Isaac Mwaura: Hakuna maandamano yoyote hapo kesho, endeleeni na kazi

MSEMAJI wa Serikali, Isaac Mwaura, amepuuza ripoti kuwa kutakuwa na maandamano kesho, akisema Wakenya wataendelea na shughuli zao kama kawaida. Bw Mwaura ameonya wale wanaolenga kuzua rabsha au kuvuruga shughuli za umma kuwa watakabiliwa kisheria. Bw Mwaura alisema Wakenya wapo huru kuadhimisha Juni 25, siku ambayo Gen Z waliingia bungeni, lakini wako huru kufanya hivyo kibinafsi. Gen Z wamesema kesho Jumatano itakuwa sikukuu ya kitaifa ya kuadhimisha mwaka moja tangu maandamano ya mwaka jana ambapo vijana waliuawa wakiendeleza maasi dhidi ya serikali. Wakati huo huo, zikiwa zimesalia saa za kuhesabu kabla ya maandamano yaliyopangwa na kizazi cha Gen Z hapo kesho, mirengo mbalimbali imeeleza kujiandaa kwao kwa shughuli hiyo ambayo huenda ikatikisa taifa huku wito wa amani ikitanda kutoka kwa wadau mbalimbali. Vijana wa Gen Z wanatarajiwa kuadhimisha mwaka mmoja tangu maandamano ya mwaka jana ambayo yalitikisa serikali na hata maafa ya zaidi ya watu 60 kutokea kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na mashirika mbalimbali. Maandamano hayo yalikuwa ya kupinga Mswada wa Fedha wa 2024 ambao ulipendekeza kuongezwa kwa ushuru. Wanasiasa, vijana, viongozi wa kidini na walinda usalama wote wamesema kuwa wako tayari kwa maandamano hayo ambayo kilele chake kitakuwa maombi ya ukumbusho na kuenzi Gen Z waliouawa kwenye bustani ya Uhuru, Nairobi. Kati ya maeneo ya jiji la Nairobi ambayo waandamanaji wamesema watapitia ni barabara za Moi Avenue, Tom Mboya, Harambee, Haile Selasie, Koinange, Muindi Mbingu, University Way, Parliament, City Hall, Aghan na Taifa. Kamanda wa Polisi ukanda wa Nairobi George Seda Ijumaa alithibitisha kuwa wamepokea barua na wameruhusu maandamano yaendelee huku akisema polisi wataimarisha usalama na kutoa ulinzi kwa watakaokuwa barabarani. Kamanda huyo hata hivyo, aliwataka waandamanaji wadumishe amani na wasiwachokoze maafisa wa usalama. Mnamo Jumanne wiki jana, maandamano jijini Nairobi yalijaa ghasia huku maafisa wa usalama wakionekana kupigwa jeki na magenge yaliyodaiwa kutumwa na wanasiasa kuwakabili waandamanaji. Maandamano hayo yalikuwa ya kulalamikia mauaji wa mwalimu na bloga Albert Ojwang’ na kwa mara mbili ambayo yamefanyika, yalijaa ghasia huku polisi wakipambana na waandamanaji. Huku polisi wakihakikisha kuwa kutakuwa na usalama, kuna hofu miongoni mwa wafanyabiashara jijini Nairobi hasa wale ambao wamepoteza mali kutokana na uporaji ambao umekuwa ukishuhudiwa wakati wa maandamano. Kwenye mawanda ya kisiasa, Viongozi wa upinzani nao wameonya vikosi vya usalama dhidi ya kutumia nguvu kupita kiasi na kuwajeruhi au kuwaua wanaoandamana. “Tuna hofu kuwa serikali haijajifunza kutokana na fujo zilizozuka 2023 na tena 2024 ambapo vijana sita waliuawa. Hatutaki damu imwagike tena,” akasema Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka. Naye aliyekuwa Jaji Mkuu David Maraga alilaumu serikali kwa uchunguzi duni huku akishutumu mwenendo ambao umeibuka wa wahuni kutumwa na wanasiasa kuingilia maandamano. Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja Jumapili usiku alikanusha kuwa alifadhili magenge kuwakabili waandamanaji na kuwalaumu wapinzani wake wa kisiasa aliodai wanalenga kumharibia sifa. “Nawaomba Wakenya na watu wa Nairobi wajiepushe na ghasia wanaposhiriki maandamano Jumatano. Nimeongea na kamanda kuhakikisha kuwa waandamanaji wanapewa ulinzi wanaposaka haki lakini kwa kufuata sheria,” akasema Bw Sakaja. Seneta wa Kilifi Stewart Madzayo naye amesema kuwa hawataki kusikia ghasia zozote au watu kujeruhiwa au kuuawa kesho. “Tunataka kumwaambia Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja kuwa watoto wetu watakuwa wakiandaa maandamano Jumatano. Msitumie afisi zenu kuwaumiza,” akasema Bw Madzayo jijini Mombasa mnamo Jumapili. Wanaharakati Boniface Mwangi na Hanifa Adan wamekuwa kati ya wale ambao wapo mstari wa mbele kuwashaajisha vijana wajitokeze kwa maandamano ya Jumatano. Viongozi wa kidini hawajawaachwa nyuma huku wakiomba maandamano yawe ya amani na kukemea mtafaruku wowote kati ya polisi na waandamanaji. Jumapili viongozi wa makanisa na wanafamilia ambao jamaa zao walijeruhiwa au kuuawa kwenye maandamano ya mwaka jana waliandaa maombi ya pamoja ya amani kwa ajili ya shughuli ya Jumatano. Wakati wa maandamano hayo walitoa wito kwa vijana wadumishe amani nayo serikali itoe fidia kwa familia zilizopoteza watoto wao kwenye maandamano ya mwaka jana. “Watoto wetu wanapotoka nje kutetea haki yao jinsi ilivyo kwenye katiba, wafanye hivyo kwa amani, wasiharibu mali ya mtu yeyote na askari wasiwapige,” akasema Kasisi wa Muungano wa Makanisa ya Kievangelisti Kepha Nyadega.

from Taifa Leo https://ift.tt/52OujyK
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post