mambo ya Nje.
Amewahi kuhudumu Baghdad, Islamabad, Moscow na katika makao makuu ya NATO, pamoja na kufanya kazi katika Baraza la Usalama la Taifa la Amerika.
Kabla ya kujiunga na Foreign Service, Wooster alikuwa afisa wa Jeshi la Washington. Sasa anajiandaa kuhamia Nairobi na kuanza rasmi kazi kama balozi wa Amerika nchini Kenya.
from Taifa Leo https://ift.tt/Bs1LrE0
via IFTTT
Tags
TRENDING NEWS