Wandani wa Ruto waanza kusuka mikakati ya 2032

VIONGOZI wanaounga mkono serikali jumuishi Ijumaa walifanya mkutano mkubwa wa kisiasa mjini Eldoret kumpigia debe Rais William Ruto 2027 huku wakianza pia kuweka msingi wa siasa za mrithi wake mwaka 2032. Mkutano huo uliowaleta pamoja wabunge kutoka vyama vinavyounda muungano wa Kenya Kwanza na baadhi ya viongozi wa ODM, uligeuka kuwa jukwaa la kuhimiza Wakenya kumpa Rais Ruto muhula wa pili na wa mwisho ili akamilishe miradi yake ya maendeleo. Viongozi hao walisema wapinzani hawana sera mbadala za kuendeleza nchi na wakawataka Wakenya ‘wasicheze kamari’ na kura zao katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027. Akiongoza mkutano huo uliofanyika katikati mwa jiji la Eldoret, Spika wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetang'ula, alisema serikali ya Rais Ruto imeleta maendeleo katika maeneo yote ya nchi bila kujali tofauti za kisiasa au kikabila. “Tangu Rais Ruto aingie madarakani, kila sehemu ya Kenya imepata maendeleo makubwa. Maendeleo hayategemei tena eneo lilivyopiga kura au kabila la wakazi wake,” alisema. Alisema serikali imeboresha maisha ya wakulima hasa katika eneo la North Rift kupitia ruzuku na mipango mbalimbali ya kuinua uzalishaji wa kilimo. Pia alitaja ujenzi na upanuzi wa barabara ya Rironi-Mau Summit kama mojawapo ya miradi mikubwa inayotekelezwa na serikali ili kuboresha uchumi wa eneo hilo. Bw Wetang'ula alikosoa vikali upinzani, akidai kuwa hauna ajenda mpya zaidi ya siasa za kikabila. “Lazima tumuunge mkono Rais Ruto amalize mihula yake miwili ili akamilishe ajenda yake ya kuibadilisha Kenya,” alisema. Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa, Kimani Ichung'wah, alisema ushirikiano kati ya Kenya Kwanza na ODM umeimarisha utulivu wa kisiasa na kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo. “Tunafanya kazi pamoja kuunganisha Wakenya wakati upinzani unakosa ajenda ya kuwasaidia wananchi,” alisema. Aliongeza kuwa viongozi wengi wa upinzani waliwahi kushika nyadhifa serikalini lakini hawana rekodi ya maendeleo. Naye kiongozi wa Wengi katika Seneti, Aaron Cheruiyot, alisema viongozi wanaounga mkono serikali tayari wanaangalia siasa za baada ya mwaka 2032, wakati Rais Ruto atakapomaliza muhula wake wa mwisho kwa mujibu wa Katiba. Alimtaja Bw Wetang'ula kuwa mmoja wa viongozi wanaoweza kupewa nafasi kubwa ya uongozi baada ya Ruto kumaliza uongozi wake. “Papa wa Roma si kiongozi wa Magharibi pekee, bali ni hazina ya taifa. Rais Ruto akimaliza mihula yake miwili mwaka 2032, viongozi wa hadhi yake wataendeleza urithi huo. Lakini kwanza lazima tushinde uchaguzi wa 2027,” alisema Bw Cheruiyot. Msaidizi wa karibu wa Rais, Farouk Kibet, alisema serikali imeanza mikakati ya kuimarisha uungwaji mkono katika Bonde la Ufa na maeneo mengine nchini kabla ya uchaguzi mkuu. Aliwataka pia vijana wa kizazi cha Gen Z kumuunga mkono Rais Ruto, akidai kuwa upinzani unachochea siasa za ukabila badala ya kutoa suluhu kwa matatizo ya wananchi. "Upinzani hauna chochote cha kuwapa Wakenya isipokuwa kuwagawanya kwa misingi ya kikabila. Wapiga kura wanapaswa kuukataa katika uchaguzi wa 2027," alisema. Viongozi hao walieleza kuwa mkutano wa Eldoret ni mwanzo wa msururu wa mikutano ya kisiasa itakayofanyika kote nchini huku washirika wa Rais Ruto wakijipanga kuimarisha kampeni za uchaguzi wa 2027 na wakati huohuo kuanza kujadili siasa za urithi wa uongozi wa mwaka 2032.

from Taifa Leo https://ift.tt/qjpe7wb
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post