
MZOZO wa mafuta unaoendelea nchini pamoja na mgomo wa sekta ya uchukuzi umeanza kuibua maswali kuhusu uwezo wa baadhi ya viongozi wa ODM waliojiunga na serikali ya Rais William Ruto chini ya serikali Jumuishi.
Mawaziri John Mbadi wa Fedha, Opiyo Wandayi wa Kawi, Wycliffe Oparanya wa Ushirika, Hassan Joho wa Madini na Uchumi wa Bahari pamoja na Beatrice Askul wa Maendeleo ya Ukanda waliingia serikalini wakitajwa kama “wataalamu” waliotarajiwa kusaidia utawala wa Kenya Kwanza kukabiliana na changamoto za kiuchumi na kisiasa baada ya maandamano ya Gen Z mwaka 2024.
Hata hivyo, mzozo wa sasa wa mafuta umeonekana kuwa jaribio gumu kwa baadhi yao, hasa Mbadi na Wandayi ambao walionekana kushindwa kutoa suluhu ya haraka huku wananchi wakitarajia majibu kutoka kwao.
Wachambuzi wanasema mazungumzo ya Jumatatu kati ya serikali na wadau wa sekta ya uchukuzi yalifichua udhaifu wa viongozi hao baada ya juhudi zao za kumaliza mgomo kugonga mwamba hadharani.
Katika mkutano huo, Waziri Wandayi alitangaza mapema kuwa kulikuwa na makubaliano, lakini viongozi wa sekta ya uchukuzi walimpinga mbele ya wanahabari wakisema hakukuwa na mwafaka uliokuwa umefikiwa.
“Hatukukubaliana chochote,” alisema Kennedy Kaunda, mmoja wa viongozi wa vyama vya wafanyakazi wa sekta ya uchukuzi.
Kwa upande wake, Mbadi alionekana kushindwa kutoa suluhu zaidi ya kueleza kuwa sababu za kupanda kwa bei ya mafuta ziko nje ya uwezo wa serikali.
Baada ya mazungumzo ya kwanza kufeli, Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja aliingilia kati kusaidia kupatanisha serikali na wahudumu wa matatu, hatua iliyosaidia kufikiwa kwa makubaliano ya kusitisha mgomo kwa wiki moja.
Seneta wa Kakamega Boni Khalwale alisema Mbadi na Wandayi wanapaswa kuondoka serikalini kutokana na changamoto za mafuta na madai ya kuingia kwa mafuta duni sokoni.
Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wamewatetea mawaziri hao wakisema waliingia katika serikali iliyokuwa tayari na matatizo mengi ya kiuchumi.
Kiongozi wa vijana wa ODM John Ketorah alisema kupanda kwa bei ya mafuta ni tatizo la kimataifa na halipaswi kutumiwa kisiasa kuwalaumu viongozi hao pekee.
Mzozo huo sasa umegeuka kuwa mtihani mkubwa kwa serikali ya Kenya Kwanza huku wananchi wakisubiri kuona iwapo “wataalamu” waliotajwa wataweza kutoa suluhu ya kudumu kwa gharama ya maisha inayozidi kupanda.
from Taifa Leo https://ift.tt/WKP3h6j
via IFTTT