
MKATABA wa Muungano wa Kenya Kwanza wa mwaka 2022 sasa uko chini ya uchunguzi wa mahakama katika kesi ya kuondolewa madarakani kwa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua. Walalamishi wenza wanadai kuwa muungano huo tawala ulijengwa kwa sera ya “serikali ya hisa” iliyobadilisha nyadhifa za umma kuwa zawadi kwa uaminifu wa kisiasa. Walalamishi hao wanataka mahakama ichunguze mkataba huo wa 2022, itangaze mfumo wake wa ugavi wa madaraka kuwa kinyume cha sheria, na kwa msingi huo ibatilishe kuondolewa madarakani kwa Bw Gachagua. Katika hati zilizorekebishwa na kuwasilishwa mahakamani, walalamishi wameanika rasmi mkataba wa Muungano wa Kenya Kwanza katikati ya mvutano huo wakisema unaonyesha jinsi mamlaka na nyadhifa katika serikali ya Rais William Ruto zilivyogawanywa kwa misingi ya kisiasa badala ya kanuni za Katiba. Wanadai kuwa mpangilio wa kisiasa unaoongozwa na Dkt William Ruto unaonyesha kuwa dhana ya “umiliki wa hisa” ambayo Bw Gachagua aliwahi kutaja hadharani haikuwa kauli ya kisiasa tu bali ilikuwa sera rasmi. Kwa mujibu wao, mkataba huo ulikuwa makubaliano ya kisiasa yenye nguvu ya kisheria yaliyoathiri muundo wa serikali na sasa yanadhoofisha uhalali wa mchakato uliosababisha kuondolewa kwake madarakani. Sehemu ya mashtaka yaliyopelekea kung’olewa kwa Gachagua mwaka 2024 ilihusu matamshi yake kwamba serikali ya Kenya Kwanza ilikuwa “serikali ya wenyehisa.” “Mashtaka ya ukabila yaliyotolewa dhidi ya mlalamishi wa kwanza (Gachagua) hayana msingi kwa kuwa ingawa huenda alitoa kauli zilizochukuliwa kuwa za kuzua mgawanyiko, kwa vitendo mshtakiwa wa sita, Rais William Ruto, ndiye aliyewajibika zaidi kwa uteuzi wa maafisa wakuu wa serikali kwa misingi ya kikabila,” inasema sehemu ya hati hiyo. Walalamishi wanasema Ibara ya 21 ya mkataba huo yenye anwani “Ugavi wa Majukumu ya Serikali ya Kitaifa” inaonyesha wazi kuwa uteuzi wa nyadhifa za serikali ulifanywa kwa hesabu za kisiasa badala ya misingi ya kikatiba. Waliotia saini mkataba huo ni pamoja na Rais Ruto, kiongozi wa Ford Kenya Moses Wetang’ula (sasa Spika wa Bunge la Kitaifa) na kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi (Mkuu wa Mawaziri). Nafasi zao serikalini zimeainishwa chini ya kipengele cha ugavi wa majukumu ya serikali ya kitaifa. Kwa mujibu wa kiapo cha mmoja wa walalamishi, Peter Koira, waliotia saini walikubaliana kugawana nyadhifa za umma na rasilmali. “Baada ya kuapishwa kwa Rais mteule William Ruto na Naibu Rais mteule Rigathi Gachagua, serikali iliundwa ikizingatia dhana ya umiliki wa hisa iliyoainishwa katika Mkataba wa Muungano wa Kenya Kwanza,” anaeleza. Kifungu kimoja cha mkataba huo kinasema: “ANC na Ford-Kenya zitakuwa na asilimia 30 ya nyadhifa katika Serikali ya Kitaifa.
from Taifa Leo https://ift.tt/qnmlLo4
via
IFTTT