Anayedaiwa kuanika safari za Ruto mtandaoni aachiliwa huru

MAHAKAMA Kuu imeamuru kuachiliwa huru bila masharti kwa Halima Ngache, mwanamke aliyekamatwa kwa madai ya kufuatilia safari za anga za Rais William Ruto na kuzichapisha kwenye mitandao ya kijamii.
Bi Ngache alikamatwa nyumbani kwake Mombasa na kuhamishiwa Nairobi, ambako Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) iliomba azuiliwe kwa siku saba ili kukamilisha uchunguzi. Hata hivyo, Mahakama ya Milimani iliruhusu azuiliwe kwa siku tatu pekee.
Baadaye aliwasilisha kesi katika Mahakama Kuu akidai hakuelezwa sababu za kukamatwa kwake na kwamba maafisa wa polisi hawakuwa na kibali cha mahakama cha kumkamata.
 Mahakama Kuu iliagiza aachiliwe mara moja bila masharti na afike mahakamani Jumatatu, Julai 6, kwa maelekezo zaidi.
Mahakama ya Milimani ilielezwa kuwa baada ya uchunguzi kukamilika, faili itawasilishwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), Bw Renson Ingonga, ili aitathmini na kuamua iwapo Bi Ngache atafunguliwa mashtaka ya uhalifu wa mtandaoni.
DCI iliambia mahakama kuwa uchunguzi utaendelea kuhusu madai ya unyanyasaji wa mtandaoni na matumizi mabaya ya mifumo ya kompyuta.
Wachunguzi walidai wanaamini kuwa Bi Ngache hakuwa peke yake na kwamba kuna washukiwa wengine waliokuwa wakichapisha ratiba za safari za Rais kwenye mitandao ya kijamii. Pia, waliomba muda zaidi kufanya uchunguzi wa kisayansi wa vifaa vya kielektroniki vilivyopatikana kutoka kwake ili kubaini iwapo watu wengine walihusika.
Mahakama ilielezwa kuwa Bi Ngache anachunguzwa kwa madai ya kukiuka Sheria ya Matumizi Mabaya ya Kompyuta na Uhalifu wa Mtandaoni baada ya akaunti moja katika mtandao wa X, zamani Twitter, kuchapisha taarifa zilizodaiwa kufichua ratiba za safari za Rais pamoja na nambari ya usajili wa ndege aliyotumia wakati wa ziara rasmi barani Ulaya.
Katika hati ya kiapo, Koplo Edwin Metto wa Kitengo cha Uhalifu Mkubwa cha DCI alisema uchunguzi ulianza baada ya akaunti hiyo kuchapisha taarifa zilizokuwa zikifuatilia mienendo ya Rais. Mojawapo ya machapisho hayo ilidai Rais Ruto aliondoka Ubelgiji kuelekea Norway kwa ndege ya kukodi, huku chapisho jingine likitaja nambari ya usajili wa ndege hiyo.
Koplo Metto alisema machapisho hayo yalizua hofu kuhusu usalama wa Rais na kwamba madhumuni ya kuyachapisha bado yanachunguzwa.
Aliongeza kuwa Bi Ngache alipokamatwa Mombasa alipatikana na simu mbili za mkononi na vifaa vitatu vya kuhifadhi data ambavyo vitafanyiwa uchunguzi wa kisayansi ili kubaini uhusiano wake na machapisho hayo.
Mpelelezi huyo pia aliambia mahakama kuwa hata baada ya Bi Ngache kukamatwa na kusafirishwa kutoka Mombasa hadi Nairobi, akaunti hiyo ya X iliendelea kuchapisha taarifa, hali iliyowafanya wachunguzi kuamini huenda inasimamiwa na zaidi ya mtu mmoja.
Awali DCI ilikuwa imeomba siku saba za kukamilisha uchunguzi, ikisema bado inasubiri matokeo ya uchunguzi wa vifaa vya kielektroniki pamoja na taarifa kutoka taasisi nyingine kabla ya kuwasilisha faili kwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma.
Hata hivyo, mahakama ilikataa ombi hilo na kuamua kuwa siku tatu zilitosha kwa uchunguzi huo. Bi Ngache anatarajiwa kufikishwa mahakamani Julai 6, 2026, kwa maelekezo zaidi.


from Taifa Leo https://ift.tt/AaW82wH
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post