Gachagua apinga madai kuwa anampigia debe Kalonzo kupambana na Ruto 2027

KIONGOZI wa chama cha DCP, Rigathi Gachagua, amesema muungano wa upinzani hautamtangaza atakayepeperusha bendera ya urais 2027 mapema kwa hofu kwamba atalengwa na serikali na kuteswa. Akizungumza nyumbani kwake Wamunyoro, Kaunti ya Nyeri, Jumamosi alipokutana na wajumbe kutoka eneo la Githunguri, Kaunti ya Kiambu, Gachagua alisema upinzani utamtangaza mgombea wake mwaka ujao, kabla ya muda wa mwisho uliowekwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC). “Hatutaharakisha jambo hilo. Tunaweza kumtangaza mgombea wetu wakati wowote kabla ya Mei 15, 2027. Tukifanya hivyo mapema, tutapatia serikali nafasi ya kumwandama kisiasa,” alisema. Alisema viongozi wakuu wa muungano huo wamekubaliana kila mmoja ajenge uungwaji mkono katika ngome yake ya kisiasa huku wakisubiri muda mwafaka wa kumchagua atakayepeperusha bendera wa upinzani. Gachagua alikanusha taarifa zinazosambazwa kuwa tayari upinzani umekubaliana kuhusu mgombea atakayemenyana na Rais William Ruto katika uchaguzi mkuu wa 2027. “Hizo ni propaganda. Bado hatujamchagua mtu yeyote. Tulichokubaliana ni kwamba tutakuwa na mgombea mmoja wa pamoja,” alisema. Pia alikanusha madai kwamba anampigia debe kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka, apewe tiketi ya urais. Alisema viongozi wote wenye azma ya kuwania urais watapata nafasi sawa wakati wa mazungumzo ya kumtafuta mgombea wa pamoja. Miongoni mwa wanaotajwa katika muungano huo ni Kalonzo Musyoka, Martha Karua wa People's Liberation Party, Justin Muturi wa Democratic Party, Fred Matiang'i wa Jubilee, Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna wa Linda Mwananchi, Eugene Wamalwa na Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya wa DAP-K. Gachagua alisema yeye binafsi angependa kuwa mgombea, lakini yuko tayari kuacha azma hiyo iwapo mgombea mwingine ataonekana kuwa na nafasi kubwa zaidi ya kushinda. “Niko tayari kujitoa ikiwa hilo litaimarisha umoja wa upinzani. Sitakuwa sababu ya kuvunjika kwa muungano huu,” alisema. Aidha, alishutumu serikali kwa madai ya kutumia propaganda, vurugu, kununua viongozi na mbinu nyingine za kujaribu kuvuruga umoja wa upinzani. Kwa mujibu wake, serikali pia inajaribu kueneza uvumi kwamba baadhi ya viongozi wa upinzani wako mbioni kujiunga nayo. Alisema lengo kuu la upinzani kwa sasa ni kueneza ajenda ya ‘Wantam’, kuwahamasisha wapigakura na kujenga umoja utakaowezesha muungano huo kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa 2027. Gachagua alisisitiza kuwa ushindi katika uchaguzi utategemea idadi ya kura, akisema hakuna eneo moja linaweza kushinda urais peke yake chini ya Katiba ya mwaka 2010. “Mlima Kenya ni ngome muhimu ya kura, lakini ushindi utapatikana kupitia ushirikiano wa kitaifa. Tunahitaji umoja na si ubinafsi,” alisema.

from Taifa Leo https://ift.tt/PXmnplC
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post