
MIEZI 14 kabla ya uchaguzi mkuu wa 2027, Rais William Ruto anategemea Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) kusimamia utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo inayochukuliwa kuwa nguzo muhimu katika kampeni yake ya kutafuta muhula wa pili.
Kuanzia ujenzi wa viwanja vya michezo 27 kote nchini, hospitali, viwanja vya ndege, daraja hadi mradi wa kufufua Mto Nairobi, jeshi limepewa jukumu la kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyohitajika.
Hatua hiyo inaonekana kuashiria imani kubwa ya Rais Ruto kwa nidhamu, utaalamu na uwezo wa jeshi kusimamia miradi mikubwa ikilinganishwa na baadhi ya wizara ambazo zimelaumiwa kwa kuchelewesha utekelezaji wa miradi ya serikali.
Miongoni mwa miradi inayosimamiwa na KDF ni Uwanja wa Talanta Sports City unaogharimu Sh48 bilioni jijini Nairobi, ambao sasa umepewa jina la Raila Amollo Odinga International Stadium.
Uwanja huo wenye uwezo wa kuketi mashabiki 60,000 unatarajiwa kuwa moja ya miundombinu muhimu wakati Kenya itakapoandaa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2027.
Mradi mwingine mkubwa ni Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Matibabu ya Kisasa mjini Eldoret inayogharimu Sh50 bilioni na yenye uwezo wa kuhudumia wagonjwa 4,000.
Hospitali hiyo inajengwa kwa awamu mbili na inatarajiwa kuwa mojawapo ya hospitali kubwa zaidi barani Afrika.
Pia kuna mradi wa kufufua Mto Nairobi wenye thamani ya Sh50 bilioni unaolenga kubadilisha mazingira ya mto huo kwa kujenga nyumba za kijamii, njia za watembea kwa miguu, njia za baiskeli, mifumo ya maji taka, daraja na maeneo ya burudani.
[caption id="attachment_185018" align="alignnone" width="1164"]
Talanta Sports City Jijini Nairobi. Picha|Hisani[/caption]
Katibu katika Wizara ya Ulinzi, Dkt Patrick Mariru, alisema serikali imeamua kutumia utaalamu wa KDF katika uhandisi na usimamizi wa miradi ili kuhakikisha miradi ya kitaifa inakamilika kwa wakati uliowekwa.
“Chini ya uongozi wa Rais, jeshi linasimamia ujenzi wa miradi ya maji, afya, barabara na michezo ili kusaidia kufanikisha maono ya kuifanya Kenya kuwa taifa lenye uchumi wa kiwango cha juu,” alisema.
Aliongeza kuwa jukumu la KDF si kutoa zabuni wala kupanga bajeti, bali ni kusimamia utekelezaji na kuhakikisha ubora wa kazi unaafikiwa.
Mbunge wa Belgut na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi katika Bunge la Kitaifa, Nelson Koech, alisema kuhusishwa kwa jeshi katika miradi hiyo ni ishara kuwa baadhi ya wizara zimeshindwa kutekeleza miradi kwa ufanisi.
“Kwa jeshi kupewa jukumu hili ni lawama ya moja kwa moja kwa baadhi ya wizara. Inaonyesha kuwa kuna changamoto za ufanisi na ndiyo maana serikali imeamua kutumia uwezo wa KDF kuhakikisha miradi inakamilika,” alisema.
Kwa mujibu wa Bw Koech, jeshi lina sifa ya nidhamu, uwajibikaji na kutovumilia ufisadi, jambo ambalo limefanya serikali kuliamini katika kusimamia miradi yenye thamani ya mabilioni ya pesa.
Wakili Kipkirui Kemboi Kap Telwa, alisema hatua ya Rais Ruto kupatia KDF jukumu kubwa katika miradi ya maendeleo inaonyesha jinsi anavyotaka kuona ahadi alizotoa kwa wananchi zikitimizwa kabla ya uchaguzi mkuu ujao.
“Hii inaonyesha kuwa Rais ameona changamoto zilizopo katika baadhi ya idara za serikali na ameamua kuamini jeshi kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo,” alisema.
Hata hivyo, alionya kuwa serikali inapaswa kuwa makini ili kuepuka kuingiza jeshi katika siasa za uchaguzi.
“Ni jambo jema kutumia uwezo wa KDF, lakini ni muhimu kuhakikisha jeshi halihusishwi katika siasa kwa sababu limeendelea kuwa taasisi inayoheshimika nchini na barani Afrika,” alisema.
Miongoni mwa miradi mingine inayosimamiwa na jeshi ni Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Bomas (BICC) kinachogharimu Sh42 bilioni, uwanja wa ndege wa Lokichogio Turkana, hospitali mpya katika Kaunti ya Narok na viwanja kadhaa vya michezo katika kaunti mbalimbali.
Dkt Mariru alisema viwanja 27 vya michezo nchini kwa sasa viko chini ya usimamizi wa jeshi, hatua ambayo haijawahi kushuhudiwa katika historia ya Kenya.
“Katika miezi miwili ijayo tutakuwa tumekamilisha na kukabidhi Uwanja wa Talanta kwa Rais. Huu ni ushahidi wa umakini wa jeshi katika kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati,” alisema.
Kwa sasa, viwanja vya michezo katika maeneo ya Kericho, Bomet, Nandi, Kisii, Nyamira, Nakuru, Siaya, Lodwar, Kitale, Eldoret, Meru, Mavoko, Kilifi, Busia, Kakamega, Vihiga, Maua, Wajir na Mandera ni miongoni mwa vinavyosimamiwa na KDF.
from Taifa Leo https://ift.tt/Zs6g2Qf
via IFTTT