Mwanamume aliyefukuza polisi kwa panga ashtakiwa

MWANAMUME aliyenaswa kwenye video iliyosambazwa mitandaoni akiwafukuza polisi kwa kutumia panga wakati wa maandamano mjini Nakuru Jumatano iliyopita, alifikishwa mahakamani Alhamisi. Bw Paul Mriti, almaarufu Hassan Mti Mkavu, alifika mbele ya Hakimu mkuu Kipkurui Kibelion na kushtakiwa kwa makosa manne yanayohusiana na kuzuia polisi kutekeleza kazi yao na kuvuruga amani ya umma. Pia, alishtakiwa kwa kufanya maandamano yasiyo halali na kuwa na silaha katika sehemu ya umma kinyume cha sheria. Kulingana na upande wa mashtaka, Bw Mriti alisababisha fujo, kupiga kelele na kuwatisha kwa panga maafisa wa polisi Charles Francis na Koplo Kambo mnmo Juni 11 katika mtaa wa London, Kaunti ndogo ya Nakuru Magharibi. Shtaka la tatu lilisema mshtakiwa alipatikana akimiliki panga bila idhini au sababu ya kisheria. Silaha hiyo iliwasilishwa mahakamani kama ushahidi. Bw Mriti alikana mashtaka yote aliyosomewa. Hakimu Mkuu Kibelion alimwachilia kwa dhamana ya Sh100,000 na mdhamini wa kiasi sawa au kulipa Sh50,000 pesa taslimu. Kesi hiyo itatajwa Julai 1.

from Taifa Leo https://ift.tt/8PZavbf
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post