Ruto: Serikali yangu ni ‘kazi bila break’ na kazi yenyewe itanipa ‘TuTam’

RAIS William Ruto ametetea rekodi ya serikali yake akitaja mipango kadhaa ya maendeleo inayotekelezwa kwa nia ya kuimarisha maisha ya Wakenya. Akiongea Jumapili alipoongoza makala ya 62 ya sherehe za Madaraka Dei katika Kaunti ya Homa Bay, Dkt Ruto alisema kuwa ufanisi katika utekelezaji wa mipango hiyo ya maendeleo ni ithibati kuwa sera yake ya kuchochea maendeleo kuanzia mashinani (BETA- ‘bottom up’) inafanya kazi jinsi ilivyokusudiwa. Kiongozi wa taifa aliweka wazi mafanikio ya serikali yake katika sekta za afya, kilimo, elimu, biashara, uchumi wa majini, miongoni mwa nyingine, aliyosema umechangia kuimarisha maisha ya raia. “Leo sera ya maendeleo ya BETA siyo kauli mbiu tu, bali ni halisi kwa sababu inabadilisha maisha ya Wakenya kote nchini siku baada ya siku. Ikiwa haukuelewa maana ya ‘bottom up’, sasa unaelewa kwa sababu unaona matunda yake maishani mwako,” Rais Ruto akaeleza kwenye hotuba yake katika uwanja wa Raila Odinga mjini Homa Bay. Kiongozi wa taifa alisema kuwa kutokana na sera bora za kiuchumi zilizotekelezwa na serikali yake tangu Septemba 13, 2022, kiwango cha mfumko wa bei kimeshuka pakubwa kufikia Mei, 2025. Pia Rais Ruto alisema thamani ya shilingi ya Kenya imeimarika kutoka Sh162 kwa dola moja ya Amerika mnamo Oktoba 2022, hadi Sh129 wakati huu, hali ambayo imepunguza gharama ya uzalishaji na uendeshaji biashara. Rais Ruto alisema kuwa baada ya serikali yake kuanzisha mpango wa utoaji mbolea kwa bei nafuu, gharama ya uzalishaji katika sekta ya kilimo imepungua kwa kima cha asilimia 50. “Na matokeo yake ni ongezeko la uzalishaji wa mahindi, majanichai na kahawa hali ambayo imewaongezea wakulima wetu faida na kuchangia azma yetu ya kujitosheleza kwa chakula,” akasema. Kiongozi wa taifa pia alitaja mageuzi ambayo serikali yake imetekeleza katika sekta ya maziwa yaliwezesha wakulima kulipwa Sh50 kwa lita moja ya maziwa. “Kabla ya hapo wakulima wetu walikuwa wakilipwa Sh35 kwa lita ya maziwa waliyokuwa wakiwasilisha kwa kampuni za maziwa,” Dkt Ruto akasema. Rais pia alitumia fursa hiyo kutetea sera yake ya ukodishaji wa kampuni nne za kutengeneza sukari. “Lengo letu ni kuhakikisha kuwa wakulima na wafanyakazi wanalipwa kwa wakati na pia uzalishaji wa sukari kwa wingi. Kampuni hizi zilikuwa mzigo kwa serikali kuu na hazikuwa zikizalisha sukari ipasavyo; hali hiyo itabadilika sasa,” Dkt Ruto akaeleza. Kampuni zilizokodishwa kwa wawekezaji wa kibinafsi ni pamoja na; Nzoia iliyoko Bungoma, Sony (Migori) na kampuni za Chemelil na Muhoroni zilizoko Kaunti ya Kisumu. Rais Ruto pia aliangazia ufanisi wa mpango wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu (AHP) akitaja kukamilishwa na kupokezwa kwa nyumba hizo katika kaunti za Nairobi na Homa Bay. “Juzi, ilikuwa furaha yangu kupokeza jumla ya nyumba 1080 kwa wakazi wa Mukuru, Nairobi na nyumba nyingine hapa Homa Bay, na Kisumu. Siku zijazo nitapokezana nyumba nyingine katika kaunti za Nakuru, Migori, Kakamega, Vihiga, Nandi na Nanyuki,” akasema huku akielezea furaha yake kuona familia zinazoishi katika mitaa duni zikiisha katika nyumba bora. Rais Ruto pia alitangaza kuwa serikali itawasilisha bungeni mswada wa mageuzi ya sheria ili kuwezesha wanaochangia ushuru wa nyumba kupata mikopo ya hadi Sh5 milioni ili kuweza kununua nyumba hizo. “Mikopo kama hii ya gharama nafuu itawawezesha watu wengi kununua nyumba hizo za gharama nafuu kote nchini,” Rais Ruto akaeleza. Kuhusu mpango wa afya kwa wote (UHC), Rais Ruto alisema kuwa changamoto ambazo zilikuwa zikikumba utendakazi wa Mamlaka ya Bima ya Afya ya Kijamii (SHA) sasa hazipo tena, huku Wakenya wengi wakiendelea kujisajili kwa bima hiyo. “Habari ninayopokea ni kwamba SHA sasa inafanya kazi ipasavyo. Matatizo yaliyoshuhudiwa kuanzia Oktoba mwaka jana sasa hayapo na Wakenya wanapata huduma za afya kwa gharama nafuu,” Rais Ruto akaeleza. Kiongozi wa taifa alitangaza kuanzisha kwa mfumo utakaowawezesha Wakenya kulipa michango yao kwa SHA, kwa awamu, kama njia ya kuwapunguzia gharama. Huduma hiyo kwa jina, ‘Lipa SHA Pole Pole' inapatikana kwa njia ya simu ya mkono kwa kubonyeza *147# na unalenga kufaidi Wakenya wenye mapato ya chini. “Kupitia mfumo huu, Wakenya wataweza kupata matibabu kwa wakati,” Rais Ruto akasema huku akiwahimiza raia kuendelea kujiandikisha kwa SHA. Rais Ruto pia alitangaza mpango kwa jina, NYOTA, unaofadhiliwa na serikali pamoja na Benki ya Dunia kwa lengo la kutoa mafunzo ya biashara kwa vijana. Chini ya mpango huo, vijana pia watapata ruzuku za kupiga jeki biashara zao. “Tumetenga Sh5 bilioni kama ruzuku zitakazoelekezwa kuwasaidia jumla ya vijana 100,000, kila mmoja akipokezwa Sh50,000 za kuanzishia biashara baada ya kupewa mafunzo. Mpango huu unaojulikana kama NYOTA, unaanza kutekelezwa Agosti mwaka huu,” Rais Ruto akasema. Kiongozi wa taifa pia alitangaza kuwa mpango wa kazi kwa vijana, maarufu kama ‘Climate Works’ utatekelezwa katika kaunti zingine 46 kote nchini baada ya mpango huo kufanikiwa katika kaunti ya Nairobi. “Jumla ya vijana 110, 000 wataajiriwa kufanya kazi kama vile ujenzi wa barabara, upanzi wa miti na udumishaji usafi mijini na vijijini,” Dkt Ruto akasema. “Kwa hivyo, vijana mjipange baada ya majuma mawili mtaanza kusajiliwa kwa kazi mtaani ambayo sasa inajukulika kama Climate Works,” kiongozi wa taifa akaeleza. Kuhusu miundomsingi, Rais Ruto alisema kuwa mradi wa upanuzi wa barabara ya Rironi-Mau Summit utaanza kutekelezwa Julai mwaka huu. Vile vile, akaeleza, mpango wa utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Naivasha hadi Malaba umekamilishwa.

from Taifa Leo https://ift.tt/W5Vor7a
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post