Ni kama wengi hawatapata maua hii Valentino bei ya bidhaa hiyo ikipanda

SHADA la maua 10 nyekundu ya waridi lililokuwa likiuzwa kwa takriban Sh500 mwaka jana sasa linauzwa kwa Sh2,000, ongezeko kubwa la bei lililofanya Wakenya wengi kutomudu bei Siku ya Wapendanao inayoadhimishwa leo.
Bei imepanda kwa kasi kuelekea Februari 14, wafanyabiashara wakisema mahitaji makubwa pamoja na soko la nje kuchukua waridi bora zaidi kutoka Kenya kumeacha upungufu mkubwa kwa wanunuzi wa hapa nchini.
Baadhi ya wauza maua wanasema hawajapata waridi tangu Januari.
Upungufu huo umechochea ongezeko la bei, ambapo mnunuzi anayetaka kununua shada la maua 100 sasa analazimika kulipa hadi Sh15,000.
“Bei zimepanda sana. Wasambazaji wametuambia tu kuwa waridi haipatikani, bila maelezo yoyote,” anasema Zippora Wachira, muuza maua, akiongeza: “Maua machache tunayopata ni ghali kupindukia, hivyo tunalazimika kuongezea wateja bei wabebe gharama.”
Afisa Mkuu Mtendaji wa Baraza la Maua Kenya Clement Tulezi, anasema uhaba katika soko la ndani hautokani na uzalishaji mdogo bali mahitaji makubwa sana katika masoko ya kimataifa. “Mahitaji yalikuwa makubwa mno. Waridi zote za kiwango cha usafirishaji nje zilichukuliwa. Wakulima waliuza karibu kila kitu,” alisema wateja wakiondoka mikono mitupu.


from Taifa Leo https://ift.tt/8UxtETb
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post