Mabadiliko Wakenya wanataka hayatasubiri muhula wa pili, Ruto aambia mawaziri

RAIS William Ruto Alhamisi alitoa onyo kali kwa Baraza lake la Mawaziri na maafisa wakuu wa serikali, akisisitiza kuwa serikali ya Kenya Kwanza lazima itimize ahadi ilizotoa kwa Wakenya au itakuwa inaisaliti nchi. Akizungumza katika Mkutano wa Tatu wa Uongozi wa Kitaifa uliofanyika Karen, Rais Ruto aliwakemea maafisa wake kwa kutawaliwa na uzembe, woga na siasa za kujilinda, akisema serikali yake haiwezi kulegea katika kipindi chake cha kwanza cha miaka mitano. "Sina nia hata kidogo ya kukwepa ahadi tulizotoa. Tunakusudia kuzitimiza, kwa sababu hivyo ndivyo tutakavyobadilisha Kenya," alisema Rais Ruto. Katika wakati ambao kuna shinikizo kubwa kuhusu gharama ya maisha, madai ya ukatili wa polisi na huduma duni kwa wananchi, Rais aliweka wazi kuwa visingizio havitakubalika tena. Alisisitiza kuwa mabadiliko hayawezi kusubiri hali nzuri ya kisiasa wala muhula wa pili. "Kama jambo linaweza kufanywa katika miaka mitano, kwa nini ulifanye kwa miaka 10?" alihoji. "Hivyo ndivyo tunakwama kama taifa, kwa sababu tunafanya maamuzi kwa kuzingatia hali ya kisiasa badala ya kile kilicho sahihi kwa taifa." Mkutano huo uliadhimisha nusu ya muhula wa utawala wa Kenya Kwanza, takribani miezi 30 tangu ilipoingia madarakani. Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki, Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi na Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei waliunga mkono wito wa Rais wa kuchukua hatua kwa haraka, kuratibu na kupata matokeo halisi. Profesa Kindiki alisema serikali ilipata nchi ikiwa katika hali ngumu ya kiuchumi kutokana na athari za janga la Covid-19, vita nchini Ukraine, na viwango vya juu vya riba vilivyoyumbisha uchumi wa ndani na kimataifa. "Tulichaguliwa kwa ajenda maarufu ya kujenga uchumi jumuishi ambapo mafanikio ya nchi yanagawanywa kwa matabaka yote. Malalamishi tunayasikia leo ni ya kawaida kwa sababu tulishinda kwa kutumia ahadi za kishujaa," alisema.

from Taifa Leo https://ift.tt/zWe86LN
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post