Serikali haina pesa za kutosha kurejesha Wakenya waliokwama vitani Urusi – Mudavadi

SERIKALI imekiri kuwa haiwezi kuthibitisha idadi kamili ya Wakenya waliojiunga na jeshi la Urusi ikisema wengi wao husafiri kwa siri bila kufahamisha familia zao wala ubalozi wa Kenya.

Waziri Mkuu Musalia Mudavadi, ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Kigeni, aliambia Kamati ya Seneti kuhusu Ajira na Ulinzi wa Wafanyakazi kuwa serikali bado inapokea taarifa mpya kutoka maeneo ya vita, jambo linalofanya takwimu kuendelea kubadilika.

Bw Mudavadi aliongeza kuwa serikali haina pesa za kuwarejesha nyumbani Wakenya wanaokumbwa na mateso wakifanya kazi nje ya nchi.

“Tulikuwa tunazungumzia wale tulioweza kuthibitisha. Inawezekana wako zaidi,” alisema Musalia Mudavadi mbele ya maseneta.

Alisema baadhi ya Wakenya hao waliingia maeneo ya vita bila kuarifu familia zao wala ubalozi wa Kenya nchini Urusi, hivyo kufanya iwe vigumu kwa serikali kuwafuatilia.

Kwa mujibu wa wizara hiyo, serikali ilianza kwa kuthibitisha visa 252 vya Wakenya waliohusishwa na kujiunga na vikosi maalum vya kijeshi vya Urusi, lakini idadi hiyo sasa imeongezeka hadi 291 huku taarifa mpya zikiendelea kujitokeza.

Katika taarifa iliyowasilishwa kwa Seneti, wizara ilisema Wakenya 47 tayari wamerejeshwa nchini huku familia zikiripoti vifo 10, ingawa serikali bado haijathibitisha rasmi vifo hivyo.

Waziri huyo alisema serikali ya Kenya imezungumza na z Urusi kuhusu suala hilo na kupewa hakikisho kuwa hakutakuwa tena na uajiri wa Wakenya katika vikosi vya kijeshi vya Urusi.

Wakati huo huo, Mudavadi aliambia Seneti kuwa balozi za Kenya nje ya nchi zinakabiliwa na ukosefu mkubwa wa fedha, jambo linalodhoofisha uwezo wa serikali kusaidia Wakenya waliokwama nje ya nchi.



from Taifa Leo https://ift.tt/OqLvZYt
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post