Ajabu kituo cha afya kilichokuwa tegemeo kwa wakazi chabadilika makazi ya nyoka

Kituo cha Afya cha Kimalel, Baringo Kusini, kilikuwa zaidi ya kituo cha afya cha kawaida vijijini; kilikuwa nguzo ya uhai, mahali ambapo matumaini yalichipuka na maisha kuokolewa.

Katika kilele cha umaarufu wake, wagonjwa walimiminika kutoka maeneo mbalimbali ya Bonde la Ufa Kaskazini, wengi wakikabiliana na ugonjwa hatari wa kala-azar. Hapa , walipata matibabu ya kitaalamu, huduma muhimu na nafasi ya kuishi.

Leo, hali hiyo imepotea kabisa. Unapokaribia kituo hicho sasa, ukimya wa kutisha unachukua nafasi ya uhai uliokuwa hapo awali.

Hakuna foleni, hakuna harakati za haraka, wala sauti za wahudumu wa afya. Ukimya huo ni mzito, unaotia hofu, kinyume kabisa na historia yake.

Kudorora kwa kituo hicho kulianza miaka kadhaa iliyopita baada ya kituo cha matibabu ya kala-azar kuhamishiwa Chemolingot, katika eneo bunge la Tiaty ya Kati.

Baada ya uhamisho huo, mapigo ya moyo ya Kimalel yalianza kudhoofika: wagonjwa walipungua, rasilimali zilikauka na macho ya serikali yakahama.

Ziara katika kituo hicho Jumanne inaonyesha wazi madhara ya hali hiyo. Ukifika hapo, eneo la nje linakukaribisha kwa uharibifu: nyasi ndefu zilizoota hovyo, kuta zinazobomoka na njia zilizoharibika.

Vichaka vyenye miiba vimeanza kuingia karibu na majengo, vikichuku nafasi ya ardhi iliyokuwa ikitunzwa. Katika eneo hilo ambako nyoka ni hatari, kila hatua ni ya tahadhari.

Majengo yenyewe yanaonekana kuchoka kutokana na muda wa kutelekezwa. Ndani, hewa ni nzito yenye vumbi na harufu hafifu ya uozo.

Katika chumba cha upasuaji, wodi za wagonjwa waliolazwa, eneo la wagonjwa wa nje na maabara, dari zimetobolewa na mchwa, zikining’inia kwa hatari. Sakafu zimejaa vumbi na uchafu ulioganda kwa miaka.

Kuta zilizokuwa zimepakwa rangi safi sasa zimechubuka na kuchafuka.

Hata hivyo, licha ya hali hiyo, kituo hakijaachwa kabisa. Wahudumu wa afya bado wanaripoti kazini, wakipitia majengo yaliyoharibika na kuwahudumia wagonjwa wachache waliobaki kwa uwezo mdogo walio nao.

Uwepo wao ni ishara ya ustahimilivu, lakini pia onyo la kimya la mfumo ulioshindwa kuwasaidia.

Kutoka nje, Kituo cha Afya cha Kimalel kinaeleza simulizi ya matumaini yaliyopotea, uzembe na mmomonyoko wa imani ya wananchi kwa huduma za umma.

Kilichokuwa kituo cha kupigiwa mfano katika mapambano dhidi ya kala-azar sasa kinajitahidi hata kutoa huduma za msingi.

Bw Joel Chebolei, mkazi wa eneo hilo, anasema jamii imekuwa ikilalamika kwa miaka mingi bila majibu.

Mwanachama wa wbodi ya kituo hicho, Bw Solomon Kulei, alithibitisha hali hiyo akieleza kuwa paa zinavuja na miundombinu ya mbao inaliwa na mchwa baada ya dari kuanguka.

“Tumeomba msaada kutoka serikali ya ugatuzi ili kukarabati kituo hiki lakini imechelewa. Tulikuwa na chumba cha upasuaji kizuri lakini sasa hakifanyi kazi baada ya vifaa kuondolewa,” alisema.

Mkuu wa kituo hicho, Bw Silvano Kibet, alisema alipoletwa miaka miwili iliyopita kituo kilikuwa tayari kimeharibika sana na hakukuwa na mengi ya kuokolewa.

Hali hiyo iliwakumba pia wananachama wa Kamati ya Afya ya Seneti waliotembelea kituo hicho Jumanne wakati wa ukaguzi wa vituo vya afya kaunti ya Baringo.

Wakiongozwa na mwenyekiti wao, Seneta wa Uasin Gishu Jackson Mandago, pamoja na Seneta Richard Onyonka (Kisii) na Vincent Chemitei (Baringo), walikuta hali ya kusikitisha.

“Naomba sana Gavana Benjamin Cheboi na timu yake waone hali hii. Ni aibu kubwa. Kama Mkenya, nimeshtushwa kwamba vituo kama hivi bado vipo nchini,” alisema Seneta Onyonka.



from Taifa Leo https://ift.tt/tiD7pXz
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post