Nyasi ya miujiza inavyobadili maisha ya wafugaji na wakulima wakati wa ukame

KADRI athari za mabadiliko ya tabianchi zinavyozidi kushika kasi kuanzia ukame wa muda mrefu hadi mafuriko, wadudu na magonjwa, wakulima na wafugaji nchini Kenya wanalazimika kubadili mbinu za uzalishaji ili kuhimili hali hizi ngumu. Katika maeneo kame na nusu kame (ASAL), ambako maisha yanategemea pakubwa mifugo, changamoto hii imekuwa ya dharura.

Kwa Abdirahman Ali Hassan, mfugaji kutoka Kaunti ya Wajir, simulizi ya ukame si ya kusimuliwa tu—ni majeraha aliyoyapitia.

Anakumbuka kwa uchungu ukame wa mwaka 2021–2022, uliotajwa kuwa miongoni mwa mibaya zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini Kenya katika kipindi cha miongo kadhaa. Katika kipindi hicho, alipoteza zaidi ya ng’ombe 100 na ngamia karibu 60, hasara ya mamilioni ya pesa. Lakini zaidi ya fedha, anasema kilichouma zaidi ni thamani ya kihisia. “Haikuwa tu hasara ya kiuchumi. Ilikuwa huzuni kubwa. Kila siku mfugaji alikuwa akiamka kuhesabu mifugo waliokufa,” anakumbuka.

Takwimu za Wizara ya Kilimo na Maendeleo ya Mifugo zinaonyesha kuwa zaidi ya mifugo milioni 2.5 walipotea kote nchini wakati huo, huku malisho yakikauka na vyanzo vya maji kupungua kwa kiwango cha kutisha.

Hali hiyo ilimsukuma Hassan kutafuta suluhisho la kudumu.

Kugundua Juncao

Mwaka 2023, alipotembelea mradi wa kisasa wa mifugo huko Malindi, alishuhudia kitu tofauti—malisho ya kijani kibichi licha ya ukame uliokuwa umekumba nchi. Hapo ndipo alipokutana na nyasi ya Juncao, teknolojia kutoka China inayozidi kupata umaarufu.

Juncao ni nyasi ndefu inayokua kwa kasi, yenye uwezo mkubwa wa kustahimili ukame na kutoa mavuno mengi ya malisho kwa muda mfupi.

[caption id="attachment_186771" align="aligncenter" width="300"] Abdirahman Ali Hassan, mfugaji kutoka Kaunti ya Wajir anakuza Juncao kupunguza gharama ya ufugaji. Picha|Sammy Waweru[/caption] “Nilipoona mifugo wanalishwa vizuri bila kutegemea mvua, nilijua lazima nibadilishe mfumo wangu,” anasema Hassan.

Alianza na ekari moja tu, akitumia vipandikizi (cuttings) alivyopata kutoka Nakuru.

“Leo hii, nina zaidi ya ekari 10 za Juncao ambapo pia huchanganya na nyasi aina ya Brachiaria na mazao kama viazi vitamu ili kuimarisha lishe ya mifugo,” anaambia Akilimali Dijitali. Mbali na kupanda malisho, Hassan amewekeza katika teknolojia za kuongeza thamani—ikiwemo mashine za kukatakata majani (chaff cutter), kutengeneza pellets na kuhifadhi malisho (hay baler). Pia ana maghala mawili ya silage yenye uwezo wa kuhifadhi tani 90 kila moja. Matokeo yake yamekuwa ya kuvutia. Wakati wafugaji wengi walipohangaika kutafuta malisho wakati wa kiangazi cha hivi karibuni (2026), yeye hakuwa na wasiwasi. Badala yake, aliuza malisho ya ziada na kupata karibu Sh1.7 milioni.

Aidha, amepunguza idadi ya mifugo na kuwekeza kwa ng’ombe wa maziwa walioboreshwa—hasa chotara wa Sahiwal—wanaotoa kati ya lita 14 hadi 16 za maziwa kwa siku.

Leo hii, shamba la Hassan limegeuka kuwa kituo cha mafunzo kwa wafugaji wengine, hasa katika jamii za kuhamahama (pastoralists) ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zikitegemea mbinu za jadi.

[caption id="attachment_186772" align="aligncenter" width="300"] Kevin Mwangi Kamau, anatumia nyasi ya Juncao iliyosagwa kukuza uyoga Nairobi. Picha|Sammy Waweru[/caption] Fursa mpya kwa wakulima mijini

Mbali na ufugaji, Juncao pia imefungua milango mipya ya kipato kwa wakulima wa mazao mbadala.

Jijini Nairobi, Kevin Mwangi Kamau aligeukia teknolojia hii baada ya kupoteza kazi wakati wa janga la Covid-19 mwaka 2021. Akiwa na mtaji wa Sh15,000 pekee, alianza kilimo cha uyoga.

Awali alitumia mabaki ya ngano kama malighafi na kuzalisha karibu kilo 100 kila baada ya wiki mbili. Lakini baada ya kuanza kutumia Juncao, uzalishaji wake umeongezeka maradufu—akifikia kilo 2,000 za uyoga aina ya oyster na kilo 800 za button kila mwezi.

“Juncao hufanya uyoga kukua kwa haraka na kwa ubora wa juu,” anasema.

Biashara yake sasa imeajiri watu 10, wengi wao wakiwa wanawake, na kuwa chanzo muhimu cha kipato mijini.

Teknolojia ya Juncao ilibuniwa nchini China na Profesa Lin Zhanxi wa Chuo Kikuu cha Fujian Agriculture and Forestry. Mbali na kulisha mifugo na kukuza uyoga, nyasi hii ina matumizi mengi—ikiwemo uhifadhi wa mazingira, kudhibiti mafuriko na uzalishaji wa nishati ya biomasi. Serikali ya Kenya, kwa ushirikiano na mashirika ya kimataifa kama UNDESA, inaendeleza matumizi ya Juncao kupitia miradi ya kuimarisha mifumo ya chakula, kupunguza umaskini na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Kwa sasa, zaidi ya hekta 400,000 duniani zimepandwa Juncao.

from Taifa Leo https://ift.tt/5tWSoED
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post