Wakenya 17.7 m wanategemea mkopo wa Fuliza

MIKOPO inayotolewa kupitia huduma ya Fuliza ya Safaricom imevuka Sh1 trilioni kwa mara ya kwanza katika mwaka ulioishia Machi 2026, ikionyesha ongezeko kubwa la Wakenya wanaotegemea mikopo ya haraka kwa mahitaji ya msingi kama chakula, kodi ya nyumba na dawa.
Kwa mujibu wa ripoti ya kampuni hiyo ya mawasiliano, jumla ya mikopo iliyotolewa kupitia huduma hiyo ilifikia Sh1.46 trilioni, ikiwa ni ongezeko la asilimia 49.3 kutoka Sh981.6 bilioni mwaka 2025.
Fuliza, ambayo inawawezesha wateja wa M-Pesa kufanya malipo hata kama hawana salio la kutosha, hutolewa kwa ushirikiano na benki za NCBA Kenya na KCB Kenya.
 Safaricom inasema ongezeko hilo limetokana na kuongezeka kwa idadi ya watumiaji pamoja na kupandishwa kwa viwango vya mikopo mapema Januari 2026.
Huduma hiyo sasa inatumiwa na wateja binafsi na biashara ndogo ndogo, na imeendelea kuwa sehemu muhimu ya mfumo wa kifedha wa M-Pesa.
Hata hivyo, matumizi makubwa ya Fuliza yanaonyesha pande mbili tofauti za uchumi.
Kwa upande mmoja, huduma hiyo imeleta urahisi wa miamala na kuokoa wateja katika hali za dharura za kifedha.
Kwa upande mwingine, inaonyesha ongezeko la Wakenya wanaokopa kukidhi mahitaji ya kila siku badala ya uwekezaji.
Kupungua kwa shughuli za kiuchumi, kupanda kwa gharama za maisha na mishahara inayoongezeka polepole vimechangia hali hiyo.
Takwimu zinaonyesha kuwa mishahara halisi ilipanda kidogo hadi Sh56,566 mwaka 2025 kutoka Sh55,450 mwaka 2024, lakini bado iko chini ya kiwango cha Sh62,256 kilichorekodiwa mwaka 2020.
Hii inaashiria kupungua kwa uwezo wa kununua kwa takriban Sh5,690 katika kipindi cha miaka sita.
Mwaka 2024, sekta ya benki ilibaini kupungua kwa mikopo ya uwekezaji kama ujenzi na upanuzi wa biashara, huku mikopo ya matumizi ya haraka ikiongezeka.
Hali hii inaonyesha mabadiliko ya tabia ya wakopaji kuelekea mikopo ya kujikimu.
Fuliza sasa ina wateja takriban milioni 17.7, kutoka milioni 7.9, huku kiwango cha wastani cha mkopo kikipungua hadi Sh217.90.
Safaricom ilipata Sh6 bilioni kama mapato kutoka huduma hiyo, ongezeko la asilimia 46.
Ada za Fuliza hutofautiana kulingana na kiwango cha mkopo, pamoja na malipo ya kila siku na ushuru wa serikali.
Hata hivyo, kiwango cha ulipaji kimeendelea kuwa kizuri, kikionyesha kuwa bado kuna nidhamu ya wastani ya kulipa mkopo.
Safaricom inasema imeongeza viwango vya mikopo kwa kutumia Akili Unde (AI) kutathmini tabia ya wateja, hatua iliyoongeza matumizi ya huduma hiyo.
Pia imezindua Fuliza ya Biashara ili kusaidia wafanyabiashara wadogo kupata mikopo ya haraka.
Hata hivyo, wataalam wanaonya kuwa kuongezeka kwa watu kutegemea mikopo ya dharura kunaonyesha shinikizo la kiuchumi linalowakabili Wakenya wengi.


from Taifa Leo https://ift.tt/jlYB394
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post