Serikali yabanwa kuweka wazi upanuzi wa JKIA baada ya rafiki wa Ruto kuhusishwa

SHINIKIZO zinaongezeka kwa serikali kuelezea wazi kuhusu hali ya mkataba wa upanuzi na uboreshaji wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA), baada ya kuibuka kuwa kampuni moja ya China huenda imepata kandarasi hiyo.

Mashirika ya kiraia, wanasiasa na mawakili wamekosoa serikali kwa kile wanachosema ni ukosefu wa uwazi katika utoaji wa zabuni ya mradi huo wa mabilioni ya pesa.

Wameonya kuwa wako tayari kwenda mahakamani kulazimisha serikali kufichua wahusika wote kwenye mkataba huo.

Habari zinaonyesha zabuni ya mradi wa kisasa wa JKIA tayari imetolewa kwa kampuni ya China na kutiwa saini kunatarajiwa wiki ijayo.

Duru kutoka taasisi zinazohusika na mchakato huo zilisema zabuni hiyo ilitolewa mwezi huu na kwa sasa inasubiri muda wa siku 14 unaoruhusu waliokosa zabuni kupinga uamuzi huo kisheria.

Kulingana na duru hizo, thamani ya mradi huo ni kati ya Sh150 bilioni na Sh180 bilioni kutegemea mabadiliko ya viwango vya ubadilishaji fedha.

Duru kutoka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Kenya (KAA) zilisema kampuni za China Road and Bridge Corporation (CRBC) na Sinohydro ndizo zilizowasilisha zabuni, huku dalili zikionyesha kuwa CRBC ndiyo ina nafasi kubwa kushinda.

Mjadala umechochewa zaidi na madai kuwa kampuni inayohusishwa na mfanyabiashara wa Zimbabwe Wicknell Chivayo itashirikiana na CRBC katika utekelezaji wa mradi huo.

Seneta wa Busia Okiya Omtatah amekosoa serikali kwa kuendesha mchakato huo kwa siri huku akisema Wakenya na hata Bunge hawajapatiwa taarifa za kutosha kuhusu hatari za kifedha zinazoweza kuwakumba walipa ushuru.

“Taratibu za uwazi na haki ya kupata habari zimekiukwa. Hatutakubali hali hii na tutatumia njia za kisiasa na kisheria kuipinga,” alisema.

Taasisi ya The Institute for Social Accountability (TISA) pia imetaka serikali kufichua maelezo yote ya zabuni, masharti ya mkataba na umiliki halisi wa kampuni iliyopewa kazi hiyo.



from Taifa Leo https://ift.tt/lAGHR4T
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post