Jinsi Ruto alivyoingiza ODM kwenye mtego

Ilianza kwa mikutano ya chinichini na ishara za kisiasa za heshima, kisha ukafuata uteuzi wa wanachama wa upinzani katika Baraza la Mawaziri, na baadaye majukwaa ya pamoja ya kisiasa. Leo, Chama cha Orange Democratic Movement (ODM) kinakabiliwa na swali gumu: je, kiliingia kwa hiari kwenye mtego wa kisiasa uliowekwa na mpinzani wake wa muda mrefu, Rais William Ruto? Kwa miongo kadhaa, ODM kilikuwa ngome kubwa ya upinzani nchini Kenya, kikijengwa juu ya uongozi thabiti wa mwanzilishi wake marehemu Raila Odinga. Hata hivyo, urithi huo sasa uko katika mtihani, chama kikikabili changamoto za ushirikiano wa kisiasa unaosemekana kukipunguzia nguvu. Mnamo Alhamisi, Kamati Kuu ya ODM ilitoa taarifa kali ikitaka “heshima” kutoka kwa washirika wake, ishara kuwa mambo si shwari ndani ya ushirikiano huo mchanga. “Kuhusiana na ushirikiano wetu na mshirika wetu katika serikali Jumuishi, UDA, Kamati Kuu imeeleza wasiwasi kuhusu matamshi ya baadhi ya viongozi wakuu wa UDA ambayo yameacha wanachama wetu wakiwa na taharuki,” chama kilisema. Lakini kabla ya mazungumzo rasmi ya muungano wa 2027, vyama hivi viwili vilikuwa tayari vimeanza kukaribiana kimyakimya kupitia mikutano isiyo rasmi, ikiwemo hafla kubwa ya ODM Mombasa ambayo inasemekana ilikuwa na baraka za Ikulu. Baada ya hapo, kauli mbiu mpya iliibuka ndani ya ODM: “Tutam”—ikimaanisha kumuunga mkono Rais Ruto, kabla hata ya mazungumzo rasmi ya muungano. Baadhi ya wachambuzi wanasema hali hiyo ilikuwa ya kushangaza kwa chama kilichojengwa juu ya msingi wa siasa za upinzani. Gavana wa Siaya James Orengo alikuwa miongoni mwa waliotoa onyo  mapema, akisema ODM ilikuwa ikipoteza mwelekeo wake wa kiitikadi kwa “kusifia serikali kupita kiasi”. Lakini mvuto wa Ikulu uliendelea kuongezeka. Hatua kubwa zaidi ilikuja pale Rais Ruto alipowateua viongozi kadhaa wa ODM katika Baraza la Mawaziri, akiwemo Hassan Joho, Wycliffe Oparanya, Opiyo Wandayi, John Mbadi na Beatrice Askul. Hapo ndipo wachambuzi wanasema hatua ya “kuvutwa ndani” ilianza kwa kasi, badala ya mapambano ya moja kwa moja. Baada ya kifo cha Raila Odinga, changamoto ndani ya ODM ziliongezeka, huku mgawanyiko wa uongozi ukionekana wazi zaidi. Uongozi ulichukuliwa na Oburu Oginga, lakini mabadiliko hayo yalifichua mipasuko ya ndani. Baadhi ya shughuli za chama zilianza kupata msaada wa kiufundi na kifedha kutoka vyanzo vya serikali, hali iliyozua maswali mapya kuhusu uhuru wa ODM. Wakati huo, mgawanyiko mpya uliibuka ndani ya chama kati ya makundi mawili—“Linda Ground” na “Linda Mwananchi”—kila moja likidai kuwakilisha misingi halisi ya ODM. Katika hatua nyingine, viongozi wa chama walianza kugawanyika kuhusu mwelekeo wa 2027, baadhi wakisisitiza ODM ipate wadhifa wa juu kama urais au makamu wa rais katika muungano wowote. Lakini kauli hizo zilianza kubadilika mara kwa mara, hali inayoonyesha kutokuwa na msimamo thabiti wa kisiasa. Rais Ruto naye ameendelea kutetea ushirikiano huo, akisema Kenya inahitaji vyama hivi kufanya kazi pamoja kwa manufaa ya taifa. Hata hivyo, ndani ya UDA, viongozi kama Hassan Omar wamepinga pendekezo la “  kuhifadhi ngome”, wakisisitiza ushindani wa moja kwa moja katika uchaguzi. Hali hii imezua mvutano mpya, huku ODM ikisisitiza kulinda ngome zake za Nyanza, Magharibi, Pwani na Nairobi. Lakini wachambuzi wanasema hatua ya kufungua milango ya ushirikiano na serikali tayari imebadilisha hali ya kisiasa. Kwa mujibu wa baadhi ya wataalamu, Ruto ameweza kufanikisha jambo muhimu: kudhoofisha upinzani mkuu bila vita vya moja kwa moja, kwa kuuvuta ndani ya mfumo wake wa serikali. Huku uchaguzi wa 2027 ukikaribia, ODM sasa inakabiliwa na uamuzi mgumu wa kuendelea kushirikiana na serikali au kujiondoa na kurudi upinzani kamili.

from Taifa Leo https://ift.tt/7tUndAc
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post