
KWA karibu miaka miwili, pikipiki moja ilionekana kutoweka kabisa, angalau kwenye rekodi rasmi za kampuni ya kukopesha.
Iliripotiwa kuibwa mapema mwaka wa 2023, na mteja aliyeichukua kwa mkopo alieleza kuwa ilipotea katika mazingira yasiyoeleweka, kama ilivyo kwa visa vingi vya wizi wa bodaboda vinavyoripotiwa kila mara Kenya.
Kesi hiyo iliwekwa katika faili ya kawaida ya pikipiki zilizopotea, bila matarajio makubwa ya kupatikana.
Hata hivyo, ukweli ulijulikana baadaye kwa njia ya kushangaza. Mwaka wa 2025, pikipiki hiyo hiyo iliibuka tena wakati mmiliki wake wa awali alipojaribu kuiuza kwa siri kwa mnunuzi mpya.
Hatua hiyo ilizua shaka, na ikachochea msururu wa uchunguzi uliowezesha maafisa wa kurejesha mali za kampuni ya Watu-Kenya, kwa kushirikiana na polisi na wanunuzi waliotoa taarifa, kuifuatilia hadi ilikofichwa.
Operesheni ya kuirejesha haikuwa rahisi. Wakati waliotumwa kuitwaa walipofika, mmiliki alijaribu kuzua upinzani ili kuzuia pikipiki hiyo kuchukuliwa.
Hata hivyo, jaribio hilo lilishindwa, na pikipiki ikapatikana ikiwa salama na kurejeshwa kwa kampuni iliyomkopesha.
Kilichokuwa kimechukuliwa kama wizi kiligeuka kuwa kisa cha udanganyifu uliofichuliwa. Uchunguzi zaidi umeonyesha kuwa kisa hiki si cha kipekee.
Kwenye sekta ya ufadhili wa pikipiki nchini Kenya, kumekuwa na ongezeko la visa ambapo wateja wanaodai kuwa waathiriwa wa wizi baadaye hugunduliwa kuwa walihusika moja kwa moja katika kupotea kwake.
Kwa mujibu wa data, baadhi ya pikipiki “zilizoripotiwa kuibwa” huwa zimefichwa, zimeuzwa kimya kimya, au zimebadilishwa ili kuepuka mikopo.
Mbinu zinazotumika ni pamoja na kubadilisha namba za usajili, kuficha pikipiki maeneo ya mbali, au kuziuza katika soko lisilo rasmi.
Katika kisa kimoja, pikipiki iliyochukuliwa kwa mkopo iliripotiwa kuibwa miezi michache baada ya ununuzi.
Baadaye iligunduliwa kuwa ilibadilishwa namba za usajili na kuuzwa kwa mtu mwingine kabla ya kurejeshwa tena baada ya uchunguzi wa kina.
Kuna pia visa vinavyohusisha familia. Katika kesi inayoendelea katika Mahakama ya Thika, uchunguzi ulibaini kuwa baba na mwana walishirikiana kupanga “wizi” wa pikipiki, kisha wakaripoti kwa polisi ili kuficha ukweli na kuepuka kulipa mkopo.
Wote wawili walikamatwa baada ya pikipiki kufuatiliwa kupitia kifaa cha GPS.
Katika kaunti ya Kitui, kisa kingine kilibainika ambapo pikipiki ilifichwa kwenye shimo nyuma ya nyumba kwa miezi kadhaa kabla ya kugunduliwa wakati mgogoro wa kifamilia ulipoibuka na mke kufichua siri hiyo kwa polisi.
Wataalamu wanasema sababu kuu ya vitendo hivi ni shinikizo la kifedha.
Mfumo wa mikopo ya pikipiki unaotegemea malipo ya kila siku huweza kuwa mzigo kwa baadhi ya wateja, na kuwafanya wachukue hatua za kukwepa deni kwa njia za udanganyifu.
from Taifa Leo https://ift.tt/eGhWBi7
via IFTTT