
KILICHOANZA kama uvumi wa ajabu sasa kimegeuka kuwa chanzo cha hofu, vurugu na vifo katika baadhi ya maeneo ya Pwani, huku polisi na wataalamu wa afya wakikanusha madai kwamba mwanaume anaweza kupoteza sehemu zake za siri baada ya kuguswa na mtu mwingine.
Uvumi huo, ambao hauna msingi wa kisayansi wala kitabibu, umefanya watu wengi kuishi kwa wasiwasi.
Katika visa kadhaa, watu wasio na hatia wamepigwa na umati wenye hasira baada ya kutuhumiwa kwa madai hayo, huku wahalifu wakidaiwa kutumia taharuki hiyo kuiba simu, pochi na mali nyingine.
Kisa kilichotikisa wengi kilitokea Nyali, Mombasa, ambapo waumini wa dhehebu ya Jehovah Witness wanne walishambuliwa walipokuwa wakihubiri kutoka nyumba moja hadi nyingine.
Umati uliwalaumu kwa kuhusika na “kupotea” kwa sehemu za siri za wanaume kabla ya polisi kuwaokoa.
Baadaye, wakazi wawili, Al Amin Mgunya Johnson na Kennedy Mersyden Milimo, walifikishwa mahakamani wakikabiliwa na mashtaka ya kuchochea vurugu.
Milimo pia alishtakiwa kwa kosa la kumshambulia mmoja wa wahubiri hao. Wote walikana mashtaka na kuachiliwa kwa dhamana.
Mzee wa Mashahidi wa Yehova katika Jumba la Ufalme la Bamburi, Martin Henya, alisema madai hayo ni ya uongo na kusisitiza kuwa dhehebu hilo halihusiki kwa njia yoyote na uchawi au nguvu za kishirikina.
Huku kesi hiyo ikiendelea mahakamani, familia moja Mombasa inaendelea kuomboleza baada ya John Kaleghe, mwenye umri wa miaka 24, kuuawa kwa kupigwa na umati katika Soko la Marikiti baada ya kutuhumiwa kwa madai hayo.
Msemaji wa familia, Leah Mwandaghina, alisema Kaleghe alikuwa kitindamimba na tumaini la wazazi wake.
Alisema familia ilimtafuta kwa siku kadhaa kabla ya kupata mwili wake katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Pwani.
Kwa mujibu wake, majeraha aliyopata yalikuwa makubwa kiasi kwamba ilikuwa vigumu kumtambua. Familia pia inadai kuwa alikimbilia polisi kuomba msaada lakini hakufaulu kuokolewa kwa umati.
Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) Pwani imesema tayari imerekodi visa 19 vinavyohusiana na uvumi huo katika kaunti za Mombasa, Kilifi na Kwale. Watu wawili tayari wameuawa kwa kupigwa na umma.
Mratibu wa DCI Pwani, Benson Kasyoki, alisema watu wote waliodai kupoteza sehemu zao za siri walifanyiwa uchunguzi wa kitabibu na kubainika hawakuwa na jeraha lolote wala mabadiliko ya viungo vyao.
Alisema uchunguzi unaonyesha makundi ya wahalifu yanatumia uvumi huo kuwalenga watu, huku washirika wao wakiiba mali wakati umati unamzingira mtuhumiwa.
Wakati huo huo, DCI imeanzisha uchunguzi wa video za CCTV na ujumbe unaosambazwa mitandaoni ili kubaini wanaochochea vurugu na kusambaza taarifa za uongo.
Daktari wa mfumo wa mkojo, Dkt Omar Bin Salman wa Kliniki ya Mombasa Urology, alisema kisayansi haiwezekani kwa sehemu za siri za mwanaume kutoweka kwa kuguswa na mtu mwingine.
Alifafanua kuwa mabadiliko ya muda yanayoweza kutokea hutokana na misuli ya mwili kujikaza, lakini haimaanishi kuwa kiungo kimepotea.
Aliongeza kuwa kama sehemu hizo zingetoweka kweli, mgonjwa hangeweza kuenda haja ndogo na hiyo ingekuwa hali ya dharura inayohitaji matibabu ya haraka.
Kwa sasa, maafisa wa usalama wanatoa wito kwa wananchi kupuuza uvumi huo, kutochukua sheria mikononi na kuripoti visa vyovyote kwa polisi.
from Taifa Leo https://ift.tt/zcZM4T5
via
IFTTT