Amerika yampiga marufuku afisa mkuu wa polisi Tanzania kufuatia kuteswa kwa Mwangi

Serikali ya Amerika imempiga marufuku  afisa mmoja mkuu wa polisi wa Tanzania  na watu wengine w kutokana na madai ya kuwazuilia kinyume cha sheria, kuwatesa na kuwafanyia unyanyasaji wa kingono wanaharakati Boniface Mwangi na mwenzake wa Uganda Agather Atuhaire. Katika taarifa ya Mei 21, 2026, Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Amerika Marco Rubio alitangaza kuwa Idara ya Masuala ya Kigeni imemzima Kamishna Mkuu Msaidizi wa Polisi wa Tanzania, Faustine Mafwele, kutokana na madai ya kuhusika kwake katika ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu. Kwa mujibu wa Rubio, kuna taarifa za kuaminika zinazomhusisha Mafwele na unyanyasaji dhidi ya Mwangi na Atuhaire walipokuwa chini ya ulinzi wa polisi nchini Tanzania mnamo Mei 2025 na afisa huyo sasa amepigwa marufuku kuingia Amerika. “Idara ya Masuala ya Kigeni inampiga marufuku Kamishna Msaidizi wa Polisi wa Tanzania Faustine Jackson Mafwele chini ya Kifungu 7031(c) kutokana na taarifa za kuaminika kwamba alihusika katika ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu,” alisema Rubio. “Miaka miwili iliyopita, maafisa wa polisi waliwakamata, kuwatesa na kuwafanyia unyanyasaji wa kingono raia wa Uganda Agather Atuhaire na Mkenya Boniface Mwangi, ambao walikuwa Dar es Salaam kufuatilia kesi ya kiongozi wa upinzani Tundu Lissu. Hatua hii inamzima Mafwele kuingia Amerika,” aliongeza. Mwangi na Atuhaire walikuwa wamesafiri kwenda Tanzania kuhudhuria kesi ya kiongozi wa upinzani Tundu Lissu, ambaye anakabiliwa na mashtaka ya uhaini. Wanaharakati hao wawili waliripotiwa kutekwa kutoka hoteli yao muda mfupi baada ya kuwasili Dar es Salaam, kisha wakazuiliwa, kuhojiwa, kuteswa na kufanyiwa ukatili wa kingono kabla ya kutupwa karibu na mipaka ya nchi zao. Mwangi alipatikana akiwa hai Ukunda Mei 22, 2025, baada ya kuzuiliwa nchini Tanzania kwa zaidi ya siku tatu, huku Atuhaire akitupwa Mutukula kati ya Uganda na Tanzania siku moja baadaye. Kukamatwa kwao kulijiri baada ya watu watu wengine kukamatwa na kutimuliwa kutoka Tanzania akiwemo Martha Karua, Jaji Mkuu mstaafu Willy Mutunga na mwanaharakati Hanifa Adan.  Walikamatwa baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere. Baada ya kuachiliwa, Mwangi alisimulia masaibu yake  akiyataja kama moja ya aina mbaya zaidi za mateso aliyowahi kukumbana nayo, akilaumu maafisa wa Tanzania kwa kutisha kuwaaibisha hadharani iwapo wangezungumzia unyanyasaji waliopata. “Kila kilichotupata Tanzania kilifanyika kwa jina la Samia Suluhu, na tutahakikisha dunia inajua. Tutazungumza kwa niaba ya waathiriwa wa Tanzania wanaoogopa kuzungumza,” Mwangi alisema.

from Taifa Leo https://ift.tt/t65TDas
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post