MWANAMKE aliyeuawa na mumewe baada ya kupewa talaka katika Kaunti ya Lamu, alikuwa ametoroka vita Somalia akaishi kama mkimbizi humu nchini.
Najma Athman Bwanamusa, 34, aliuawa kwa kupigwa risasi na Shafi Swaleh Bwana, 36, Jumatatu wiki hii baada ya kupewa talaka ya tatu siku moja awali.
Imebainika kuwa, Najma alikuwa akiishi mjini Kiunga kwenye mpaka wa Kenya na Somalia kwa karibu miaka 14 sasa tangu alipotoroka mapigano na ukosefu wa usalama nchini mwao Somalia pamoja na jamaa zake.
Rafiki yake, Bi Mariam Alal Yusuf, 37, ambaye pia alipigwa risasi na kujeruhiwa vibaya wakati wa kisa hicho, pia ni mkimbizi kutoka Somalia aliyeishi Kiunga.
Amani na utulivu ambao Najma alikutana nao Kiunga ulimwezesha kupata mpenzi, hivyo kuishi kama raia wa Kenya.
Alikutana Shafi, ambaye ni Mkenya Mswahili wa asili ya Jamii ya Wabajuni wanaoishi Kiunga, wakafunga ndoa mwaka wa 2019.
Maafisa wa utawala wa serikali katika eneo la Kiunga, waliwataja wawili hao kuwa wanandoa walioishi kupendana kwa muda mrefu hadi wakapata mtoto msichana ambaye kwa sasa ana umri wa miaka miwili.
Hata hivyo mambo yalianza kuharibika mwaka huu walipoanza kushuhudiwa wakitofautiana. Juhudi za kujaribu kuiokoa ndoa yao ziligonga mwamba, hadi Shafi akaanza harakati za kumtaliki mkewe.
“Sisi tulimjua Bw Shafi kuwa kijana wa heshima na mtiifu wa sheria. Hatukutarajia kwamba angetekeleza kisanga hicho cha kusikitisha. Nidhamu yake ilifanya serikali yenyewe kumwamini na kumpa bunduki ya kuhudumu kijijini mwetu kama NPR,” akasema mmoja wa maafisa wa utawala aliyeomba asitajwe kwani hana idhini kuzungumzia suala hilo.
Afisa huyo alithibitisha kuwa, Najma na jamaa zake walipokewa Kiunga walipowasili kama wakimbizi kutoka Somalia katika mwaka wa 2011.
Baada ya tukio la Jumatatu, maafisa wa kushughulikia huduma za kibinadamu Lamu sasa wanashinikiza kuundwe mpango utakaowahusisha kikamilifu wakimbizi wanaoishi eneo hilo na kuhakikisha wanalindwa vilivyo.
Afisa wa Masuala ya Huduma za Jamii, Wakimbizi na Amani katika jamii, Bw Shee Kupi, alikashifu kisa hicho.
“Ilibidi niingilie kati kuhakikisha Bi Mariam, ambaye ni mkimbizi kutoka Somalia, anapokea matibabu hospitalini kupitia Huduma ya Matibabu Kitaifa (SHA). Tayari nimeanzisha harakati za kuhamasisha wakimbizi tunaoishi hapa Lamu kuhusu kuzijua haki zao na ulinzi wao pia udumishwe,” akasema Bw Kupi.
Eneo la Kiunga liko na karibu wakimbizi 505 waliopiga kambi ilhali wengine wakiishi kwa kutangamana au kuhifadhiwa na familia za wenyeji kwenye mji huo wa mpakani.
Naibu Kamishna wa Lamu Mashariki, Bw George Kubai, alishauri jamii kutafuta ushauri kwa watalaamu, marafiki na jamaa zao wengine badala ya kuchukua hatua za haraka na kujiua na kuathiri wengine wanapotofautiana nyumbani.
from Taifa Leo https://ift.tt/AenFt3c
via IFTTT