‘Kwa ground vitu ni different’: Ajira za Nyumba Nafuu zatofautiana na idadi inayotajwa na Rais

RAIS William Ruto na maafisa wake wamekuwa wakitia chumvi athari za Mpango wa Nyumba Nafuu (AHP) katika uundaji wa ajira, takwimu mpya rasmi zinafichua.

Takwimu za ajira katika sekta ya ujenzi nchini Kenya zinatofautiana na idadi ya nafasi za kazi zinazotajwa na Rais na maafisa wa serikali, na kuibua maswali kuhusu mchango halisi wa mpango huo miaka mitatu tangu uanzishwe.

Kulingana na Ripoti ya Hali ya Uchumi Kenya, jumla ya Wakenya waliokuwa wakifanya kazi katika sekta ya ujenzi mwaka jana walikuwa 728,400.

Kati yao 490,100 walikuwa katika sekta ya juakali na 228,300 katika ajira rasmi.

Shirika la Kitaifa kuhusu Takwimu (KNBS) lilisema kuwa ajira mpya 35,800 ziliundwa mwaka jana, hii ikiwa ongezeko la asilimia 5.2 kutoka 692,600 mwaka 2024.

“Sekta ya ujenzi iliendelea kuwa kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi mwaka 2025 ikichangia uwekezaji na ajira,” KNBS ilisema na kutaja mpango wa nyumba nafuu kama mojawapo ya wachangiaji.

Hata hivyo, takwimu hizo zinakinzana na zile ambazo zimetolewa na Rais kuhusu ajira zilizotokana na mpango huo mkuu wa serikali yake.

Tangu Septemba 2022 Rais Ruto amekuwa akipigia debe mpango huo kama nguzo kuu ya kutimiza ahadi ya ajira milioni moja kila mwaka.

“Mpango huu umeunda zaidi ya ajira 428,000,” alisema wakati wa hotuba yake ya hali ya taifa Novemba mwaka jana.

Aidha, taarifa ya Sera ya Bajeti ya Februari 2026 ilisema nyumba 214,057 zilikuwa zikijengwa kati ya 2022 na 2025, huku ajira zikitarajiwa kutinga milioni moja kufikia 2026.

Ripoti ya Mwenyekiti wa Bodi ya Nyumba Nafuu Jeremiah Simu pia ilitaja ajira 330,000 kama zile ambazo zilikuwa zimeundwa kufikia Juni 2025.

Utafiti uliodhaminiwa na Idara ya Makazi na kufanywa na kampuni ya Grant Thornton ulipata kuwa, ajira za moja kwa moja zilikuwa 464,759 kufikia Januari 2026.

Aidha, idadi ya jumla ya ajira zilizoundwa - za moja kwa moja na pia zisizo za moja kwa moja - ilikuwa 640,442.

Kati ya ajira hizo, 379,194 zilitokana na ujenzi wa nyumba nafuu, huku zingine zikiwa kutoka kwenye miradi ya ujenzi wa taasisi na masoko.

Ajira zisizo za moja kwa moja 175,683 zilihusisha sekta ya juakali na biashara ndogo.

Utafiti huo ulifanywa katika miradi 215 inayojumuisha nyumba 198,947.

Hata hivyo, uchambuzi wa takwimu za KNBS unaonyesha picha tofauti.

Tangu 2023, sekta nzima ya ujenzi imeongeza ajira 77,000 pekee, ikijumuisha maeneo kama ujenzi wa barabara.

Ajira ziliongezeka kutoka 651,400 mwaka 2022 hadi 728,400 mwaka jana.

Ongezeko kubwa lilirekodiwa 2023 (ajira 41,900) na 2025 (35,800), lakini bado liko chini ya madai ya serikali.

KNBS ilieleza kuwa ukuaji wa sekta hiyo ulichangiwa zaidi na ujenzi wa barabara na majengo ya makazi.

Katika kipindi cha miaka mitatu na nusu, serikali ilitumia Sh298 bilioni kwa barabara na Sh160 bilioni kwa nyumba.

Hata hivyo, Katibu wa Makazi Charles Hinga alikosoa KNBS, akisema walihusika katika utafiti huo lakini sasa wanatoa takwimu tofauti.

“KNBS hawajui wanachofanya. Tutatoa majibu kwa ukweli,” alisema Hinga.

Tofauti hizo za takwimu zinaendelea kuzua mjadala kuhusu athari halisi ya mpango wa nyumba nafuu kwa ajira nchini.



from Taifa Leo https://ift.tt/q5JKBUM
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post