Mpiga mbizi hodari ambaye ameokoa maisha ya wengi baharini kwa miaka 32

BW Mohamed Salim Ahmed ni mpiga mbizi mashuhuri ambaye ametumia sehemu kubwa ya maisha yake kuitumikia jamii, taifa na mataifa ya nje.

Hata hivyo, mchango wake kwa jamii haujatambuliwa rasmi.

Bw Salim, 52, kutoka Majengo, eneobunge la Mvita, kaunti ya Mombasa, tangu akiwa kijana amekuwa akihatarisha maisha yake katika kuokoa maisha na hata kuopoa miili ya wale wanaokufa baharini.

Alikuwa kwenye kikosi cha wapiga mbizi waliojitolea kuokoa maisha, kusaka na kuopoa miili ya mamia ya wasafiri waliozama baharini kwenye mkasa wa Feri ya MV Mtongwe mwaka wa 1994.

Ajali hiyo ilisababisha vifo vya watu 272.

Wakati huo Bw Salim alikuwa akifanya kazi na kampuni ya wapigambizi ya Divecon.

“Mimi na wapiga mbizi wenzangu wapatao 14 tulifikishwa haraka kwenye eneo la mkasa. Nilikuwa mstari wa mbele kupiga mbizi tukisaka watu na kuwaokoa na pia kuiopoa miili ya wale ambao tayari walikuwa wameangamia,” akasema Bw Salim.

Shughuli hiyo ilichukuwa karibu siku saba mfululizo, usiku na mchana.

[caption id="attachment_190448" align="alignnone" width="2560"] Salim Mohamed Ahmed, 52, ambaye alikuwa miongoni mwa walioshughulikia waathiriwa wa ajali ya MV Mtongwe mnamo 1994. PICHA|KEVIN ODIT[/caption]

Mbali na Mtongwe, Bw Salim amewahi kuiwakilisha Kenya katika shughuli ya kutafuta manusura na kuopoa miili ya waliofariki kwenye majanga ya feri na meli nchi jirani za Tanzania, Zanzibar, Madagascar na kwingineko.

Anakumbuka Mei 21, 1996, wakati huo akifanya kazi na jeshi la wanamaji la Kenya kama mpiga mbizi ambapo walitumwa eneo la Mwanza, Tanzania.

Hii ni baada ya ajali ya Meli ya MV Bukoba kutokea katika Ziwa Victoria, hatua chache kabla ya kufika bandari ya Mwanza.

Meli hiyo, iliyokuwa ikitokea Bukoba, ilizama na kusababisha vifo vya watu karibu 1000 katika moja ya majanga mabaya zaidi ya usafiri wa majini kuwahi kutokea nchini Tanzania na Bara zima la Afrika kwa jumla.

Uzito wa janga hilo ulilemea nchi ya Tanzania, hali iliyomlazimu Rais Benjamin Mkapa kwa wakati huo kuitisha msaada wa wanamaji na wapiga mbizi kusaidia kwenye shughuli za uokoaji na utafutaji.

Bw Salim pia alikuwa miongoni mwa wapiga mbizi wataalamu waliofika Mwanza, Tanzania kutoa msaada wa kiufundi.

“Tulishirikiana na wenzetu kutoka Tanzania na Afrika Kusini kutafuta na kuopoa miili ya mamia ya abiria waliopoteza maisha,” akasema Bw Salim.

Anakiri kuwepo kwa mazingira magumu na changamoto tele zilizokumba shughuli hiyo.

“Meli yenyewe ilikuwa imezama umbali wa mita kadhaa ndani ya ziwa. Meli yenyewe ilikuwa na daraja la kwanza, la pili na la tatu. Wengi wa waathiriwa walikuwa wamejifungia ndani kabisa ya vyumba vya daraja la tatu, hivyo ilitulazimu kukata vyuma,kuingia ndani na kuopoa miili,” akaeleza Bw Salim.

Bw Salim anasema kuwa licha ya kutekeleza majukumu hayo mazito na ya kishujaa, serikali bado haijamtambua kwa lolote.

“Mara nyingi nimekaa kujiuliza kwani serikali inakosa shukrani? Najivunia kutekeleza majukumu ya kishujaa miaka yote ila hakuna utambuzi rasmi hadi sasa,” akasema Bw Salim.

Bw Salim kwa sasa anafanya kazi kama Afisa wa Divisheni wa Masuala ya Majanga chini ya serikali ya kaunti ya Mombasa.



from Taifa Leo https://ift.tt/3kqsvo9
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post