
VIONGOZI wakuu wa usalama nchini wanatarajiwa kukutana Jumatatu chini ya mwavuli wa Baraza la Ushauri wa Usalama wa Kitaifa (NSAC) kujadili wimbi la vurugu katika shule mbalimbali nchini.
Mkutano huo unatarajiwa kuangazia ongezeko la visa vya moto, fujo za wanafunzi na kufungwa kwa baadhi ya taasisi za elimu katika wiki tatu zilizopita, hali ambayo imezua hofu miongoni mwa wazazi na jamii.
Ingawa Inspekta Jenerali wa Polisi hahusiki moja kwa moja kuweka ajenda, duru zasema suala la usalama shuleni litapewa kipaumbele kutokana na uzito wake.
Tayari kumekuwepo na mijadala kuhusu uwezekano wa kufunga shule mapema au kuharakisha likizo ya muhula wa kati ili kupunguza mivutano, ingawa uamuzi huo unategemea matokeo ya kikao hicho. Wizara ya Elimu, hata hivyo, imekanusha uwezekano wa kufunga shule mapema. Katibu wa Elimu ya Msingi, Profesa Julius Bitok, alisema zaidi ya asilimia 99 ya shule zinaendelea na masomo kama kawaida.
“Kwa takwimu zetu, hali ni tulivu katika shule nyingi. Hakuna sababu ya kubadilisha kalenda ya masomo,” alisema Prof Bitok.
Hali hii inajiri baada ya matukio kadhaa ya moto na vurugu kuripotiwa, likiwemo tukio la kusikitisha katika Utumishi Girls Academy, Gilgil, ambapo wanafunzi 16 walifariki kwenye mkasa wa moto.
Baada ya tukio hilo, shule nyingine ikiwemo Maranda, St Paul’s Githakwa, Tarakwa na Alliance High School zimeripoti visa vya moto au dalili za vurugu, hali iliyopelekea baadhi kufungwa kwa muda. Maafisa wa usalama na elimu sasa wanachunguza iwapo matukio haya ni ya pekee au sehemu ya mwelekeo mpana wa changamoto za nidhamu na msongo wa wanafunzi.
Matokeo ya mkutano wa NSAC yanatarajiwa kubainisha hatua za haraka zitakazochukuliwa kukabiliana na hali hiyo.
from Taifa Leo https://ift.tt/pRBock6
via IFTTT
Tags
TRENDING NEWS