
WANASAYANSI wamegundua hali mpya ya kutisha ya virusi vya Ukimwi kuanza kustahimili dawa muhimu inayotumika katika matibabu ya ugonjwa huo katika nchi nne za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Utafiti uliowasilishwa katika mkutano wa International Aids Society (IAS) mjini Rio de Janeiro, Brazil, umeonyesha hali hiyo miongoni mwa watu wanaoishi na Ukimwi nchini Kenya, Tanzania, Msumbiji na Lesotho.
Watafiti wameonya kuwa hali hiyo ikiendelea, maambukizi mapya ya Ukimwi yanaweza kuongezeka. Kinga ya mwili ya wagonjwa ambao virusi vyao vitakuwa vimekuwa sugu kwa dawa hiyo inaweza pia kudhoofika na kuwa katika hatari ya kupata magonjwa mengine ambayo yanaweza kusababisha kifo.
Dawa inayohusika ni dolutegravir, inayojulikana kwa kifupi kama DTG. Tangu 2018, dawa hiyo imekuwa chaguo la kwanza na la pili katika matibabu ya Ukimwi.
Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema DTG ina ufanisi mkubwa, ni rahisi kutumia na husababisha madhara machache ikilinganishwa na baadhi ya dawa nyingine zinazotumika.
Dawa hiyo pia inajulikana kwa kuwa na uwezo mkubwa wa kuzuia virusi vya Ukimwi kuzoea na kustahimili matibabu.
Daktari Loice Ombajo, mtafiti mkuu wa utafiti huo na mtaalamu wa magonjwa ya kuambukiza, alisema sampuli za kwanza za utafiti zilikusanywa kutoka kwa watu 2,994 katika vituo 131 nchini Kenya.
Washiriki hao walikuwa wametumia matibabu yenye DTG kwa angalau miezi sita.
Baadhi ya washiriki waliopatikana kuwa na mabadiliko ya virusi yanayohusishwa na usugu wa DTG waliingizwa katika utafiti maalumu ili kupata ushahidi wa kusaidia kuboresha matibabu ya wagonjwa ambao dawa hiyo imeshindwa kuwasaidia.
“Bado kuna ushahidi mdogo kuhusu namna ya kuwahudumia watu wanaoishi na Ukimwi ambao virusi vyao vimekuwa sugu kwa dolutegravir,” alisema Dkt Ombajo.
Alisema utafiti huo unalenga kutoa ushahidi utakaosaidia wataalamu kufanya maamuzi bora kuhusu matibabu ya wagonjwa hao.
Takriban watu tisa kati ya 10 wanaotumia DTG hufikia kiwango ambacho virusi vya HIV havionekani kwa wingi katika damu.
Hata hivyo, baadhi yao hushindwa kufikia kiwango hicho. Dkt Ombajo alisema sababu kubwa ni kutotumia dawa ipasavyo.
Alisema baadhi ya wagonjwa huchoka kutumia dawa kila siku, wengine husahau, huku wengine wakikosa hamu ya kuendelea na matibabu kutokana na hali yao.
“Usipotumia dawa au ukaitumia mara kwa mara bila kufuata ratiba, virusi vinaweza kubadilika na kuwa sugu kwa dawa hiyo,” alisema.
Katika utafiti huo, watafiti walifanya kazi na washiriki waliokuwa hawatumii dawa ipasavyo ili kuwasaidia kuendelea na matibabu.
Takriban asilimia 70 walifikia kiwango cha kudhibiti virusi, huku asilimia 30 wakishindwa. Watafiti walilenga kundi hilo kubaini iwapo kiwango kikubwa cha virusi kilisababishwa na kuzoea dawa.
Waligundua kuwa watatu kati ya kila washiriki 10 katika kundi hilo virusi vilikuwa sugu kwa DTG.
Dkt Ombajo alisema hali hiyo ni ya kutia wasiwasi kwa sababu dawa hiyo inaweza kushindwa kufanya kazi hata mgonjwa akiendelea kuitumia.
Tatizo jingine ni gharama kubwa ya vipimo vya kubaini hali ya dawa kwa virusi, huku nchi nyingi zikikosa rasilimali za kutosha kufanya vipimo hivyo mara kwa mara.
Utafiti pia ulibaini baadhi ya wanawake wajawazito na wanaonyonyesha wanakumbwa na hali hiyo.
Alisema hali hiyo inaweza kuongeza hatari ya mama mwenye kiwango kikubwa cha virusi kumwambukiza mtoto au mwenzi wake wa ngono.
from Taifa Leo https://ift.tt/e1BWAQN
via IFTTT
Tags
TRENDING NEWS