Atwoli aletea wafanyakazi ‘dili’ ya kupata nyumba za gharama nafuu

WAFANYAKAZI wanaopokea mishahara kila mwezi sasa watapewa kipaumbele katika ununuzi wa nyumba za gharama nafuu, kulingana na makubaliano yaliyofikiwa kati ya Rais William Ruto na Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (COTU) Francis Atwoli. Aidha, wawili hao wamekubaliana kwamba wafanyakazi wanaotaka kununua nyumba hizo sasa watahitajika kulipa arubuni (deposit) ya kiwango cha asilimia 5 pekee ya bei ya nyumba badala ya asilimia 10 wanayohitajika kulipa wakati huu. Kulingana na Atwoli, wamekubaliana pia kwamba pesa za Hazina ya Nyumba, zinazotokana na makato kutoka kwa mishahara ya wafanyakazi kila mwezi, zitatumika katika ujenzi wa nyumba pekee wala sio masoko, inavyofanyika sasa. Kwenye taarifa aliyoitoa baada ya kukutana na Rais Ruto, Jumatano, Juni 18, 2025, Bw Atwoli alisema walikubaliana kwamba serikali itasitisha mara moja ujenzi wa masoko kwa kutumia pesa Ushuru Wa Nyumba za Gharama Nafuu. “Na serikali imejitolea kurejesha pesa zote ambazo tayari zimetumika kufadhili ujenzi wa masoko chini ya mpango wa ujenzi wa nyumba,” Bw Atwoli akasema baada ya mkutano huo. Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Naibu Katibu Katibu Mkuu wa COTU Ernest Nadome, ambaye pia ni mwanachama wa Bodi ya Nyumba za Gharama Nafuu. Kulingana na Bw Atwoli, serikali pia imekubali kuunda kamati maalum itakayotwikwa jukumu la kukomboa pesa za Hazina ya Nyumba zilizoelekezwa katika miradi ya ujenzi wa masoko kote nchini. “Kamati hiyo itashirikisha wawakilishi kutoka serikali ya kitaifa na serikali za kaunti na itaendesha shughuli zake chini ya uangalizi wa Bodi ya Nyumba za Gharama Nafuu,” Bw Atwoli akaeleza. Kiongozi huyo wa COTU alielezea kufurahishwa kwake na mabadiliko hayo akisema yanajibu malalamishi yaliyowasilishwa na wafanyakazi kuhusu matumizi na usimamizi wa pesa za mpango wa ujenzi wa Nyumba za Gharama Nafuu (AHP). “Tunampongeza Rais kwa kukubali kufanya mazungumzo nasi na kujitolea kwake na serikali yake kuhakikisha kuwa wafanyakazi wanafaidika kutokana na ada nyumba wanazolipa,” akaeleza. Afueni hii inajiri siku kadhaa baada ya Bw Atwoli kulalamika waziwazi kwamba fedha za Ushuru wa nyumba zinatumiwa vibaya kwa kuelekezwa katika miradi mingine kama vile ujenzi wa masoko, shule, barabara miongoni mwa mingine. Lakini mnamo Juni 8, 2025, Katibu wa Idara ya Nyumba Charles Hinga alimjibu Atwoli kwa kufafanua kuwa kuelekezwa wa fedha za nyumba kwa miradi mingine hakumaanishi kuwa pesa hizo zinatumika vibaya. “Idara ya Nyumba na Ustawi wa Miji inatambua malalamishi yaliyoibuliwa na Muungano wa Vyama vya Kutetea Masilahi ya Wafanyakazi (COTU) kuhusiana na matumizi ya fedha za Ushuru wa Ujenzi wa Nyumba za Gharama Nafuu. Hata hivyo, kwa heshima, tungependa kufafanua kuwa matumizi ya fedha hizo katika ujenzi wa masoko na miundo mbinu nyingine ni kwa faida ya watakaonunua nyimbo hizo," akasema kwenye taarifa.

from Taifa Leo https://ift.tt/DKxt8Gg
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post