SERIKALI imezuiwa kuzima au kuvuruga huduma za intaneti hadi kesi ambayo iliwasilishwa na mashirika kadhaa ya umma isikizwe na iamuliwe.
Mashirika manne yalielekea mahakamani yakisaka amri kuzuia serikali kuzima intaneti ikitaja matukio manne ya hapo nyuma ambayo intaneti ilizimwa.
Ilitaja Juni 25, 2024 ambapo intaneti ilizimwa kwenye kilele cha maandamano ya Gen Z na kusema hatua hiyo ilizuia uhuru wa kujieleza, ule wa wanahabari na ule wa kupata habari jinsi ambavyo imenakiliwa kwenye sheria.
Jaji Bahati Mwamuye alitoa amri inayozuia Mamlaka ya Mawasiliano Nchini (CA), Waziri wa Teknolojia na Mawasiliano na kampuni zinazotoa huduma za teknolojia na intaneti kuvuruga intaneti pamoja na kuzima mitandao ya kijamii, hadi kesi hiyo isikizwe na iamuliwe.
Jaji huyo pia aliagiza serikali na kampuni zinazotoa huduma za intaneti kukusanya na kuhifadhi maelezo yote, stakabadhi na maafikiano yote kuhusu matukio ya nyuma ya kuzimwa kwa intaneti.
Mashirika yaliyowasilisha kesi mahakamani ni Tume ya Kimataifa ya Majaji (ICJ), Muungano wa Wanablogu (BAKE), Chama cha Wanahabari Nchini (KUJ) yakihofia kuzimwa kwa intaneti katika uchaguzi mkuu wa 2027, mitihani au wakati wa maandamano.
“Tumechukua hatua hii ya kisheria kutokana na serikali kuzima intaneti wakati wa maandamano ya Gen Z 2024 na kuzima kwa mitandao ya kijamii, Telegramu na pia wakati wa Mitihani ya Kitaifa ya Kidato cha Nne (KCSE) 2023 na 2024,” kesi hiyo ikasema.
Makundi hayo yanataka mahakama iamue kuwa haki ya kutumia intaneti inatambuliwa kisheria. Pia wanataka mahakama iweke wazi kuwa kuzimwa kwa intaneti inakiuka haki ya kujieleza, uhuru wa vyombo vya habari, uhuru wa kutangamana, haki za kisiasa na maoni.
“Kuzimwa kwa intaneti ina athari ya kijamii na kiuchumi kwenye sekta mbalimbali na huwa inavuruga shughuli nyingi na kuathiri mapato. Hapa Kenya, uhuru wa kutumia intaneti unaendelea kupungua enzi hizi za kidijitali,” akasema wakili Dudley Ochiel
Makundi hayo yalisema kuwa mnamo Juni 25, 2024 wakati wa maandamano dhidi ya Mswada wa Fedha 2024, serikali ilizima intaneti kinyume cha sheria.
from Taifa Leo https://ift.tt/AvXyw8K
via IFTTT