
Profesa Hiroyuki Hino
Profesa Hino ni raia wa Japan mwenye tajriba ya miongo kadhaa katika masuala ya fedha na maendeleo. Aliwahi kufanya kazi katika Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) tangu mwaka 1975 na baadaye kuwa mkurugenzi wa ofisi yake ya Asia na Pacific. Pia aliwahi kuwa mshauri wa kiuchumi wa aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga wakati wa Serikali ya Muungano. Kulingana na Ikulu, tajriba yake kuhusu mageuzi ya kiuchumi katika mataifa ya Asia kama Korea Kusini, Singapore, China na Vietnam itasaidia Kenya kuandaa mkakati wa kufikia uchumi wa viwanda.Profesa Anyang' Nyong'o
Gavana wa Kisumu, Profesa Anyang' Nyong'o, analeta uzoefu mkubwa katika siasa, utawala na taaluma. Baada ya kupata shahada ya kwanza katika Chuo Kikuu cha Makerere, aliendelea na masomo katika Chuo Kikuu cha Chicago alikopata Shahada ya Uzamili na Uzamivu katika Sayansi ya Siasa. Aliwahi kuwa mhadhiri na baadaye profesa katika Chuo Kikuu cha Nairobi pamoja na kufundisha katika vyuo vikuu vya Mexico na Ethiopia. Katika serikali ya Rais Mwai Kibaki, alihudumu kama Waziri wa Mipango na Maendeleo ya Kitaifa na kushiriki katika mageuzi yaliyozaa Ruwaza ya 2030. Profesa Nyong'o anasema ruwaza mpya haikusudiwi kufuta ile ya 2030 bali kuendeleza msingi uliowekwa na mipango ya awali ya maendeleo.Profesa Michael Chege
Profesa Michael Chege ni mtaalamu wa utawala bora, uchumi wa kisiasa na ujenzi wa taasisi za serikali. Kwa sasa anafundisha sera za umma katika Chuo Kikuu cha Nairobi baada ya kuhudumu katika taasisi mbalimbali zikiwemo UNDP, Ford Foundation na Chuo Kikuu cha Florida nchini Amerika. Amefanya pia kazi za ushauri kwa Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo Afrika na mashirika mengine ya kimataifa. Ikulu inaamini mchango wake utasaidia kuimarisha taasisi zinazoweza kuendeleza sera za maendeleo bila kutegemea mabadiliko ya serikali.Profesa Karuti Kanyinga
Profesa Karuti Kanyinga ni mmoja wa wataalamu wakuu nchini kuhusu ugatuzi, utawala bora, Katiba na sera za umma. Kwa zaidi ya miaka 30 amefanya utafiti kuhusu haki za ardhi, demokrasia, uchaguzi, ushiriki wa wananchi na maendeleo. Akiwa katika Taasisi ya Tafiti za Maendeleo ya Chuo Kikuu cha Nairobi, ameongoza tafiti nyingi zilizochangia mageuzi ya utawala nchini.Profesa Peter Wanyande
Profesa Peter Wanyande anakamilisha timu hiyo. Yeye ni mtaalamu wa utawala wa umma, taasisi za kidemokrasia na usimamizi wa serikali. Mbali na kuwa mhadhiri wa muda mrefu katika Chuo Kikuu cha Nairobi, aliwahi pia kuwa mshauri wa sera wa aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga. Kwa mujibu wa Ikulu, kila mmoja wa wasomi hao analeta utaalamu tofauti unaokamilishana. Kwa pamoja, wamekusanya mamia ya miaka ya uzoefu katika kufundisha, kufanya tafiti, kuhudumu serikalini na kutoa ushauri kuhusu sera za maendeleo. Serikali inaamini kuwa mchango wao utaisaidia Kenya kuandaa ruwaza mpya ya maendeleo itakayodumu kwa vizazi na kuendelea kutekelezwa bila kujali mabadiliko ya kisiasa baada ya uchaguzi.from Taifa Leo https://ift.tt/4MnFRYH
via IFTTT
Tags
TRENDING NEWS