TSC yamulikwa kwa kukosa usawa katika kuwaajiri walimu

TUME ya Huduma kwa Walimu (TSC) inapigwa darubini na wadau wa elimu kuhusu kile kinachodaiwa kuwa upendeleo katika usambazaji wa walimu katika shule za umma.
Katika Kongamano la Kitaifa la Elimu mjini Naivasha wadau wa elimu walielezea wasiwasi kuhusu ukosefu wa usawa unaojitokeza kila mara ambapo kuna baadhi ya shule zilizo na walimu kupita kiasi huku nyingi zikishuhudia uhaba.
Mwanachama wa Baraza la Chuo Kikuu cha Multimedia, Dkt Beatrice Tonui, aliibua tafrani alipofichua kuwa kipindi akitekeleza mafunzo yake ya uanagenzi nyanjani alizuru shule moja katika Kaunti ya Kericho na kushangaa kupata mgao wa idadi ya walimu kwa wanafunzi haiendani.
“Nilitembelea shule na kustaajabu nilipogundua ina wanafunzi 30 na walimu 10. Tatizo hili ni kubwa linalohitaji suluhisho la dharura kuhakikisha kuna usawa katika shule za nchi hii,” alisema.
“Kuna raslimali muhimu zinatumiwa vibaya na inasikitisha. Mbona TSC isigawe walimu kwa usawa?” akauliza.
Dkt Tonui alihimiza tume kuendesha zoezi la kutathimini idadi ya walimu katika kila shule nchini ikilinganishwa na idadi ya wanafunzi.
“Najua hiyo si shule pekee iliyojipata katika hali hiyo. Baadhi ya shule zina idadi kubwa ya walimu zingine zikiwa na wachache, kinyume na mgao unaostahili wa idadi ya walimu kwa wanafunzi. Ni muhimu, hivyo basi, kuendesha zoezi la kusawazisha idadi ya walimu kote nchini kote,” alieleza.
Mdahalo huo uliibua kwamba baadhi ya shule zenye idadi chache ya wanafunzi zina wahudumu wengi kupita kiasi, nyingine zenye wanafunzi wengi zina upungufu mkubwa wa walimu.
Wadau kadhaa wa elimu waliozungumza katika kongamano hilo Naivasha wanataka suala hilo lisiluhishwe kuhakikisha usawa katika usambazaji wa walimu shule zote.
“Ni sharti TSC ihakikishe kuwa walimu wote ikiwemo wale walio maeneo ya mashinani zinapata idadi ya kutosha ya walimu. Usambazaji wenye usawa wa walimu ni muhimu sana. Kuna haja ya usawa. Hatuwezi kuendelea na hali ambapo shule zenye wanafunzi wawili zina walimu 10 huku taasisi nyinginezo zikihangaika,
"Serikali inapaswa kutumia teknolojia kukusanya data inayopaswa kuelekeza maamuzi ya TSC kuhusu wahudumu,” alisema Profesa Michael Ntabo Mabururu, mtafiti na naibu chansela anayesimamia Elimu na Masuala ya Wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Rongo.
Katibu wa Wizara ya Elimu, Profesa Julius Bitok vilevile alikiri kuwa TSC imekosa kusambaza kwa usawa walimu katika shule zote nchini.
“Suala kuhusu usambazaji wa walimu ni kero kuu. Ni bayana TSC imeshindwa kusambaza walimu shuleni kwa usawa nchini kote. Kwa sasa tuna walimu 458,000 walioajiriwa,” alisema.


from Taifa Leo https://ift.tt/wTk9WdY
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post