Rais kukutana na wawakilishi wa PSV kuepusha mgomo wa mafuta kurejelewa

RAIS William Ruto ameanza ziara yake ya maendeleo ya wiki moja katika eneo la Pwani Kaunti ya Mombasa huku shinikizo zikiongezeka kwa serikali kuzuia mgomo mwingine wa kulalamikia bei za mafuta uliopangwa wiki ijayo.

Rais, aliyerejea nchini Alhamisi asubuhi kutoka ziara rasmi katika mataifa ya Azerbaijan na Kazakhstan, anatarajiwa kurekebisha ratiba yake ili kutoa nafasi kwa mkutano na wadau wa sekta ya uchukuzi kuhusu ongezeko la bei ya mafuta.

Duru za kuaminika zilithibitisha kuwa mkutano kati ya Rais na wawakilishi wa vyama vya usafiri kutoka Nairobi umepangwa kufanyika Ijumaa katika jiji la Mombasa.

Vyama hivyo vimepatia serikali siku saba kufikia muafaka kuhusu masuala ambayo vinadai yanaweza kusaidia kuzuia kupanda zaidi kwa bei ya mafuta.

Kutokuwepo kwa Rais nchini kulizua wasiwasi miongoni mwa wananchi wakati taifa lilipokaribia kusimama baada ya wahudumu wa uchukuzi kusitisha huduma Jumatatu kulalamikia bei mpya za mafuta zilizotangazwa wiki iliyopita na Mamlaka ya Kudhibiti Kawi na Petroli (Epra).

Akizungumza katika eneo la Mama Ngina Waterfront jijini Mombasa, ambapo hatimiliki 33,000 zilitolewa kwa wakazi kutoka kaunti sita za Pwani, Dkt Ruto aliepuka kuzungumzia moja kwa moja suala la bei ya mafuta.

Badala yake, alitumia hafla hiyo kuhimiza mazungumzo huku akiwashutumu viongozi wa upinzani kwa madai ya kueneza chuki na migawanyiko miongoni mwa Wakenya.

Kwa mujibu wa Rais, serikali imefanikiwa kutatua changamoto nyingi kupitia mazungumzo, ikiwa ni pamoja na kuundwa kwa serikali jumuishi pamoja na chama cha ODM ili kuendeleza siasa zenye suluhu.

“Serikali jumuishi imetuwezesha kupata suluhisho kwa matatizo ya ardhi na changamoto nyingine zinazoikabili nchi.

Tumejitolea kuhakikisha serikali hiyo inaleta matokeo kwa Wakenya. Huo ndio moyo wa umoja utakaotusukuma mbele,” alisema.

Dkt Ruto aliwataka wananchi kutofuata siasa za viongozi bila kutafakari, akisema wapinzani wake hawana ajenda wala dira ya kuipeleka nchi mbele.

Alisema siasa za migawanyiko na ubaguzi zinazoshuhudiwa sasa tayari zimeanza kugharimu maisha ya watu, akimtaja mwanamuziki wa injili Rachel Wandeto ambaye alifariki akipokea matibabu katika Hospitali ya Kenyatta baada ya kuchomwa moto.

Kwa mujibu wa viongozi wa vyama vya uchukuzi waliozungumza na Taifa Leo, eneo la mkutano huo halikuwa limewekwa wazi lakini waliarifiwa kwamba wangeelekezwa mara tu watakapowasili Mombasa.

Mwenyekiti wa kitaifa wa Chama cha Wamiliki wa Matatu (MOA), Bw Albert Karakacha, alisema walialikwa na Rais kufuatia makubaliano yaliyofikiwa Jumanne katika kikao cha pamoja na Waziri wa Usalama wa Ndani, Bw Kipchumba Murkomen pamoja na mwenzake wa Nishati, Bw Opiyo Wandayi.

“Ndio, tumealikwa na niko njiani lakini tunataka kuwahakikishia wanachama wetu kwamba hatutatishwa. Tunaenda huko tukiwa na msimamo wazi kuhusu masuala yanayopaswa kushughulikiwa,” alisema Bw Karakacha.

Alisema hawajafurahishwa na madai yanayosambazwa mitandaoni kwamba walihongwa ili kusitisha mgomo huo.

“Hatujafurahishwa na yanayosemwa. Tunajigharamia sisi wenyewe kwa safari hii ya Mombasa. Tuna uwezo wetu. Mimi binafsi nina matatu na siwezi kuhongwa,” alisema.

Mwenyekiti wa chama cha Mass Mobility Operators Association, Bw Wilfred Bosire , alisema madai hayo ya hongo yanaendelea kuchunguzwa.

“Mimi na baadhi ya wenzangu bado tunajiuliza fedha hizo zilitoka wapi na ni nani aliyepewa. Tunaelewa mambo mengi yanaendelea kusemwa na huenda pesa zilihusika na baadhi yetu hatukufaidika,” alisema Bw Bosire.

Baadhi ya maafisa wa vyama hivyo tayari wamewasili Mombasa huku kukiwa na sintofahamu kuhusu ni viongozi gani hasa walipaswa kuhudhuria mkutano huo.

Wakati huo huo, Gavana wa Nairobi, Bw Johnson Sakaja alipuuza madai kwamba ndiye aliyefadhili usafiri wa viongozi hao kuelekea Mombasa.

“Ni habari za uongo,” gavana aliambia Taifa Leo.

Bw Sakaja alisema anapendekeza kuwepo kwa kiwango maalum cha kodi ya mafuta ili kupunguza makali ya gharama kubwa ya mafuta kwa sekta ya matatu na wananchi kwa jumla.

“Tukiketi chini na kufikiria kwa kina tunaweza kupata suluhu. Kwa mfano, tunaweza kuweka mfumo ambapo ushuru wa mafuta utatozwa tu ikiwa bei ya mafuta ni Sh200 au chini ya hapo. Bei ikipita kiwango hicho, kodi isimamishwe,” alisema.

Aliongeza kuwa jukumu la serikali ni kuhakikisha gharama ya kuingiza mafuta nchini pamoja na kodi haipelekei bei ya mafuta kuzidi Sh200 kwa lita.

“Ikiwa gharama ya kuagiza mafuta iko chini kiasi kwamba kodi inaweza kutozwa bila bei kuzidi Sh200, basi kodi ibaki. Lakini gharama ikipanda na kufanya bei kuvuka kiwango hicho, kodi isimamishwe ili kuwalinda wananchi. Hilo ndilo pendekezo langu kuhusu suala la mafuta,” alisema Bw Sakaja.

Wadau wa sekta ya matatu walisema watafutilia mbali mgomo huo iwapo tu serikali itakubali matakwa yao.



from Taifa Leo https://ift.tt/zCRrSQx
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post