Ngono, pombe, sigara zapigwa marufuku wakati wa tohara za Bukusu

KWA miezi mitano ijayo, maeneo ya Magharibi mwa Kenya yataingia katika msimu wa tohara za kitamaduni, huku wanaume wanaotekeleza jukumu hilo wakijitenga na maisha ya kawaida na kufuata kanuni kali. Wanaume hao wanaojulikana kama Ngariba kwa Kiswahili, na Omukhebi kwa lugha ya Bukusu, huamini kwamba tohara ni ibada muhimu ya kumfanya mvulana aingie katika utu uzima. Katika kipindi hicho, maisha yao hutawaliwa na nidhamu, kujinyima na uwajibikaji mkubwa. Hakuna kufanya ngono. Hakuna kuvuta sigara au kutumia dawa za kulevya. Hakuna kunywa pombe. Hakuna kuhudhuria mazishi. Na zaidi ya yote, hawapaswi kukiuka kanuni zinazohusiana na kisu kitakatifu kinachojulikana kama Lukhembe. Wanaotekeleza tohara hiyo wanaamini kwamba kuvunja kanuni hizo kunaweza kuathiri mchakato wa tohara na uponaji. Siminu Wekesa, aliye na tajriba kuhusu tohara, anasema marufuku hayo yanalenga kulinda heshima ya kiroho ya tohara, maadili ya jamii na usalama wa wavulana wanaopitia desturi hiyo. “Katika kipindi tunachowashughulikia wavulana katika tohara, haturuhusiwi kushiriki ngono hadi wavulana waanze kupona mwezi Oktoba kwa sababu ni kama kwenda vitani. Ukirejea au kuvunja kanuni hii, itachukua muda mrefu kwa watoto kupona kama inavyotarajiwa,” anasema Bw Wekesa. Marufuku ya ngono pia inawahusu wanaume wanaoshughulikia Busaa, kinywaji cha kienyeji ambacho hutumika katika sherehe za kitamaduni. Kifo pia kinaweza kumlazimisha Omukhebi kujiondoa katika shughuli hizo. Ngariba anayefiwa na mtu wa karibu wa familia, hasa mke, anatarajiwa kusitisha shughuli hizo na kufanyiwa tambiko la kujitakasa kabla ya kurejea mwaka unaofuata. Uvutaji sigara na matumizi ya dawa nyingine za kulevya pia hauruhusiwi wakati wa msimu huo. Wapashaji tohara wanasema baadhi ya masharti hayo yanalenga pia kuwalinda wavulana dhidi ya maambukizi na matatizo mengine ya kiafya. Rajab Kituyi, aliyeanza kupasha tohara mwaka wa 1982, anasema pombe hairuhusiwi kwa sababu shughuli hiyo inahitaji mikono thabiti, umakini na uwezo mzuri wa kuona. “Haturuhusiwi kunywa pombe, ili kuepuka matitizo ya kuona au kushindwa kushikilia kisu vizuri wakati wa tohara,” anasema. Omukhebi anatarajiwa kufanya kazi hiyo kwa usahihi mkubwa. Tohara isiyofanyika vizuri inaweza kumletea aibu na unyanyapaa Ngariba pamoja na mvulana, huku imani za kitamaduni pia zikihusisha makosa hayo na madhara ya kiroho. Kanuni hizo pia zinahusu uhusiano kati ya vizazi vya watoa tohara. Marufuku hiyo inalenga kuhifadhi heshima na uhusiano kati ya vizazi vya ngariba. Kisha kuna Lukhembe, kisu kitakatifu kinachotumiwa katika tohara. Kwa mujibu wa Bw Wekesa, kukiangusha kisu hicho, iwe kwa bahati mbaya au kwa makusudi, ni ukiukaji mkubwa wa kanuni. Ngariba anapaswa kusitisha shughuli mara moja na kusubiri msimu unaofuata. “Ukiangusha kisu, sitisha shughuli zako hadi msimu unaofuata. Ukipuuza na kuendelea na tohara, utaleta aina fulani ya mkosi,” anasema. Ngariba anapaswa kuondoka kimya kimya na kuepuka kueleza yaliyotokea njiani kuelekea nyumbani. Bw Wekesa anasema akiulizwa maswali, anapaswa kujibu neno moja pekee, “Ahoro”. Ngariba pia wanatarajiwa kuwa watu wenye maadili mema, wenye nidhamu na wanaoweza kuwa mifano kwa jamii. Pia hawapaswi kuwa na historia ya uhalifu. Kwa jamii ya Bukusu, tabia ya mtu anayemshughulikia mvulana inaweza kuathiri namna anavyoingia utu uzima. Hasira, ugomvi na mabishano pia hayaruhusiwi. Wakati wa msimu wa tohara, watoa tohara wanatarajiwa kubaki watulivu hata wanapochokozwa. Pamoja na kanuni hizo za kitamaduni, kuna umuhimu wa usafi na viwango vya kisasa vya usalama. Bw Wekesa, ambaye ni mwenyekiti wa Chama cha Wapashaji Tohara Kaunti ya Bungoma, anasema wazazi wanapaswa kuhakikisha mtu anayefanya tohara amepata mafunzo na cheti kutoka serikalini. “Usafi si jambo la kujadiliwa wakati wa tohara. Walioidhinishwa pekee ndio wanaoruhusiwa kufanya shughuli hiyo, na yeyote anayefanya bila cheti atachukuliwa hatua za kisheria,” anasema. Ngariba wanapaswa kudumisha usafi wa mwili, kukata kucha ziwe fupi, kuvaa vizuri na kuhakikisha mazingira pamoja na vifaa vinavyotumiwa ni safi.

from Taifa Leo https://ift.tt/aKTAfku
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post