
SHUGHULI za uchukuzi zinatarajiwa kulemezwa katika maeneo mbalimbali nchini huku mgomo wa matatu kwa kusudi la kupinga bei ya mafuta ukianza leo.
Watumiaji wa bidhaa za petroli, wakiwemo wanachama wa Muungano wa Wamiliki wa Matatu (MOA), wametangaza mgomo huo kupinga bei za juu ya mafuta zilizoongezwa wiki jana .
Mmoja wa Maafisa wa Muungano wa Wamilki wa Matatu maarufu kama ROA, Cornelius Chepsoi, alisema mgomo huo utaendelea hadi serikali itakapopunguza kwa kiasi kikubwa bei ya mafuta.
Hatua hiyo ya mgomo inafuatia tangazo la Mamlaka ya Kudhibiti Kawi na Petroli (EPRA) mnamo Alhamisi la kuongeza bei za mafuta za Mei hadi Juni 14.
Epra iliongeza bei ya dizeli kwa Sh46.29 kwa lita, huku bei ya petroli ikiongezeka kwa Sh16.65 kwa lita. Hivyo basi, petroli sasa inauzwa Sh214.25 kwa lita na dizeli kwa Sh242.92, huku bei ya mafuta ya taa ikibaki Sh152.78.
"Tunatangaza kama wafanyabiashara na watumiaji wa bidhaa za petroli kwamba kuanzia saa sita usiku wa leo (jana), hakutakuwa na shughuli yoyote ya usafiri kote nchini. Tunasimamisha safari zote," alisema Bw Chepsoi katika mkutano na wanahabari katika ukumbi wa Bomb Blast Memorial, Nairobi.
"Kuanzia sasa, hatutarejea kazini hadi serikali ipunguze bei ya mafuta nchini kwa sababu hali hii inatuathiri sote. Hatuzungumzi kwa niaba ya wamiliki wa matatu pekee, bali watumiaji wote wa bidhaa za petroli wakiwemo mama mboga," akaongeza.
Ongezeko hilo kubwa la bei linajiri licha ya ruzuku ya Sh15.67 kwa kila lita ya dizeli na Sh98.60 kwa kila lita ya mafuta ya taa.
Serikali haijatoa ruzuku kwa petroli huku ikijaribu kupunguza mzigo kwa Wizara ya Fedha ambayo tayari inakabiliwa na madeni ya ruzuku yanayokadiriwa kufikia Sh17 bilioni.
Kupanda kwa bei ya mafuta kunatokana na athari za vita kati ya Amerika-Israel na Iran, vilivyosababisha bei kupanda mnamo Machi na mwezi jana kote duniani. Hali hii inatokana na kufungwa kwa Njia-bahari ya Hormuz inayodhibitiwa na Iran.
Kwa sasa Kenya inaagiza mafuta chini ya mpango wa Serikali kwa Serikali (G-to-G). Wasambazaji wa mafuta walikuwa tayari wameonya kuhusu kupanda kwa bei licha ya uwepo wa mpango huo.
Akiwa ameandamana na Mwenyekiti wa MOA, Albert Karakacha na viongozi wengine, Bw Chepsoi aliishutumu serikali kwa kuongeza bei ya mafuta kwa zaidi ya asilimia 70 ndani ya miezi miwili tu.
Alisema uchumi wa nchi unategemea sana dizeli, ambayo imepanda kwa kiwango kikubwa na kusababisha watumiaji kubeba mzigo mkubwa wa gharama.
"Uchumi hauendeshwi na mafuta ya taa ambayo pia hutumika kama mafuta ya ndege. Tunategemea sana dizeli iwe ni viwanda vidogo au vikubwa. Wachimbaji visima, watengenezaji wa bidhaa wanateseka kutokana na gharama kubwa ya dizeli," akasema.
Wiki jana wadau wakuu katika sekta ya uchukuzi walitangaza kuwa mgomo huo hautajumuisha matatu tu bali pia mabasi, malori ya masafa marefu na hata teksi wakisema wanapanga kufunga barabara ili kulemaza usafiri.
Hata hivyo, Waziri wa Kawi Opiyo Wandayi pamoja na wandni wa Rais William Ruto wametetea ongezeko hilo la bei, wakisema limesababishwa na misukosuko ya soko la kimataifa kutokana na mzozo unaoendelea Mashariki ya Kati.
Akizungumza katika Kaunti ya Vihiga wakati wa uzinduzi wa miradi ya kituo cha kusambaza umeme, Bw Wandayi aliwashutumu wanaolaumu mpango wa G-to-G kwa bei ya juu ya mafuta kuwa si waaminifu.
"Mpango wa Serikali kwa Serikali haukuanza jana. Ulianzishwa mwaka 2023 wakati Rigathi Gachagua alikuwa naibu rais, na alikuwa mstari wa mbele kupokea shehena ya kwanza ya mafuta chini ya mpango huo. Imekuwaje sasa mpango huo uwe mbaya?" akauliza Bw Wandayi.
"Akiwa naibu rais ulikuwa mzuri. Huo ni unafiki. Siwezi kuendelea kunyamaza kama waziri," akaongeza.
Wakizungumza katika hafla ya shukrani katika Shule ya Wasichana ya Kapkoiga eneobunge la Kesses, Kaunti ya Uasin Gishu, wandani wa Rais walisisitiza kuwa serikali imefanya kila iwezalo kulinda wananchi dhidi ya kupanda kwa bei ya mafuta.
"Serikali haiwezi kulaumiwa kikamilifu kwa ongezeko la bei kwa kuwa usambazaji na mahitaji ya mafuta yanategemea mambo ya nje ambayo Kenya haiwezi kudhibiti," akasema Seneta wa Uasin Gishu Jackson Mandago.
Mbunge wa Kesses Julius Ruto alisema serikali imejitahidi kulinda Wakenya dhidi ya athari ya bei ya mafuta akisema gharama ya juu ni kutokana na yaliyojiri Mashariki ya Kati.
"Serikali imefanya kila iwezalo kudhibiti bei za mafuta licha ya shinikizo la kimataifa. Tunachoshuhudia ni mgogoro wa kimataifa unaoathiri uchumi mwingi," alisema.
Kauli zao ziliungwa mkono na Katibu wa Wizara ya Elimu Profesa Julius Bitok pamoja na Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei.
from Taifa Leo https://ift.tt/bv7TDZa
via IFTTT
Tags
TRENDING NEWS