Upinzani waunga tikiti ya Kalonzo-Matiang’i kubwaga Ruto 2027, utafiti wasema

WAFUASI wa upinzani wanapigia debe tikiti ya Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka na aliyekuwa Naibu Rais Dkt Fred Matiangí kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Kulingana na kura ya maoni iliyotolewa Alhamisi na Tifa, kuibuka kwa Katibu Mkuu wa ODM, Edwin Sifuna hata hivyo kunaweza kusababisha mabadiliko makubwa ya kisiasa ndani ya upinzani.

TIFA pia imeonyesha kuwa Rais William Ruto anakabiliwa na kibarua kigumu katika kutetea kiti chake, kwani upinzani ulioungana unaweza kumshinda kwa urahisi.

Hata kama upinzani utasalia kugawanyika, bado unaweza kumzuia Rais Ruto kufikia hitaji la asilimia 50 pamoja na kura moja kwa mwaniaji wa urais kushinda katika duru ya kwanza.

Akizungumza wakati wa kutolewa rasmi kwa matokeo ya kura hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TIFA Tom Wolf, alisema wengi wa wafuasi wa upinzani wanampendelea Bw Musyoka kuwa mgombea wa urais huku Dkt Matiang’i, akiwa mgombea mwenza wake. Tiketi ya Kalonzo-Matiang’i ilipata uungwaji mkono wa asilimia 31.

Kwa upande mwingine, tiketi ya Kalonzo-Sifuna, ambayo pia imekuwa ikichangamkiwa na baadhi ya wafuasi wa upinzani ni ya pili kwa asilimia 28.

Bw Musyoka amekuwa akizunguka ngome yake ya Ukambani pamoja na Kinara wa DCP Rigathi Gachagua, huku baadhi ya mikutano yao ya pamoja ikifasiriwa kama inayotumika kumuidhinisha kisiasa.

Mnamo Machi 30, wakati wa ziara ya pamoja ya viongozi wa upinzani katika Ukambani, Bw Gachagua aliwahimiza Wakamba kujisajili kwa zaidi ya kura milioni nne ili kumwezesha Bw Musyoka kuingia Ikulu mnamo 2027.

Hata hivyo, aliyekuwa Naibu Rais anaonekana kutokuwa na imani kwa Dkt Matiang’i, ambaye anaungwa mkono na chama cha Jubilee kinachohusishwa na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta.

Ushindani kati ya wawili hao unaonekana kujikita zaidi katika siasa za eneo la Mlima Kenya, ambalo DCP inaliona kuwa ngome yake ya kisiasa.

Tiketi ya Kalonzo-Sifuna pia imeendelea kupata nguvu, huku katibu huyo mkuu wa ODM akitangaza kuwa yuko tayari kufanya kazi ndani ya muungano wa upinzani ulioungana.

Wakati wa ziara ya kisiasa ya hivi majuzi katika Kaunti ya Homa Bay, Bw Musyoka alidokeza kuwa mrengo wa Linda Mwananchi unaoongozwa na Bw Sifuna utajiunga nao hapo mbeleni.

Siasa za Bw Sifuna zinaonekana kuchangamkiwa sana na vijana akihurumiwa kwa mateso ambayo amekuwa akiyapitia ndani ya ODM.

Pia ameanza kupata uungwaji mkono katika eneo la Magharibi mwa Kenya, huku baadhi ya wafuasi wakimtaka agombee urais 2027.

Tiketi ya Rigathi Gachagua na Kalonzo Musyoka ilipata asilimia 25, huku tiketi ya Kalonzo Musyoka na Martha Karua ikipata asilimia nne pekee.

Cha kushangaza ni kuwa, wafuasi wengi wa Rais Ruto wangependelea akabiliane na tiketi ya Kalonzo-Sifuna, ambayo ilipata asilimia 19 miongoni mwao huku ile ya Kalonzo-Matiang’i ikipata asilimia 18.

Huku upinzani ukiendelea kuhangaika kuungana, Rais Ruto pia hayuko pazuri kisiasa. Kwa mujibu wa TIFA, dalili zote zinaonyesha kuwa ushindi wa duru ya kwanza unaweza kuwa mgumu kwake.

Ingawa uungwaji mkono kwa Rais umepanda hadi asilimia 24 kutoka asilimia 19 kutoka Novemba 2025 wakati kura ya mwisho ilifanyika, bado hawezi kushinda katika duru ya kwanza.

Kuhusiana umaarufu wa jumla, Bw Musyoka anaongoza miongoni mwa wanaotajwa kuwania urais kwa tiketi ya upinzani kwa asilimia 19, akifuatiwa na Dkt Matiang’i kwa asilimia 14 kisha Bw Sifuna ana asilimia 10.

Umaarufu wa Bw Musyoka umeshuka kutoka asilimia 25, huku wa Dkt Matiang’i pia ukipungua.

Ndani ya ODM, mrengo wa Linda Mwananchi unaonekana kuwa maarufu zaidi miongoni mwa wafuasi wake kuliko mrengo wa Linda Ground unaoongozwa na Seneta wa Siaya, Dkt Oburu Oginga.

Linda Mwananchi inaungwa mkono na asilimia 73, ikilinganishwa na asilimia 23 tu kwa Linda Ground, huku asilimia tatu pekee ya wafuasi wa ODM wakisema bado hawajaamua ni upande gani wa kuunga mkono.



from Taifa Leo https://ift.tt/Et92ibl
via IFTTT

Post a Comment

Previous Post Next Post