
Mji wa Machakos ulivyobaki mahame wakati wa makabiliano kati ya polisi na wakazi walioandamana kupinga bei za mafuta. Picha|Benson Matheka[/caption]
Waziri wa Fedha John Mbadi aliongeza hasira kwa Wakenya aliposema mgomo huo haukuwa na sababu za msingi.
Bw Mbadi alikuwa amewaambia Wakenya kuwa kupanda kwa bei ya mafuta ni suala ambalo haliwezi kutatuliwa na nchi pekee kutokana na kwamba chimbuko lake ni vita vilivyokuwa vikiendelea Ukanda wa Mashariki ya Kati.
“Ninasikia watu wakisema mafuta ni nafuu Uganda na Tanzania. Ushahidi uko wapi? Ongezeko la bei ya mafuta nchini Kenya ni dogo zaidi ukilinganisha na majirani zetu,” akasema Bw Mbadi.
Katika jiji la Eldoret, vijana wenye hasira walifunga barabara kuu, na kuzua makabiliano na polisi ambao waliwatawanya kwa kutumia vitoza machozi.
Makabiliano hayo yalisababisha wasafiri kukwama vituoni huku biashara zikivurugika katika barabara ya Eldoret-Kitale.
“Hali si nzuri kabisa, na ikiwa itaendelea, uchumi wa nchi utaporomoka,” akasema dereva wa matatu wa Eldoret, Alex Kemboi.
Athari za mgomo huo pia zilihisiwa Kitale, Kaunti ya Trans Nzoia, ambapo huduma katika kituo cha mabasi zilisimama kabisa.
Kufikia saa nne asubuhi, kituo hicho kinachohudumia zaidi ya magari 1,000 kila siku kuelekea Turkana, Sudan Kusini na Uganda, kilikuwa hakina shughuli zozote
Madereva, utingo na watu wengine walicheza soka kupitisha muda huku shughuli zikiwa zimesimama.
Dereva anayehudumu katika barabara ya Kitale-Kisii, Joakim Namache, alisema wataendelea na mgomo hadi serikali ishughulikie suala la bei ya mafuta.
“Hatutalegeza msimamo wetu hadi serikali isikie malalamishi yetu. Tutaendelea na mgomo hadi hali ibadilike,” alisema.
Katika Lodwar na miji mingine ya Turkana, shughuli za usafiri zilipungua licha ya kutokuwepo maandamano makubwa.
Katika mji waw Naivasha, baadhi ya maduka yalivunjwa na bidhaa kuibwa huku gari moja la mwanakandarasi anayejenga barabara ya Rironi-Mau Summit ikichomwa.
Madereva wa malori, matatu na magari ya binafsi waliepuka barabara, na kuwalazimu wananchi kutembea kwa miguu kuelekea kazini.
Kule Nyahururu, polisi walipata wakati mgumu kulinda biashara zinazodaiwa kumilikiwa na wanasiasa wanaounga mkono serikali. Waandamanaji walijaribu mara mbili kuvamia Chieni Supermarket, inayomilikiwa na Mbunge wa Kieni, Njoroge Wainaina.
Kule Meru, barabara za kuingia na kutoka miji mbalimbali kama Meru, Nkubu, Timau, Mikinduri na Maua zilifungwa kwa mawe na moto wa matairi, hali iliyosimamisha shughuli zote.
Baadhi ya waendesha tuk tuk, boda boda na matatu ya safari fupi walikaidi mgomo na kuendelea kutoa huduma kule Murang’a Hata hivyo, baadaye walilazimika kusimamisha shughuli baada ya kukutana na makundi yenye hasira.
Katika Karatina, watu wasiopungua wanne walijeruhiwa huku biashara zikisimama kutokana na maandamano.
Katika kaunti za Kirinyaga na Embu, mamia ya wasafiri walikwama baada ya waendesha matatu kusimamisha shughuli zao kupinga kupanda kwa bei ya mafuta.
Katika Kirinyaga, waendeshaji waliegesha magari yao kwenye vituo vya mafuta mjini Ngurubani na Kutus, wakifanya maandamano na kudai bei zipunguzwe.
Pia walizuia barabara za Kutus-Kagio na Embu-Mwea, wakawasha moto wa matairi na kuongeza taharuki eneo hilo.
Katika Mombasa, matatu na tuk tuk zilibaki zimeegeshwa kwenye vituo na katika vituo vya mafuta, huku zile chache zilizojaribu kufanya kazi zikishambuliwa na kulazimishwa kuondoka barabarani.
Katika kituo cha Bombolulu kwenye barabara ya Mombasa-Malindi, waandamanaji walizuia barabara kwa mawe na kuwaonya madereva dhidi ya kubeba abiria.from Taifa Leo https://ift.tt/iok4DEB
via IFTTT
Tags
TRENDING NEWS