
UCHAGUZI mkuu wa mwaka 2027 unapokaribia, juhudi za wanasiasa na wafanyabiashara wa siasa kutafuta vyama vya kisiasa zimegeuza mazingira ya siasa nchini kuwa uwanja wenye ushindani mkali, huku zaidi ya vyama 100 vikiwa vimesajiliwa.
Baadhi ya wanasiasa tayari wamenunua na kubadilisha sura ya vyama vilivyokuwepo huku wengine wakiharakisha kusajili vyama vipya. Hali hiyo imeibua maswali kuhusu nafasi halisi ya vyama vya kisiasa katika demokrasia ya Kenya.
Wachanganuzi wa siasa wanasema vyama vingi vya sasa havijajengwa juu ya misingi ya itikadi au sera za muda mrefu, bali vinatumika kama vyombo vya muda vya uchaguzi vinavyowapa viongozi nafasi ya kupata tiketi za moja kwa moja, kushawishi maamuzi na kujiongezea nguvu kisiasa.
Kwa mujibu wa Profesa XN Iraki wa Chuo Kikuu cha Nairobi, umiliki wa chama cha kisiasa sasa umegeuka kuwa biashara yenye faida kubwa.
“Kumiliki chama nchini Kenya sasa ni ishara ya hadhi na chanzo cha mapato. Wakati wa uteuzi wa wagombea, vyeti vya uteuzi hutolewa kwa malipo. Wanaotaka kuwania nyadhifa hulipa ada kubwa za uteuzi na hivyo vyama kuwa vituo vya kutengeneza fedha,” anasema.
Profesa Iraki anaongeza kuwa vyama vingi hutumika kwa uchaguzi mmoja tu kabla ya viongozi wake kuvitelekeza baada ya kufanikisha malengo yao.
“Mara nyingi mwenye chama hutumia chama kama matatu. Akifika anapotaka, hushuka na kukiacha,” anasema.
Mwanasheria na mchambuzi wa siasa Steve Kabita anakubaliana na mtazamo huo. Anasema kumiliki chama huwapa wanasiasa uhakika wa kushiriki meza ya mazungumzo ya miungano pamoja na kuwalinda dhidi ya migogoro ya uteuzi.
“Kiongozi wa chama huwa na ushawishi mkubwa katika mazungumzo ya kisiasa. Wanasiasa wengi huepuka hatari ya kunyimwa tiketi kwa kuanzisha au kumiliki vyama vyao wenyewe,” anasema.
Aidha, anasema chama kinaweza kuwa chanzo cha fedha kupitia Hazina ya Vyama vya Kisiasa inayofadhiliwa na walipa kodi. Vyama vinavyotimiza masharti ya sheria hupokea fedha za umma kulingana na idadi ya kura na viongozi waliochaguliwa katika uchaguzi uliopita.
Lakini wataalamu wanaonya kuwa hali hiyo inaweza kudhoofisha demokrasia.
Profesa Tom Nyamache wa Chuo Kikuu cha Turkana anasema vyama vinapogeuzwa biashara, sera na manifesto hupoteza maana.
“Vyama vinapokuwa kipaumbele cha faida binafsi, itikadi husukumwa pembeni na manifesto hubaki ahadi zisizo na uzito,” anasema.
Aliyekuwa Mbunge wa Mukurwe-ini Kabando wa Kabando pia anaonya kuwa Kenya inahitaji vyama imara vinavyoweza kuunganisha wananchi kitaifa badala ya vyombo vinavyotumiwa kusukuma maslahi ya mtu mmoja.
Homa ya kuanzisha vyama imeongezeka huku viongozi kadhaa wakijiandaa kwa uchaguzi wa 2027. Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna tayari amehifadhi jina la chama cha Linda Mwananchi huku Gavana wa Siaya James Orengo naye akitangaza mpango wa kuzindua chama chake.
Miongoni mwa vyama vipya vilivyosajiliwa ni Democracy for Citizens Party (DCP) ya aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, pamoja na vyama vingine kadhaa vinavyojiandaa kushiriki uchaguzi ujao.
Wanasiasa wengine kama Kawira Mwangaza, Ndindi Nyoro, Babu Owino na George Natembeya pia wamehusishwa na ununuzi au uongozi wa vyama vipya huku wakijiweka tayari kwa uchaguzi wa 2027.
Kwa sasa, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa inaonyesha kuna vyama 101 vilivyosajiliwa kikamilifu na vingine zaidi ya 30 vikiwa katika hatua ya usajili wa muda.
Msajili wa Vyama vya Kisiasa John Cox Lorionokou tayari ameonya kuwa atafanya ukaguzi wa makao makuu na matawi ya vyama hivyo ili kubaini vinavyotimiza matakwa ya sheria. Amesema vyama visivyo na ofisi katika angalau kaunti 24 vinaweza kuzuiwa kushiriki uchaguzi wa 2027.
Na uchaguzi unapokaribia, inaonekana kuwa usajili wa vyama vipya hauchochewi tu na demokrasia au itikadi za kisiasa, bali pia na tamaa ya nguvu, pesa na ushawishi. Hali hiyo imegeuza vyama vya kisiasa kuwa bidhaa inayotafutwa kwa bidii na wanasiasa wanaotaka kujihakikishia nafasi katika siasa za baada ya 2027.
Zaidi ya hayo, wimbi la kuanzishwa kwa vyama vipya limeibua hofu kuhusu mustakabali wa mfumo wa vyama vya kisiasa nchini. Wataalamu wanaonya kuwa bila mageuzi ya kina, Kenya inaweza kujikuta ikiwa na mamia ya vyama ambavyo vipo kwa jina pekee bila kuwa na ushawishi wa kweli kwa wananchi.
Sheria ya Vyama vya Kisiasa inaeleza kwamba jukumu la chama si kusimamisha wagombeaji pekee wakati wa uchaguzi. Vyama vinapaswa pia kuandaa sera za umma, kuelimisha wapigakura kuhusu masuala ya kitaifa, kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika uongozi na kusaidia kuendesha serikali. Hata hivyo, wachambuzi wanasema vyama vingi havitimizi wajibu huo na vinaonekana tu wakati wa kampeni.
Kumbukumbu za zinaonyesha kuwa miongoni mwa vyama vipya ni Democracy for Citizens Party (DCP) kinachohusishwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, pamoja na We Alliance Party na National Economic Development Party. Vingine ni People's Forum for Rebuilding Democracy, Nationalists Patriotic Party, Vision for Development Alliance (VIDA), Msingi wa Taifa na United Patriotic Movement inayohusishwa na Seneta wa Kakamega Boni Khalwale.
from Taifa Leo https://ift.tt/Rxaw7dp
via
IFTTT