Wetang’ula, Mudavadi waambia Sifuna bado hajaiva kupata kura kila pembe ya nchi

VITA vya kisiasa vya kung’ang’ania kura za Magharibi vimezidi kushika kasi baada ya Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi na Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula kupinga azma ya Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna kuwania urais 2027.

Kwa mara ya kwanza, viongozi hao wawili walimlenga moja kwa moja kiongozi huyo wa Linda Mwananchi, wakisema hana uzoefu wa kutosha kisiasa wala uungwaji mkono wa kitaifa kumwezesha kuingia Ikulu.

Mvutano huo unajiri huku eneo la Magharibi likitarajiwa kuwa na zaidi ya wapigakura milioni 3.3 katika uchaguzi wa 2027.

Akizungumza nyumbani kwa aliyekuwa mwenyekiti wa ANC Ken Lunani mjini Busia Jumapili, Bw Mudavadi alisema Bw Sifuna anakabiliwa na kazi ngumu kupata kura zinazohitajika kushinda urais.

“Ili uwe Rais lazima upate zaidi ya asilimia 25 katika kaunti 24. Hata ukipata kura zote katika kaunti hizi tano, bado utahitaji kura kutoka maeneo mengine, kwa sababu Katiba inahitaji kaunti 24,” akasema.

Alitaja Busia, Kakamega, Vihiga, Bungoma na Trans Nzoia, akisema hata iwapo mgombea angezinyakua zote, bado angehitaji uungwaji mkono mkubwa katika maeneo mengine.

Bw Mudavadi aliwakumbusha wapigakura kuwa aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga alipata kura milioni 6.5 katika uchaguzi uliopita, huku Rais William Ruto akipata karibu milioni 6.7.

Alisema kura za Magharibi pekee hazitoshi kwa mgombea yeyote kuingia Ikulu na akawahimiza wakazi wa eneo hilo kumuunga mkono Rais Ruto katika uchaguzi wa 2027.

Kwa upande wake, Bw Wetang’ula alisema mtu hawezi kuamka leo na kutangaza azma ya kuwa Rais bila kuwa na uzoefu wa kisiasa.

Alisema viongozi waliowahi kuongoza Kenya walipitia safari ndefu na madhila ya kisiasa yaliyowapa uzoefu wa kuendesha serikali kabla ya kufika Ikulu.

Spika huyo alisema nafasi nzuri zaidi kwa Magharibi kupata Rais ni mnamo 2032 badala ya 2027.

Kauli hizo zinajiri huku makundi kadhaa ya kisiasa yakipigania ushawishi katika eneo hilo.

Kambi ya Linda Mwananchi inayoongozwa na Bw Sifuna inajumuisha Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi, Seneta wa Kakamega Boni Khalwale, Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya na wabunge Wanami Namboka na Oundo Mudenyo.

Kambi nyingine inaunga mkono Serikali Jumuishi na inawashirikisha Mabw Mudavadi, Wetang’ula, Waziri wa Vyama vya Ushirika Wycliffe Oparanya na Katibu Mkuu wa COTU Francis Atwoli.

Pia kuna wabunge wa Kakamega wanaomsukuma Bw Oparanya awe mgombea mwenza wa Rais Ruto, huku kiongozi wa DAP-Kenya Eugene Wamalwa akiongoza kambi nyingine ya upinzani.

Mbunge wa Mumias Mashariki Peter Salasya anahoji ikiwa kambi ya Bw Sifuna inalenga kumng’oa Rais Ruto au inamakinikia kumjenga seneta huyo kuwa kinara wa Waluhya.

Umaarufu wa Bw Sifuna umeanza kuwatia hofu baadhi ya viongozi ndani ya Serikali Jumuishi.

Utafiti wa TIFA uliofanywa kati ya Juni 13 na 22 na kuwashirikisha watu 2,048 ulimweka Rais Ruto wa kwanza katika asilimia 24, huku Bw Sifuna akiwa wa pili kwa asilimia 15, kutoka asilimia 10 mnamo Mei.

Utafiti huo pia ulimweka Bw Sifuna mbele ya wagombea wengine wa urais katika eneo la Magharibi.



from Taifa Leo https://ift.tt/H7UZxQw
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post