Aliyekosa nafasi ya kusafiri asimulia alivyoepuka mauti katika ajali iliyoua waumini 17

Cornelius Korir, 41, anaamini yuko hai baada ya kukosa nafasi katika gari lililowabeba waumini 17 wa Kanisa Katoliki la St Mathias Mulumba, Parokia ya Mikindani, waliofariki katika ajali mbaya eneo la Salama. Korir, baba wa watoto watatu, alipanga kusafiri pamoja na waumini wenzake kuhudhuria Siku ya Kitaifa ya Maombi katika madhabahu ya Subukia. Hata hivyo, alivunjika moyo alipoambiwa kuwa gari walilokuwa wametengewa tayari lilikuwa limejaa.Kutokana na azma yake ya kushiriki maombi hayo, Chama cha Wamishonari wa Kikatoliki tawi la Mikindani kilimpa fedha za kukata tikiti ya usafiri wa umma. Alielekea katika afisi za Dreamline na kufanikiwa kuhifadhi nafasi.Baadaye jioni, akiwa kanisani kwa misa, alipata habari kuwa nafasi moja ilikuwa imepatikana katika gari la waumini. Hata hivyo, tayari alikuwa amenunua tikiti yake.“Nilikuwa tayari nimekata tikiti, kwa hivyo wakaamua kumpatia mtu mwingine nafasi hiyo,” alisema. Korir alisafiri kivyake na kufika salama Subukia. Alipofika ndipo alipopokea simu kutoka kwa mwenyekiti wa jumuiya yake akimfahamisha kuwa gari la waumini wenzake lilikuwa limepata ajali mbaya eneo la Salama.“Nilishtuka sana. Nilikuwa nimefika tu Subukia nilipoambiwa wenzangu wamefariki katika ajali,” alisema. Wingu la simanzi limetanda katika Kanisa Katoliki la St Mathias Mulumba, Parokia ya Mikindani, Mombasa, baada ya waumini 17 waliokuwa wakielekea Subukia, Kaunti ya Nakuru, kuhudhuria siku ya kitaifa ya maombi kufariki katika ajali ya barabarani eneo la Salama kwenye barabara kuu ya Mombasa-Nairobi. Waathiriwa hao waliondoka Mombasa wakiwa na matumaini ya kushiriki ibada ya kiroho, lakini safari yao ikakatizwa ghafla walipohusika katika ajali iliyojumuisha magari kadhaa katika eneo la Mlima Kiu. Kwa mujibu wa polisi, ajali hiyo ilitokea majira ya saa moja usiku baada ya lori lililokuwa likielekea Mombasa kujaribu kupita magari mengine katika sehemu ya kupanda mlima. Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Mukaa, Hussein Abduba, alisema lori hilo liligonga magari kadhaa baada ya dereva wake kuingia katika njia ya magari yanayokuja kutoka upande mwingine.“Lori hilo liligonga magari kadhaa baada ya dereva kujaribu kuyapita magari mengine kwenye njia ya kupanda mlima,” alisema. Habari za mkasa huo zilipowafikia waumini wa St Mathias Mulumba, mamia yao walifika kanisani kuthibitisha huku wengine wakianza safari ya kuelekea Sultan Hamud kutambua miili ya wapendwa wao. Padre Kizito Iloka alisema kanisa limepoteza waumini 17 katika ajali hiyo na kwamba, miili yao ilihifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Sultan Hamud. “Tuko hapa kuwaombea waumini wetu waliofariki katika ajali ya barabarani walipokuwa njiani kwenda Subukia. Tumepoteza waumini 17,” alisema.Katika misa maalumu ya maombi, Padre Augustine Lape aliwataka waumini kuwa na nguvu huku wakikabiliana na mshtuko wa msiba huo. “Jambo muhimu zaidi tunashughulikia kwa sasa ni jinsi ya kukabiliana na mshtuko huu kwa sababu hii ni habari ya kushtua. Chini ya uongozi wa Askofu Mkuu Martin Kivuva na Askofu Mkuu Mteule Dominic Kimengich, tutaendelea kutoa msaada wa kiroho kwa familia zilizoathirika,” alisema. Padre huyo pia aliomba hatua zaidi zichukuliwe kuzuia ajali za barabarani ambazo zimeendelea kuangamiza maisha ya Wakenya wengi kila mwaka.Miongoni mwa walioguswa zaidi na msiba huo ni Bi Sarah Nashivanda, 20, aliyempoteza mama yake. Kwa machozi, alisema mazungumzo yao ya mwisho yalifanyika saa mbili usiku kabla ya ajali.“Aliniambia walikuwa katika maombi na angenipigia simu asubuhi baada ya kufika Subukia. Hiyo ndiyo ilikuwa mara yangu ya mwisho kuzungumza naye. Kabla ya kuondoka aliniambia nijitunze na niwe salama,” alisema. Naye Sheila Rose, aliyempoteza shangazi yake Scholastica Ochieng, alisema bado haamini kwamba mkutano wao wa wiki hiyo ulikuwa wa mwisho. Marehemu ameacha watoto wawili.    

from Taifa Leo https://ift.tt/sZztRx5
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post