
KUMBUKUMBU za maandamano ya mwaka jana bado ni kidonda kisichopona kwa Brian Mwangi, kijana mwenye umri wa miaka 29 na waathiriwa wenzake wa ukatili wa polisi. Mwangi alijeruhiwa kwa risasi siku hiyo, na sasa anaishi na shangazi yake eneo la Ruiru, akimtegemea binamu yake wa kiume kumbadilisha nepi, kumuosha na kumvisha. Muuguzi huja mara kwa mara kutibu vidonda vyake na kubadilisha mpira wa mkojo, huku shangazi na mjomba wake wakigharimia kila kitu katika maisha yake. Mwangi anakumbuka uhuru aliokuwa nao awali alipokuwa akifanya vibarua vya kutengeneza matairi ya magari, kunyoa nywele kama kinyozi wa kujitegemea, na mara nyingine kuosha magari mjini Karatina. Kwa sasa, kiti cha magurudumu alichonunuliwa na marafiki kutoka Karatina ndicho tu kinachomruhusu kutembea katika boma la shangazi yake. Siku ya tukio, alipoteza fahamu baada ya kupigwa risasi, na alizinduka saa tatu usiku akiwa katika Hospitali ya Karatina. Aliomba wahudumu wa hospitali wamjulishe shangazi yake. Baada ya siku mbili, alihamishiwa Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH), ambako alisubiri zaidi ya miezi saba ili kufanyiwa upasuaji wa kuondoa risasi iliyokwama kwenye uti wa mgongo wake. “Upasuaji ulicheleweshwa kwa sababu nilikuwa na vidonda vilivyohitaji kupona kwanza. Madaktari walikuwa na wasiwasi, wakasema ilikuwa hatari mno. Lakini niliamua kubeba hiyo hatari – nikawaambia waiondoe risasi,” anakumbuka Mwangi. “Risasi hiyo ilinijeruhi vibaya sana. Sifanyi chochote tena mwenyewe. Hicho ndicho serikali ilinifanyia,” anasema kwa uchungu. Shangazi yake, Bi Esther Mwangi, ambaye sasa ni mlezi wake pamoja na dada yake, anaelezea hali ngumu ya kifedha wanayopitia. “Tunamnunulia nepi kila baada ya siku tano, pakiti moja ni Sh1,000. Tunamlipa muuguzi anayekuja kila baada ya siku mbili kumtibu. Tunagharamia usafiri kwenda na kurudi kliniki, na kila mwezi tunahudhuria kliniki KNH ambapo tunakodi teksi kwa angalau Sh6,000,” asema Bi Esther. Anaeleza kuwa alipokea simu kutoka Mamlaka Huru ya Kuchunguza Utendakazi wa Polisi (IPOA), waliotaka majina yake na ya Brian pamoja na uhusiano wao. Pia waliuliza kuhusu iwapo risasi ilihifadhiwa na hospitali. “Niliwaambia hospitali ilihifadhi. Kisha simu ikakatika.” Mtaani Githurai, Samuel Kinyanjui naye alipigwa risasi Julai 16. Akiwa mhasibu na mwalimu wa shule ya upili, alijiunga na maandamano baada ya kutoka nyumbani saa tisa alasiri. Polisi walitawanya maandamano kwa vitoa machozi, hali iliyowachochea wakazi kuungana, na umati mdogo ukageuka maandamano makubwa. Alipokea simu muhimu na akajitenga na umati kuijibu. Hapo ndipo alihisi maumivu makali pajani. “Niliona shimo kwenye paja langu la kulia, damu ikitiririka. Nikagundua nimepigwa risasi,” asema. Alikimbizwa KNH, ambapo siku iliyofuata alipelekwa chumba cha upasuaji. Daktari alimwambia kuwa risasi ilipasua mfupa na walifanikiwa kutoa vipande viwili pekee, kilichosalia hakikuweza kutolewa. “Hadi leo, X-ray inaonyesha risasi bado ipo. Naweza kuisikia chini ya ngozi,” asema. Hajawahi kuhudhuria kliniki kwa ukosefu wa pesa. Mke wake, aliyekuwa mjamzito wakati huo, alirudi kwao baada ya yeye kushindwa kumhudumia. “Bado sijamuona mwanangu. Maisha yangu yamefungwa ndani. Nahitaji Uber kutembea. Natumia sindano kila siku.” Kinyanjui anaomba msaada wa upasuaji kuondoa risasi na kurekebisha mguu wake. “Nataka hata robo ya maisha yangu niliyokuwa nayo,” anasema kwa huzuni. Rodgers Mwabe, fundi wa Jua Kali jijini Nairobi, alipoteza mguu wake katika maandamano ya Gen Z. Mnamo Juni 25 2024 akiwa Kahawa Sukari alipigwa risasi na kupelekwa Hospitali ya Thika Level 5, kisha KNH ambako alikumbana na taarifa mbaya – mguu wake ulikatwa kwa kuchelewa kupata huduma. “Asubuhi nilipoamka, niliambiwa mguu haungepona ,ulikuwa umekatwa. Nilijua maisha yangu yameisha,” asema Mwabe. Watoto wake walimuuliza mguu uko wapi. “Niliwaambia nimeuacha hospitali, nitarudi kuuchukua. Lakini moyoni nilijua si kweli.” Safaricom ilimpatia mguu wa bandia, lakini hali ya ngozi yake humzuia kuutumia mara kwa mara. Hata hivyo, bado anatamani kukutana na Mkurugenzi Mkuu wa Safaricom Peter Ndegwa, ili kudai marupurupu aliyokuwa ameahidiwa. Tobius Thuo, mwenye miaka 23, alipigwa risasi kwenye paja la kushoto alipokuwa akishiriki maandamano. Alifanyiwa upasuaji katika KNH, lakini sasa hawezi tena kucheza muziki kama hapo awali, jambo lililoathiri taaluma yake ya usanii. “Nilidhani ni kitoa machozi. Kumbe ilikuwa risasi. Nilihisi damu ikitiririka,” anakumbuka. Alipewa huduma ya kwanza katika Holy Family Basilica na baadaye akapelekwa KNH kwa upasuaji. Mwabe, Thuo, Mwangi na Kinyanjui wote wanatoa wito wa haki na fidia kutoka kwa serikali. Wanasisitiza kuwa hawakustahili kupigwa risasi. “Tuko tayari hata kurudi barabarani leo hii, Juni 25, kuadhimisha mwaka mmoja wa maumivu, mateso, na makovu ya maisha. Tunatafuta haki,” wanasema kwa sauti moja.
from Taifa Leo https://ift.tt/8lZ7JDV
via
IFTTT