Waziri Ruku ataka Gen Z waachane na maandamano, waongee na serikali

WAZIRI wa Utumishi wa Umma, Geoffrey Ruku, mnamo wikendi aliwataka vijana wa Gen Z washiriki mazungumzo ili kutatua changamoto zinazokabili nchi badala ya kushiriki maandamano yanayoishia kwa uharibifu wa mali.

Bw Ruku alisema serikali iko tayari kushughulikia matakwa ya Gen Z huku akiwataka wafahamu nchi hupiga tu hatua kimaendeleo ikiwa kuna amani.

“Nguvu yetu kama nchi hutegemea umoja wetu na kukabili changamoto zetu kwa njia ya amani. Lazima tujizuie kuharibu na kusambaratisha nchi yetu na sote tushirikiane kujenga nchi,” akasema Bw Ruku.

Alikuwa akizungumza katika katika Kanisa Katoliki la Iriamurai, eneobunge la Mbeere Kusini.

Bw Ruku alimshutumu aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kwa kujaribu kugawanya nchi kikabila akisema hatafaulu kamwe.

Aliwataka Wakenya wawapuuze viongozi wa upinzani akisema hawana chochote cha kuwapa kimaendeleo.

Waziri huyo aligusia baadhi ya miradi ya serikali ambayo imeanzishwa eneo la Mbeere alilosema lilikuwa limebaguliwa kwa miaka mingi na tawala zilizopita.

Kati ya miradi hiyo ni ule wa maji ambao thamani yake ni Sh2 bilioni na Sh600 milioni zishawekwa ili kuanzisha mradi wenyewe.

Ujenzi wa Barabara ya Kiritiri–Kiambere na mradi wa maji wa Kamburu pia unaendelea pamoja na madarasa na shule Embu na kaunti nyingine.

Kitaifa, alisema walimu 76,000 wameajiriwa kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita huku walimu 24,000 zaidi wakitarajiwa kupewa ajira mnamo Disemba mwaka huu.

“Kama viongozi, lazima tujitume na kumakinikia uimarishaji wa huduma. Wakati wa siasa utakuja 2027 lakini kwa sasa tufanye kazi,” akaongeza Bw Ruku huku akisema kuanzishwa kwa vituo vya Huduma vimerahisisha utoaji wa huduma za serikali.

Waziri huyo aliandamana na Seneta wa Embu Alexander Mundigi, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Nchini (KNUT) Wilson Sossion, wabunge Elijah Njoroge (Gatundu Kaskazini) Wachira Karani (Laikipia Magharibi) na Nabart Muriuki wa Mbeere Kusini.

“Wakenya wanaishi kama ndugu na dada na lazima tuendelee kuungana na kuhubiri umoja wa waanzilishi wa taifa hili,” akasema Bw Sossion.

Bw Karani alishutumu upinzani kwa kufumbia macho miradi ya maendeleo inayotekelezwa na utawala wa sasa huku Bw Njoroge ambaye alichaguliwa kama mwaniaji huru, akiahidi kushirikiana na serikali na kuunga juhudi za kuhakikisha maeneo yote nchini yanapata maendeleo.

Bw Muriuki alisema eneo hilo linaunga mkono serikali akisema miradi inayoendelea itabadilisha maisha ya raia.

Aliwataka wakazi wawe nyuma ya Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki na Rais William Ruto kwenye nia yao ya kuunganisha nchi.

“Lazima tutaliki siasa za kikabila ili tuwe na nchi ambayo imeungana,” akasema Bw Muriuki.



from Taifa Leo https://ift.tt/qSfytcX
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post