Kitendawili cha afisa wa GSU katika mauaji ya mwalimu Albert Ojwang

MMOJA wa washukiwa wanaohusishwa na mauaji ya Albert Ojwang’ ni afisa wa Kikosi cha polisi cha kupambana na fujo (GSU) aliyehepa kazi na ambaye alikuwa amekamatwa kwa kushukiwa kutekeleza mauaji mengine. Ojwang atazikwa Julai 4, familia yake ilitangaza Jumanne wakati ambao washukiwa wa mauaji yake walisomewa mashtaka. Upande wa mashtaka ulipokuwa ukipinga kuachiliwa kwa washukiwa sita wa mauaji ya Ojwang, akiwemo aliyekuwa Afisa Mkuu wa kituo cha Central, Nairobi (OCS), Samson Tallam, baada yao kukana kumuua Ojwang’, mahakama ilifahamishwa kuwa, John Ngige Gitau ni askari wa GSU aliyehepa kazi. Kiongozi wa mashtaka, Duncan Ondimu, alisema Gitau alikuwa akichunguzwa kwa mauaji mengine na alikuwa amezuiliwa kituoni uchunguzi ukiendelea. “Uchunguzi umebaini kuwa Gitau, akiwa mahabusu, alikuwa akiheshimiwa na mahubusu wengine na ana uwezo wa kuingilia mashahidi waliokuwa mahabusu wakati wa tukio hilo, jambo ambalo linaongeza hatari ya kuingilia na kutisha mashahidi iwapo ataachiliwa kwa dhamana,” alisema Bw Justin Nyatete katika hati ya kiapo. Bw Tallam, pamoja na maafisa wengine wawili wa polisi, James Mukhwana na Peter Kimani, Gitau, Gin Ammitou Abwao na Brian Mwaniki, walikana kuwa walimuua Ojwang’ usiku wa Juni 8 na 9 2025 ndani ya seli ya kituo cha polisi cha Central, Nairobi. Mara tu walipokana mashtaka, upande wa mashtaka uliomba Jaji wa Mahakama Kuu Diana Kavedza asiwaachilie washukiwa kwa dhamana, akisema kuna hatari ya kuingilia mashahidi na hata kutoroka nchi kutokana na uzito wa kesi hiyo. Bw Nyatete, afisa mkuu wa uchunguzi kutoka Mamlaka Huru ya Kuchunguza Utendakazi wa polisi Polisi (IPOA), alisema Tallam alikuwa msimamizi wa rekodi za CCTV katika kituo hicho wakati wa tukio.

from Taifa Leo https://ift.tt/I5NymLk
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post