
MWAKA mmoja kabla ya uchaguzi mkuu wa 2027, ubabe wa kisiasa umeanza kuchukua mkondo mwingine huku pesa zikimwagwa na viongozi wa mirengo mbalimbali.
Vyama vinapounda vikosi vyao vya kampeni, kuchagua wagombea na kujadiliana kuhusu miungano, suala la fedha limekuwa muhimu katika kuamua nani atakuwa na nafasi kubwa ya kushinda.
Kampeni za kisasa zinahitaji mabilioni ya fedha kugharimia helikopta, matangazo ya kidijitali, kura za maoni, mikutano na misafara kote nchini.
Hali hii imeibua hofu kuwa demokrasia inaweza kugeuka kuwa uwanja wa matajiri. Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imependekeza kanuni mpya za kudhibiti fedha za kampeni.
Kila mgombea wa urais, chama na mgombea mwingine atalazimika kuwa na akaunti maalumu ya benki ambapo fedha zote za kampeni zitaingizwa na kutolewa.
Wagombea pia watahitajika kutaja wafadhili wao na kuweka wazi matumizi yao. Mwenyekiti wa IEBC Erastus Ethekon alisema lengo ni kuhakikisha fedha hazipotoshi uamuzi wa wapigakura.
Chini ya mapendekezo hayo, mgombea urais ataruhusiwa kutumia hadi Sh4.44 bilioni, huku chama kinachowasilisha wagombea kuanzia urais hadi diwani kikiruhusiwa kutumia hadi Sh17.7 bilioni.
Hata hivyo, viongozi wa upinzani wanakabiliwa na changamoto ya jinsi ya kugharimia kampeni ya kitaifa dhidi ya serikali iliyoko madarakani.
Seneta wa Makueni Dan Maanzo amesema upinzani utategemea michango ya wananchi badala ya wafadhili matajiri au kutumia rasilimali za serikali.
“Rasilimali yetu kubwa ni wananchi,” alisema, akisisitiza kuwa kampeni za wananchi zinaweza kuwa nafuu kuliko zile zinazotegemea kununua kura.
Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi pia ameunga mkono mfumo wa kuchanga fedha kutoka kwa wananchi, akisema utasaidia kuzuia ufisadi unaoweza kuibuka baada ya uchaguzi kutokana na maslahi ya wafadhili.
Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna amekuwa akisisitiza msimamo huo na hata kukataa ahadi ya Katibu Mkuu wa COTU Francis Atwoli ya kuchangia Sh1 bilioni katika kampeni yake ya urais.
Hata hivyo, matamshi ya aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kuhusu jinsi alivyowahi kukusanya fedha za kampeni nje ya nchi yamezua mjadala kuhusu uwazi wa fedha za kisiasa.
Bw Gachagua alisema aliwahi kutumia marafiki wafanyabiashara kuingiza fedha nchini kwa sababu alihofia serikali ingezizuia iwapo zingepitia benki.
Wasiwasi kuhusu matumizi makubwa ya fedha umeongezeka kufuatia uchaguzi mdogo, hasa Ol Kalou, ambapo viongozi wa upinzani walidai serikali ilitumia rasilimali nyingi za umma kuwashawishi wapigakura.
Wataalamu wanasema kampeni za urais sasa zinahitaji helikopta, wataalamu wa mitandao ya kijamii, kampuni za matangazo, watafiti, walinzi na timu za uhamasishaji katika kaunti zote 47.
Profesa Karuti Kanyinga wa Chuo Kikuu cha Nairobi amewahi kukadiria kuwa kampeni kubwa ya urais inaweza kugharimu karibu Sh14 bilioni, huku mikakati mingine ikiweka gharama kati ya Sh10 bilioni na Sh20 bilioni.
Viongozi wa mashirika ya kiraia nao wanataka IEBC itekeleze kikamilifu Sheria ya Fedha za Kampeni ya 2013, ikiwemo kuwalazimisha wagombea kutaja wafadhili na matumizi yao.
Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanaonya kuwa upinzani hauwezi kushindana na serikali kwa nguvu za kifedha pekee.
Badala yake, wanapaswa kutumia teknolojia na kuwavutia vijana, hasa Gen Z, ambao wameonyesha uwezo wa kuendesha kampeni bila kutegemea miundo ya kawaida ya kisiasa.
Huku uchaguzi wa 2027 ukikaribia, mjadala mkubwa sasa ni iwapo ushindi utaamuliwa na sera na uwezo wa viongozi au ukubwa wa mifuko yao.
from Taifa Leo https://ift.tt/HUC1hdS
via IFTTT